Habari

ACT yamjibu Ole Sendeka, yasema mali, maisha ya Zitto yako wazi

Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kimeshtushwa na tuhuma dhidi ya kiongozi wake wa chama, Zitto Kabwe kwamba ana miliki mali za kifisadi pamoja na kuhusishwa na ununuzi wa ardhi maeneo ya Kigamboni uliofanywa na NSSF kwa bei ya shilingi milioni 800 kwa ekari moja, wakati bei halisi ni milioni 25 na kwamba kitendo hicho kimeitia hasara serikali .

zitto-kabwe-act-leader3

Tuhuma hizo zilitolewa Ijumaa hii na Msemaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Christopher Ole Sendeka, ambapo alivitaka vyombo kufanya uchunguzi katika shirika hilo ili kubaini waliohusika kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria, huku akimhusisha Zitto katika uchunguzi huo.

Tuhuma hizo zimekiibua chama cha ACT, ambapo Jumamosi hii Katibu wa Bunge na serikali za mitaa ACT, Habibu Mchange, amevitaka vyombo vya uchunguzi haraka iwezekanavyo kuchunguza mali, madeni, akaunti zote za benki pamoja na mfumo wa maisha ya Zitto.

“ACT imeshtushwa na tuhuma, kashfa, porojo na matusi mbalimbali yaliyotolewa jana na Ole Sendeka dhidi ya kiongozi wa chama chetu,” alisema Mchange.

“Tunaamini kama kuna kiongozi ambaye mali, madeni, maslahi, na akaunti zake viko wazi basi ni ndugu Zitto,” aliongeza.

Aidha, Mchange alidai kuwa, kilichomsukuma Sendeka kutoa tuhuma hizo kwa Zitto ni harakati zake za kuupinga muswada mpya wa habari. “Tuhuma za Ole Sendeka kuna kitu nyuma yake, jitihada za zito za kupambana na muswada wa habari ndizo zilizomuibua, sababu wanataka upitishwe ili kuviua vyombo vya habari,” amesema.

Alisema ACT itaendelea kuisimamia serikali katika mambo ya bungeni kama anavyofanya mbunge na kiongozi wao wa chama. Pia alisema katiba ya chama hicho huwataka viongozi wote kuweka hadharani matamko ya mali zao na madeni na kwamba Zitto alitekeleza matakwa hayo ya kisheria hivyo mali na madeni yake yako hadharani na mtandaoni.

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents