HabariUncategorized

Afrika iandae rasilimali watu kusimamia sekta ya madini – Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Mataifa ya Afrika yanatakiwa yaandae maarifa, vitendea kazi na rasilimali watu watakaoweza kusimamia na kuendeleza ipasavyo sekta ya madini na kuleta tija kwa Taifa husika na wananchi kwa ujumla.

Amesema taarifa za kijiolojia zinaonesha kuwa Afrika ni Bara lenye utajiri mkubwa wa rasilimali madini huku sehemu kubwa ya madini hayo yakiwa bado hayajaanza au yako kwenye hatua mbalimbali za uendelezaji.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Septemba 14, 2017) alipofungua mkutano wa 37 wa Baraza la Uongozi wa Kituo cha Madini na Jiosayansi cha Afrika (AMGC) uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kituo hicho mkoani Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amesema rasilimali za madini ilizopo Barani Afrika inaweza kuwa ni chanzo kikubwa cha kusukuma maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika nchi nyingi iwapo itasimamiwa vizuri.

Ametolea mfano Tanzania ambayo licha ya kuwa na utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu, almasi, chuma, madini ya vito kama tanzanite lakini mchango wa sekta ya madini ni asilimia 4.8 ya pato ghafi la Taifa.

“Changamoto kuu kwa sasa ni kwa jinsi gani tunaweza kuwa na sekta ya madini inayotoa mchango stahiki katika nchi husika pamoja na kusimamia sekta hii kwa kuwafanya wananchi wetu hususan katika maeneo yenye rasilimali wakanufaika na kuona fahari badala ya kuacha mashimo, umasikini na mateso kwa wananchi.”

Amesema lengo la kuanzishwa kwa kituo hicho ambacho leo kimetimiza miaka 40 ni kuhakikisha sekta ya madini inawajibika kuleta maendeleo ya kijamii na uchumi pia ikijali masuala ya mazingira, hivyo ni vema kikatumika kama ilivyokusudiwa.

Waziri Mkuu amesema kituo hicho kikitumika vema kwa mujibu wa kusudia la uanzishwaji wake kinaweza kuleta tija kubwa kwenye sekta ya uchumbaji wa madini, uongezaji wa thamani na usimamizi wa sekta.

Amesema kituo hicho ni moja kati ya taasisi chache duniani yenye teknolojia za kisasa ambazo zinaweza kusaidia kufanya uchambuzi wa miamba na madini yaliyimo. “Pia ni sehemu ambayo unaweza kupata huduma za ushauri na kusaidia teknolojia utakayoweza kutumia ili kufanya uzalishaji wa madini mbalimbali.”

Hivyo amewakumbusha wajumbe na wanachama wa AMGC kuwa kituo hicho hawajakitumia ipasavyo ni vema kikatumika ili kupata tija kwenye uendelezaji na usimamizi wa madini, ambapo ameiagiza Bodi iandae mpango utakaoziwezesha nchi wasnachama kukitumia.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani amesema kwa sasa kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali ya kwanza ni kwa wanachama kutolipa ada kwa wakati.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

ALHAMISI, SEPTEMBA 14, 2017.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents