Habari

ACT Wazalendo watoa tathmini yao ndani ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Magufuli (+Video)

Chama cha ACT Wazalendo leo alhamisi Tarehe 16 Novemba, 2017,  kimetoa tathmini ya miaka miwili ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. John P. Magufuli kwa kuangazia sehemu 9 ambazo serikali imeshindwa kufanikiwa.

Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo,  Yeremia Kulwa Maganja

Akizungungumza na Waandishi wa Habari, Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo,  Yeremia Kulwa Maganja amesema sehemu hizo zimezingatia vigezo vya Haki za Msingi, Usimamizi wa Uchumi na Uendeshaji wa Nchi kwa ujumla.

Soma tathmini hiyo iliyotolewa na ACT Wazalendo kuhusu Uongozi wa Rais Magufuli ndani ya miaka miwili.

[Tathmini ya ACT Wazalendo Juu ya Mambo 9 Yaliyofanywa Vibaya katika Miaka
Miwili ya Serikali ya Awamu ya 5]

Novemba 5, 2017, Serikali ya awamu ya 5 ilitimiza miaka miwili tangu Rais Magufuli alipoapishwa rasmi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika siku husika, Serikali kupitia Msemaji wa Serikali, ilitoa tathmini ya mambo 9 ya mafanikio ambayo yamepatikana ndani ya kipindi hiki cha miaka miwili.

Pamoja na taarifa hiyo rasmi ya Serikali, CCM pamoja na Viongozi mbalimbali wa Serikali kwa siku kadhaa
sasa wamekuwa wakitoa mwendelezo wa mafanikio mbalimbali ya Serikali. Sisi ACT Wazalendo nasi tumefanya utafiti juu ya miaka hii miwili, tukiangazia uchumi, hali ya kisiasa, uimara wa Muungano, ustawi wa utumishi wa watumishi wa umma, hali ya biashara pamoja na kilimo, na masuala yanayohusu haki za wananchi. Lengo likiwa
ni kutoa mtazamo mbadala juu ya hali ya nchi yetu katika miaka hii miwili, kuainisha changamoto (kinyume na mapungufu tu yaliyosemwa), pamoja na kuainisha mbinu pamoja na sera mbadala za utatuzi wa changamoto hizo.
Leo tutatoa tathmini yetu ya miaka miwili ya Utawala huu, tathmini hii ni zao la utafiti husika uliofanyika nchi nzima.

Tathmini yetu itaainisha mambo 10 ambayo tunaamini hayakufanywa vizuri kabisa na Serikali. ACT Wazalendo inao wajibu wa kujihusisha na masuala ya watu, tunatimiza wajibu huo kwa tathmini hii ya kuangazia mambo haya 10
ambayo ni mapungufu ndani ya miaka miwili hii ya utawala huu. Yafuatayo ni mambo 9 ambayo ACT Wazalendo tunaamini Serikali ya awamu ya 5 imeyafanya vibaya zaidi ndani ya miaka hii miwili, kiasi cha kuleta athari kubwa katika hali ya nchi yetu, kisiasa, kiutawala na kiuchumi. Tathmini yetu itayaanisha masuala hayo katika mafungu matatu kama ifuatavyo:

i). Kuminya Uhuru wa Vyama vya Siasa Kufanya Mikutano ya Hadhara, Uhuru wa
Vyombo vya Habari, pamoja na Uhuru wa Kujieleza.

Kwa kutumia amri batili iliyotolewa na Rais na baadaye kukaziwa na Jeshi la Polisi, haki
ya vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya
Siasa ya mwaka 1992, imezuiwa. ACT Wazalendo tulikuwa chama cha mwisho kufanya
Mkutano wa hadhara, viwanja vya Zakhem mbagala Juni, 2016. Tangu hapo haki hiyo
imezuiliwa kinyume na sheria.

Pia, ni katika kipindi hiki cha miaka miwili, ndipo tulipitisha Sheria mbaya ya vyombo vya
habari, Sheria ambayo imeshuhudia kufungiwa kwa Magazeti manne makubwa, ya
Mawio, Mseto, Mwanahalisi, Tanzania Daima, Raia Mwema na Mwananchi kwa vipindi
tofauti tofauti, kwa sababi tu yaliandika habari ambazo hazikupendwa na Serikali.
Miaka miwili hii pia imeshuhudia mamia ya watu wakiwa wameshtakiwa, na wengine
kuhukumiwa vifungo na faini, kwa kutumia sheria mbaya ya mitandao ya kijamii (cyber
crimes act) kwa sababu tu ya kutoa maoni yao ambayo hayapendwi na Serikali.

ii). Kuminywa kwa Haki ya Wazanzibari Kuchagua Viongozi wao.

Ni hali halisi kuwa haki ya Wazanzibari, wananchi wa sehemu moja kati ya pande mbili zinazounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuchagua viongozi wao kwa uhuru na haki iliporwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar wa mwaka 2015, kwa mtu mmoja kujiamulia kinyume na sheria, kufuta matokeo ya uchaguzi wote kwa sababu tu CCM
walielekea kushindwa.

Uchaguzi wa marudio wa Machi 20, 2016 ulikuwa pasi shaka, ni uchaguzi wa ‘kiini macho’. ACT Wazalendo tulisusia uchaguzi huo wa marudio, mpaka sasa msimamo wetu juu ya uchaguzi ule haujabadilika. Kwa miaka hii miwili, Serikali ya awamu ya 5 ya JMT imekwepa kabisa wajibu wake juu ya mustakabali mwema wa Zanzibar. Na kwa kiasi kikubwa imekuwa ndio chanzo cha kuzidisha uhasama na mpasuko utokanao na dhuluma za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na uchaguzi wa marudio wa mwaka 2016. Matamshi ya ubaguzi na vitisho ya Rais Magufuli akiwa kwenye mikutano ya hadhara, Unguja na Pemba ni ushahidi juu ya hili.

Hali hiyo imeigawanya Zanzibar, imeondoa sauti yake imara kwenye Muungano, kiasi kwa mara ya kwanza tangu 1964, Zanzibar ina Mawaziri wachache zaidi kwenye Baraza la Mawaziri la JMT, wawili tu, pamoja na Naibu Waziri mmoja, katika baraza lote lenye mawaziri wapatao 42. Si hilo tu, lakini hali hiyo ya kutoshughulikia mpasuko wa
kisiasa wa Zanzibar imeondoa sauti ya mawazo mbadala ya kisera katika kuendesha uchumi wa wananchi, na hivyo kuchangia hali mbaya ya uchumi kwa wananchi.

(iii). Kupuuzwa kwa Matakwa ya Katiba Mpya.

Serikali ya awamu ya 5 imeweka bayana kuwa Katiba mpya sio kipaumbele chake. Msimamo huu umetolewa na Rais Magufuli pamoja na Waziri Mkuu Majaliwa katika nyakati tofauti, licha ya tafiti zote zilizofanywa kuonesha kuwa Watanzania wengi wanataka kuendelezwa kwa mchakato wa Katiba Mpya.

Sababu dhaifu zinazotolewa na Serikali ni mbili, moja ni kuwa Rais anasema haikuwa ahadi yake ya Uchaguzi (lakini jambo hilo likiwa kwenye ilani ya chama chake cha CCM, sababu ya pili ni ile iliyotolewa na Waziri Mkuu kuwa Serikali haina fedha za gharama za kuendeleza mchakato husika, na kuwa fedha zote inazielekeza kwenye
miradi ya maendeleo. Hoja hii pia ni dhaifu, ni hoja itokanayo na imani ya maendeleo ya vitu ya CCM dhidi ya maendeleo ya watu. Katiba mpya imara inategemea kutoa mamlaka zaidi ya wananchi kushiriki kwenye kufanya maamuzi juu ya mustakabali wao, jambo ambalo ni maendeleo makubwa mno kuliko maendeleo ya vitu wasivyo na
ushiriki wala uamuzi navyo.

iv).Kusinyaa kwa Uchumi wa Nchi, Kudhohofishwa kwa Sekta Binafsi, Mazingira Mabaya ya Biashara Nchini, pamoja Kupaa kwa Deni la Taifa.

Mapungufu makubwa zaidi katika hii miaka miwili ya Serikali ya awamu ya 5 yako katika menejimenti ya uchumi wa Nchi. Ndilo eneo ambalo Serikali imefeli zaidi kuliko maeneo yote. Vipimo vyote vya uchumi vinaonyesha kuwa ndani ya miaka hii miwili uchumi wetu umesinyaa, sekta yetu binafsi imekaribia kuanguka kwa sababu ya mazingira magumu ya kikodi, watu wetu wamepoteza ajira zaidi, serikali imekosa mapato zaidi, nchi yetu ikitajwa kushuka katika nchi zenye mazingira mazuri ya kibiashara, katika wakati ambao biashara zimefungwa zaidi, huku tukishuhudia kupaa zaidi kwa deni la Taifa.

Tathmini yetu itokanayo na Takwimu pamoja na Taarifa rasmi za Serikali yenyewe
imeonyesha yafuatayo:
◊Uzalishaji wa bidhaa za viwandani umeshuka kwa 50%, kutoka dola bilioni 1.5
mpaka dola milioni 700.

◊Mikopo binafsi kutoka benki zetu imeshuka kutoka 25% (2015) hadi 8.9% (2017).

◊ Mikopo ya benki kwenye Kilimo imeshuka kutoka 6% (2015) hadi -9% (2017).

◊ Mikopo ya benki kwa wafanyabiashara imeshuka kutoka 24% (2015) hadi 9%
(2017).

◊Mikopo ya benki kwa sekta ya Viwanda imeshuka kutoka 30% (2015) hadi 3%
(2017).

◊Mikopo ya benki kwa sekta ya Usafirishaji na Mawasiliano imeshuka kutoka 24%
(2015) hadi – 25% (2017).

◊ Mikopo ya benki kwa sekta ya Ujenzi imeshuka kutoka 22% (2015) hadi 16%
(2017).

◊Mauzo ya bidhaa kwenda nje ya nchi (export) kwa ujumla yameshuka kwa
29.8%.

◊ TRA ikidaiwa Marejesho (VAT Returns) ya wastani wa bilioni 800, ambazo bado
hazijalipwa.

◊ Thamani ya sarafu ya Tanzania imeshuka, uwezo wa Tsh. 100 kununua bidhaa
umeshuka hadi Tsh. 92.18.

◊Deni la Taifa likipaa kwa wastani wa Dola milioni 4 kwa mwaka (trilioni 10),
kutoka dola bilioni 18 (2015), mpaka dola bilioni 22 (2016) na kufikia dola bilioni
26 (2017).

◊ Utekelezaji duni wa bajeti ya Taifa kwa mwaka 2016/17 ambapo Serikali ilipanga
kukusanya shilingi trilioni 29.6 lakini ikakusanya trilioni 23.5, kukiwa na nakisi ya
trilioni 6. Huku dalili zikionyesha kuwa utekelezaji wa bajeti ya 2017/18 ya shilingi
trilioni 32 kuwa duni zaidi.

◊ Uwiano wa deni la Taifa na Pato la Taifa (GDP) ukiwa ni takribani 53%.

◊ Mwisho, matarajio ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka yakishushwa toka 7%mpaka
6.6%.

Takwimu hizo zote zinaonyesha kwa dhahiri uchumi wa nchi ulivyosinyaa, sekta binafsi
inavyokufa, mazingira ya biashara yanavyokuwa magumu zaidi pamoja na deni la Taifa
kupaa ndani ya miaka miwili ya Serikali ya awamu ya 5, na kuhalalisha mtazamo wetu
kuwa menejimenti mbaya ya uchumi ndio mapungufu makuu ya utawala huu.

(v). Kilimo Kimetelekezwa.

Sekta ya Kilimo ndio uti wa mgongo wa Taifa, ikiajiri karibu theluthi mbili (65%) ya
Watanzania wote nchini, na kuchangia karibu theluthi moja ya pato la taifa (32%). Kwa
miaka miwili ya utawala wa awamu ya 5, ukuaji wa Kilimo haujavuka zaidi ya 2%, zaidi
ukiwa ni 1.6%, hivyo kushuka kutoka 4% wakati wa awamu ya 4.

Kwa miaka hii miwili ukuaji wa sekta inayoajiri wananchi wengi zaidi ukididimia na kuwazidishia ufukara.
Katika wakati kama huu ambapo Kilimo kinaporomoka, wakulima wa Korosho hawajapewa pembejeo, na hivyo kutishia kushusha uzalishali wa zao linalotuingia mapato ya Kigeni zaidi nchini katika msimu huu wa mavuno. Tumbaku (zao la pili Kwa kuingiza Fedha za kigeni) tayari wakulima wanalia, kukiwa hakuna kabisa soko. Mazao
ya mbaazi, choroko na kunde bei imeshuka kwa zaidi ya 500%, kutoka Tsh 2500 mpaka wastani wa Tsh 200. Huku Pamba uzalishaji ukiwa umeshuka kwa 63% kati ya mwaka 2015 na 2017.

(vi). Utekelezaji wa Miradi Mikubwa bila Kuzingatia Maslahi ya Umma.

Serikali inatekeleza miradi kadhaa mikubwa nchini, hili ni jambo zuri. Lakini mtindo wa
utekelezaji wa miradi hiyo hauzingatii maslahi ya umma, hili ni jambo baya. ACT
Wazalendo tuna mifano miwili kwenye hili, ununuzi wa ndege kwa kutumia fedha za
ndani, na ujenzi wa reli ya SGR bila kuzingatia ufungamanishaji wake na sekta 5 nyengine za uzalishaji kiasi fedha zote zinatoka kwenda nje ya nchi badala ya kubaki ndani. Ununuzi wa ndege za Bombadier na Boeing kwa fedha zetu za ndani umesaidia kukuza na kuzalisha ajira Canada na Marekani zinakozalishwa ndege hizo.

Fedha za wakulima, wafanyakazi na wafanyabiashara wa nchi hii zinatolewa ndani na kulipwa taslimu kwaajili ya ndege nje ya nchi, jambo hilo limesababisha ujazo wa fedha upungue ndani ya nchi yetu (upungufu wote ukiwa ni 51% ndani ya miaka hii miwili) na kusababisha mzunguko wa fedha kuwa mdogo na hivyo kupunguza uwezo wa kununua bidhaa (purchasing power) wa watu wetu, ikiwa ni kipimo Cha kusinyaa kwa uchumi wetu.

Ujenzi wa reli ya SGR ni jambo zuri, lakini kutokuzingatiwa ufungamanishaji wa ujenzi huo na sekta nyengine za uzalishaji kunafanya ujenzi huo uzalishe ajira Uturuki na China badala ya Tanzania. 50% ya gharama za ujenzi wa reli ni ununuzi wa chuma na chuma cha pua kwaajili ya mataruma, tungeweza kuutumia mradi huu kujenga kiwanda
cha chuma cha Liganga na Mchuchuma na hivyo kubakisha nusu ya hizo trilioni 17 za mradi huo hapa nchini. Hali ni tofauti, maana mataruma yatanunuliwa nje ya nchi, na hivyo sehemu kubwa ya fedha za mradi huu kutokubaki nchini.

(vii). Uvunjaji wa misingi ya Sera ya Mambo ya Nje.

Msingi Mkuu wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania ni kusimama na wanaoonewa kokote kule duniani. Pamoja na kufuata “Diplomasia ya Uchumi” bado msingi huo wa Sera ya Mambo ya Nje ya nchi yetu haujabadilika. Lakini hivi sasa, hatua kwa hatua, Tanzania inaanza kuuweka kando msingi huu muhimu wa kusimama na wanyonge. Jambo hili limejidhihirisha katika suala la nchi ya Sahara Magharibi inayokaliwa kimabavu na Moroko pamoja na nchi ya Israel inayofanya mauaji ya mamia ya Wapalestina.

Tangu Mfalme wa Moroko atembelee nchini na kutoa ahadi kemkem za misaada kwa Tanzania, nchi yetu imekuwa haina tena ubavu wa kuikabili Moroko na kuvikemea vitendo vyake vya kimabavu vya kuikalia Sahara Magharibi. Lakini pia ni ndani ya miaka miwili ya awamu ya 5, kwa mara ya kwanza tangu kuundwa kwa Tanzania, Oktoba 26,
2017, nchi yetu ilipiga kura kupinga hatua kali za vikwazo vya shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO, vikwazo ambavyo vililenga kuibana Israel ipunguze mashambulizi dhidi ya Palestina.

Mifano miwili hiyo inaonyesha namna tulivyoacha kabisa msingi wa Diplomasia yetu, ya kusimama na wanyonge, na sasa ndio tumekuwa vinara, watetezi, wasemaji na marafiki wa nchi zinazoonea wanyonge, kama Moroko na Israel.
Si hivyo tu, matukio kama ya kukataliwa kwa mbaazi za Tanzania nchini India, ni kielelezo kingine cha kuanguka kwa Diplomasia yetu ya uchumi.

(viii). Unyanyasaji wa Watumishi wa Umma.

Miaka miwili ya Rais Magufuli imekuwa miaka miwili ya kuyumbishwa na kupuuzwa kwa watumishi wa umma. Uhakiki usiokwisha wa wafanyakazi umetumika Kama kisingizio cha kuwanyima wafanyakazi haki yao ya kuongezwa mishahara, kupandishwa madaraja na kupata marupurupu yao kwa wakati. Kilio cha wafanyakazi kudai haki hizi
kimepokelewa na vitisho na kebehi kutoka serikalini.

(ix). Utawala unaovunja Taasisi za kikatiba na kisheria.

Utawala wa Rais Magufuli ni wa mtu mmoja. Yeye ndiye Amiri Jeshi Mkuu, Yeye ndiye Mkuu wa Nchi, Yeye ndiye Mkuu wa serikali, yeye ndiye Mlipaji Mkuu, Yeye Ndiye Waziri wa Wizara zote! Badala ya kuimarisha taasisi za umma, utawala wa Magufuli umekuwa wa kumuimarisha yeye na chama chake.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents