Habari

ACT Wazalendo wapoteza kata 17, Waahidi kufanya makubwa uchaguzi wa Wabunge

Chama cha ACT Wazalendo kimesema kimepokea kwa mikono miwili matokeo ya Uchaguzi mdogo wa Madiwani baada ya kushindwa kwenye kata 17 walizoweka wagombea wao.

Tokeo la picha la ZITTO KABWE
Mhe. Zitto Kabwe

Kupitia taarifa iliyotolewa kwenye Vyombo vya Habari na Kiongozi wa Chama hicho, Mhe. Zitto Kabwe amesema ACT Wazalendo wamepoteza nafasi ya udiwani katika Kata 17 na kukubaliana na matokeo hayo huku akikiri wazi kuwa chama chake kimepokea matokeo hayo kama funzo ili kujiandaa kwenye uchaguzi wa nafasi za Wabunge zilizoachwa wazi.

Ndugu zangu Watanzania Jana tumemaliza Uchaguzi mdogo wa madiwani nchi nzima. Katika kata zote 43 nchini zilizogombewa , sisi ACT Wazalendo tuliweka wagombea kwenye kata 17 tu. Tumepata matokeo ya kata zote na hakuna kata tuliyoshinda. Wapiga kura wameamua na sisi tumekubali. Tunafanya tathmini ya matokeo nchi nzima na tutazungumza na Wananchi. Tunawashukuru sana kwa kura tulizopata. Tutazienzi kwani ndio haki yetu. Tunajiandaa na chaguzi ndogo zinazokuja ikiwemo za Ubunge kwenye majimbo yaliyowazi. Tutatumia mafunzo tuliyoyapata kwenye chaguzi ndogo hizi kujipanga na chaguzi zinazokuja. Kwetu sisi Chama cha Wazalendo, Uchaguzi ulikuwa fursa ya kuzungumza na Wananchi na kufikisha ujumbe wetu kwani kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara kunatunyima fursa hiyo. Hatutachoka kuendelea kusambaza sera zetu kwani tunaamini ni bora zaidi na zinazoweza kuleta unafuu kwa wananchi wetu.

Juzi Kiongozi huyo alipokuwa anafunga kampeni aliwashukuru Watanzania waliojitokeza kwenye Kampeni za ACT Wazalendo na kutaja kiasi cha pesa walichochangiwa na wanachama wao kwa ajili ya Kampeni, ambapo alisema walipata shilingi milioni 15.

“ Kwanza naomba kuchukua nafasi hii kuwashukuru sana wote mliofanikisha kampeni hizi, kwanza wale ambao mlijitolea muda wenu katika mbalimbali nchini kutuombea kura, pili wale mlioitikia wito wetu wa kutuchangia fedha kwaajili ya gharama za Kampeni zetu, tukiwa tumepokea wastani wa shilingi milioni 15 mpaka sasa. Ninawashukuru sana kwa michango ya hali na mali mliyotupatia. Pia nawashukuru wananchi wote waliojitokeza kwenye kampeni zetu. Mmetufariji sana na kututia moyo kuwa inawezekana kabisa kufanya siasa za masuala ya Wananchi na kushindana kwa hoja.

Mwezi mmoja huu wa kampeni, tumepita sehemu mbalimbali za nchi yetu na kuzungumza na Wananchi, kusikiliza matumaini na changamoto zao na kuwaeleza hali ya nchi yetu kisiasa na kiuchumi. Tumeweza kufikisha ujumbe wetu wa kampeni za mwaka huu zilizojikita kwenye masuala ya Haki na Uchumi.

Tumewaeleza namna haki za raia zinavyominywa na namna Uendeshaji mbovu wa uchumi unavyowaweka kwenye dimbwi la umasikini. Tumewaeleza namna uhuru wa mawazo unaminywa, vyama kuzuiwa kufanya mikutano kueneza sera zetu, Bunge kuzuiwa kuonyeshwa moja kwa moja ili Wananchi kufuatilia namna wanavyowakilishwa na magazeti kufungiwa ili kudhibiti uhuru wa Habari.

Tumewaeleza kuhusu vitendo vya kinyama vya kushambulia wawakilishi wa Wananchi kwa lengo la kuua na kufungulia kesi wanasiasa wanaoikosoa Serikali na kutoa mawazo mbadala. Yote haya yanafanywa kwa lengo la mtu mmoja kudhibiti mamlaka ya nchi na kufanya ukiritimba wa Uendeshaji wa nchi yetu jambo ambalo ni hatari kwa Demokrasia yetu.

Tumezungumza na wakulima wa Tumbaku ambao tumbaku yao bado haijanunuliwa tangu msimu uliopita na kuwapa hasara kubwa. Tumewaeleza namna Serikali makini ingefanya kwa kununua Tumbaku yote ya Wananchi na kuitafutia soko. Lakini Serikali ya CCM imewaacha wananchi bila kuwajali.

Tumeongea na Wakulima wa Mbaazi ambao Serikali, kutokana na sera mbovu ya mambo ya nje, imeshindwa kulinda soko lao la nchini India. Tumewaeleza namna Serikali makini ingefanya kwa kununua mbaazi yote kwa bei ya kurejesha gharama za uzalishaji kwa wakulima ili kuwahami wasiingie kwenye dimbwi la umasikini. Serikali ingeweza kuingia makubaliano na Serikali nyengine (G to G) na kuuza mazao haya. Serikali ya CCM ya awamu ya tano haifanyi hivi kwa sababu kwayo Maendeleo ni vitu sio watu. Kwa CCM kiashiria cha Maendeleo ni idadi ya Ndege ambazo Serikali imenunua na sio idadi ya Watu walioondoka kwenye umasikini.

Tumewaeleza Wananchi kote tulipopita namna Serikali inavyotekeleza miradi mikubwa bila kujali maslahi ya nchi yetu. Miaka 110 iliyopita Wajerumani walijenga Reli ya kati kwa kubeba chuma kutoka Ujerumani. Sasa hivi tunajenga Reli hiyo hiyo kwa kubeba chuma kutoka Uturuki. Tanzania ina utajiri wa Madini ya Chuma na makaa ya mawe ya kuzalisha chuma cha pua kule Mchuchuma na Liganga. Serikali ya CCM ya awamu ya tano badala ya kutumia malighafi za ndani kujenga reli, inafanya vile vile walivyofanya wakoloni kana kwamba nchi hii haijasomesha watu wake katika miaka 110 hii tangu mjerumani ajenge reli ya kwanza nchini.

Tumewaeleza Wananchi kuwa Serikali makini ingefanya FUNGAMANISHO kati ya sekta ya ujenzi na sekta ya Viwanda ili kufaidika na uwekezaji mkubwa tunaoufanya na kuzalisha ajira nchini.
Uchumi wetu unasinyaa kwa sababu ya maamuzi mabovu ya uwekezaji mkubwa kwenye Reli na Ndege ambapo kodi inayokusanywa kwa shilingi inapelekwa nje kununua vitu kwa fedha za kigeni.

Mzunguko wa fedha unapungua nchini kwa sababu kutoa fedha nje (outflows) badala ya kushaswishi fedha kutoka nje (inflows) na kuziingiza kwenye Uchumi (injection). Kwa mfano UNCTAD wametoa ripoti yao ya mwaka inayoonyesha kuwa uwekezaji kutoka nje umeshuka kwa 15% tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani. Vile vile uagizaji wa bidhaa za kuzalisha bidhaa nyengine (capital goods) umeshuka na hivyo kuhatarisha uzalishaji nchini.

Mikopo kwa sekta binafsi imeporomoka kabisa na hivyo Viwanda na Biashara za ndani kufunga au kupunguza wafanyakazi. Haya yote ndio yanapelekea Uchumi wetu kutokukua kwa viwango inavyostahili kwa chumi za aina yetu. Hii ndio inapelekea wananchi kuwa na hali mbaya na vyuma kukaza. Vyuma havikazi kwa sababu ya hatua za kupambana na ufisadi, la hasha, ni matokeo ya utekelezaji mbaya wa sera za Uchumi na miradi ya Maendeleo.

Tumewaeleza wananchi namna tunatekeleza kwa vitendo sera zetu maeneo ambayo tumepewa dhamana ya kuongoza. Tumewaeleza kuwa Katika Manispaa ya Kigoma Ujiji Elimu bure ni mpaka kidato cha tano na sita. Na pia tumewaeleza namna tunatekeleza sera ya hifadhi ya jamii ili kuwezesha watu wetu kuwa na bima ya afya, kuweka akiba, kupata mikopo ya gharama nafuu kuendesha Biashara zao na mafao mengine kadha wa kadha.

Tumewaeleza namna tunavyojitahidi kuwa Chama tofauti ambacho kinafanya tofauti kwenye maeneo ambayo tumepewa dhamana ya kuongoza na kuepuka kuwa chama cha kukosoa tu. Tumewaomba Wananchi watupe madiwani ili kuzifanya kata zao kuwa tofauti kwa kutekeleza mipango ya ACT Wazalendo.

Tumewakumbusha Wananchi kuhusu ahadi ya CCM ya shilingi milioni 50 kila kijiji. Tumeitaka Serikali itekeleze ahadi hiyo sasa kwani ikitekelezwa sasa ina faida kubwa kwa wananchi na uchumi wa nchi yetu. Tumewaeleza kuwa ahadi hii ikitekelezwa kwa mfumo wa hifadhi ya jamii watu 36 milioni wataweza kuingia kwenye bima ya afya na watu milioni 6 wataweza kupata mikopo midogo midogo kupitia vikundi vyao vya kuweka na kukopa au vyama vyao vya ushirika.

Ukiacha yote hayo, tumejionea kwa macho yetu namna maji ilivyo kero inayoongoza kote tulipopita kwenye kampeni. Kuanzia Kalemela Urambo, Kijima Misungwi mpaka Lukumbule Tunduru Wananchi wanalia na maji. Kina mama wanatembea zaidi ya saa nzima kutatuta maji. Ukisikia takwimu za Serikali utadhani nchi yetu ni neema tupu katika miaka miwili tangu Serikali ya CCM ya awamu ya tano iingie madarakani kumbe wananchi bado wanakunywa maji pamoja na mifugo sehemu mbalimbali za nchi yetu.

Tumewaeleza Wananchi kuwa sisi ni Chama pekee cha siasa ambacho kiliweka kwenye ilani yake ahadi ya kuanzisha wakala wa Maji Vijijini ili kumaliza kero hii ya maji ya kudumu. Tumewaambia kuwa tumeendelea kusimamia wazo hili Bungeni na limepata uungwaji mkono mkubwa, na tumewaeleza kuwa tumeitaka Serikali iharakishe kuanzishwa kwa wakala huu. Hakuna sababu yeyote inayohalalisha Serikali kushindwa kutoa huduma ya Maji kwa wake.

Masuala yote hayo yanatuonyesha namna ACT Wazalendo inavyojihusisha na mambo ya wananchi, inavyojipa jukumu la kuwa msemaji mkuu wa matatizo yao. Na yanaonyesha namna Serikali ya CCM ilivyofeli kujishughulisha na masuala yao na pia kuendesha vibaya uchumi, jambo linalofanya hali yenu ya maisha iwe mbaya mno.

Huko kote tulikopita tumewaeleza wananchi umuhimu wa kuichagua ACT Wazalendo ili kwanza kutupa ari ya kuwasemea zaidi, kutupa hamasa ya kufanya zaidi siasa za masuala yanayowahusu, na kutoa nafasi kwetu kutekeleza sera na mipango mbadala katika yale maeneo tunayoyaongoza. Tumewaeleza ni muhimu kiasi gani sera na mawazo haya mbadala kuingia kwenye mabaraza yao ya Madiwani”. Mwisho wa kunukuu.

Wananchi wametusikia lakini hawakutuchagua. Tunaamini kuwa ujumbe wetu kwao bado ni muhimu. Tutawasikiliza tuboreshe nini ili ujumbe wetu kwao uendane na matamanio yao. Hatutachoka kuendelea kuwasemea Wananchi masikini wa nchi yetu. Pia tutajitazama na kuboresha utendaji wetu wa kazi. Kura chache tulizopata ni changamoto kwetu kuongeza bidii za kioganaozesheni na mikakati.

Sisi kama Chama cha Wazalendo, tumesikitishwa sana na vitendo vya vurugu na fujo kwenye chaguzi hizi. Vurugu isiwe jambo la kawaida kwenye siasa zetu. Huo sio Utanzania. Tunalaani vikali matumizi ya nguvu za dola kudhibiti vyama vya upinzani. Kukamata Viongozi wetu siku ya Uchaguzi ni ushiriki wa polisi kusaidia Chama tawala. Sio jambo jema. Sio mwelekeo mzuri kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020. Tunasihi Jeshi la Polisi lifanye kazi yake kwa weledi na kubakia kuwa jeshi la wote.”

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents