Habari

1,500 hatihati kufanya mtihani Chuo Kikuu kesho

Zaidi ya wanafunzi 1,500 wa Chuo Kikuu cha St. Augustine cha jijini Mwanza (SAUT) wanaodhaminiwa na serikali, wako katika hatihati ya kutofanya mitihani yao ya muhula wa kwanza inayoanza kesho kwa madai kwamba Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu haijakamilisha ada.

Na Richard Makore
Zaidi ya wanafunzi 1,500 wa Chuo Kikuu cha St. Augustine cha jijini Mwanza (SAUT) wanaodhaminiwa na serikali, wako katika hatihati ya kutofanya mitihani yao ya muhula wa kwanza inayoanza kesho kwa madai kwamba Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu haijakamilisha ada.

 

Hata hivyo, Bodi hiyo imeutaka uongozi wa chuo hicho kutowazuia wanafunzi hao kwa kuwa hilo siyo kosa lao.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa bodi hiyo, Bw. George Nyatega wakati akizungumza na Nipashe ofisini kwake.

 

Alitoa agizo hilo baada ya kuwepo kwa tishio la kutoruhusiwa kufanya mitihani ya muhula wa kwanza kwa wanafunzi hao wa mwaka wa kwanza na wa pili kwa sababu Bodi haijakamilisha sehemu ya ada yao.

 

Bw. Nyatega alisema, kuchelewa kulipiwa kwa wanafunzi hao, kumesababishwa na dosari iliyofanywa na chuo chenyewe kwa kuchelewesha kuwasilisha fomu maalum za malipo (Invoice) kwa Bodi ili ziweze kuandaliwa hundi ya malipo.

 

Alisema walipokea fomu ya malipo Januari 9, mwaka huu kutoka chuo hicho kwa ajili ya malipo ya wanafunzi wa mwaka wa pili na wa tatu, jambo ambalo ni vigumu kuandaa hundi hiyo katika kipindi hicho kifupi.

 

Alikiagiza chuo hicho kutowazuia wanafunzi hao ambao wanatarajia kuanza mitihani yao kesho kwani kosa hilo siyo lao bali ni la uongozi wa chuo.

 

Hata hivyo, alikiri kupokea fomu ya malipo ikiwa na idadi ya wanafunzi wanaotakiwa kulipiwa na kiasi cha fedha kwa kila mwanafunzi.

 

Bw. Nyatega alifafanua kuwa, kama Bodi imekubali kulipa malipo hayo kwa wanafunzi inayowadhamini, hakuna sababu kwa chuo kuendelea kuwasumbua na kuwazuia wanafunzi kufanya mitihani.

 

“Sisi hatuna makosa yoyote, tupo hapa ofisini kusubiri Invoice kutoka kwa kila chuo lakini hawa SAUT, walileta yao Januari 9, mwaka huu na kesho ndiyo mitihani inaanza,“ alisema.

 

Alifafanua kuwa, baada ya kupokea fomu hizo za malipo, hulazimika kuzihakiki kwa kupitia majina yaliyotumwa na chuo na kwamba kazi hiyo inahitaji muda na sio ya ghafla.

 

Bw. Nyatega aliahidi kuwa, bodi yake itakilipa chuo hicho fedha wanazodai lakini kwa sasa kinapaswa kuwaruhusu wanafunzi wao kufanya mitihani.

 

Aliongeza kuwa, baadhi ya vyuo mbalimbali hapa nchini huchelewesha kuwapelekea fomu za malipo na mara wanapozituma, huwatangazia wanafunzi kwamba asiyelipa ada hatafanya mtihani.

 

Mkurugenzi huyo alisema, wanafunzi wengi wanadhani Bodi ndiyo yenye makosa siku zote kumbe tatizo kubwa husababishwa na vyuo vyao.

 

Alisema anashangaa kuona vyuo vinashindwa kufuata utaratibu wakati walikaa na wakuu wa vyuo husika pamoja na wakuu wa idara na kuwaeleza taratibu za kufuata ili kupata malipo kutoka Bodi ya Mikopo.

 

Awali, taarifa zilizopatikana SAUT jijini Mwanza zilieleza kuwa, wanafunzi zaidi 1,500 wako katika hatihati ya kutofanya mitihani ya muhula inayoanza kesho kutokana na kudaiwa ada.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents