Habari

Afya ya Kimesera yaimarika

HALI ya mgombea ubunge wa Kiteto kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Victor Kimesera, inaendelea vizuri na wakati wowote anaweza kutoka hospitalini.

na Irene Mark

 

HALI ya mgombea ubunge wa Kiteto kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Victor Kimesera, inaendelea vizuri na wakati wowote anaweza kutoka hospitalini.

 

Kimesera anayedhaniwa kula chakula chenye sumu, amelazwa chumba namba 26, ghorofa ya pili, katika Hospitali ya Aga Khan Dar es Salaam, kwa matibabu zaidi, baada ya kuletwa kwa ndege ya kukodi kutoka mji wa Kibaya, Kiteto, baada ya afya yake kuzorota kutokana na maumivu ya tumbo.

 

Akizungumza na Tanzania Daima, Mkurugenzi wa Vijana wa Chadema, John Mnyika, alisema afya ya mgombea huyo inaendelea vizuri baada ya taarifa ya madaktari kuonyesha kuwa hakuna madhara makubwa yaliyosababishwa na chakula hicho.

 

“Madaktari wamesema Kimesera anaendelea vizuri na kwamba muda wowote kati ya kesho (leo) au kesho kutwa (kesho) anaweza kuruhusiwa…pia wamemtaka kupumzika kwa siku kadhaa.

 

Sisi kama chama tumepokea taarifa hiyo kwa faraja. Tunajipanga kumrejesha mpambanaji wetu kwenye uwanja wa mapambano pindi atakapopona kabisa…ushindi ni wetu, kwanza wananchi wa Kiteto wamemwandalia mapokezi makubwa mgombea huyo,” alisema Mnyika.

 

Alisema, baada ya madaktari kuwahakikishia kuwa afya ya mgombea huyo inaendelea vema, uongozi wa chama hicho umejizatiti kuendeleza kampeni huku ukitumaini kupata ushindi.

 

Katika uchaguzi huo, Kimesera anayeungwa mkono na vyama vitano vya upinzani, alidhaniwa kula sumu kwenye chakula katika hoteli ndogo mjini Kibaya, Jumapili iliyopita, baada ya kuhitimisha kampeni za siku ya nne.

 

Mgombea huyo aliletwa Dar es Salaam kwa ndege ya kukodi yenye namba za usajili N30MS, ambayo ni maalumu kwa kubeba wagonjwa, kabla ya kuchukuliwa kwa gari la wagonjwa la Kampuni ya Knight Support lenye namba T 360 AAU, kisha kukimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa matibabu zaidi.

 

Alipowasili kwenye uwanja mdogo wa ndege juzi, alionekana kuwa na maumivu makali yaliyomfanya apige kelele.

 

Kufanyika kwa uchaguzi huo mdogo kunatokana na kifo cha aliyekuwa mbunge wa Kiteto kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Benedict Losurutia, aliyefariki dunia mwishoni mwa mwaka jana baada ya kusumbuliwa na maradhi ya tumbo.

 

Uchaguzi huo unafanyika Februari 24, mwaka huu, hivi sasa kampeni za kambi ya chama tawala na ile ya upinzani zimeshika kasi.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents