Habari

Acheni kuajiri watoto kwenye mashamba ya tumbaku – Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa mkoa wa Tabora kuwapeleke watoto wao shule na kuacha kuwatumia kama vibarua kwenye mashamba ya tumbaku.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na watumishi wa idara za kilimo na ushirika na viongozi wa wilaya ya mkoa huo kwenye kikao alichokiitisha ili awape maagizo maalum.

“Ninasisitiza kuanzia sasa jamii iwapeleke watoto shule kuanzia elimu ya awali hadi sekondari na tuache kuwatumia watoto wadogo kama vibarua kwenye mashamba ya tumbaku. Wakuu wa wilaya simamieni eneo hili la kuondoa watoto kwenye ajira,” alisema Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo pia kusisitiza viongozi wa mkoa huo wasimamie elimu ya mtoto wa kike na kuhakikisha kuwa wanahitimu elimu ya sekondari.

“Kuna tatizo la mimba kwa watoto wa shule. Eneo hili pia linahitaji usimamizi ili kuwalinda watoto wa kike wamalize elimu yao. Tuwalinde wanaposoma elimu ya msingi na sekondari, wakishafika vyuo vikuu watakuwa wamepevuka na kuweza kufanya maamuzi ya kujilinda,” alisema.

Akihutubia kwenye mikutano ya hadhara wakati wa ziara yake ya siku nne moani Tabora, Waziri Mkuu aliwaasa vijana wa kiume wasithubutu kuwaoa mabinti wanaosoma, kwani kwa kufanya hivyo, wataishia kufungwa jela miaka 30.

Pia aliwaasa wazazi wanaoamua kuwaoza mabinti zao ili wapate mahari, nao pia wana hatari kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 endapo watabainika kushirikiana na waoaji.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMATATU, AGOSTI 14, 2017.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents