Afya ya Sajuki yawa mbaya baada ya Bongo Movie kutaka kuharibu tamasha lake la Arusha

Sajuki

Afya ya msanii wa filamu nchini Sadick Juma Kilowoko maarufu kwa jina la Sajuki hivi karibuni ilibadilika ghafla na kuwa mbaya baada ya baadhi waigizaji wa Bongo Movie kumtaka aahirishe tamasha lake la kuchangisha fedha za matibabu yake nchini India alilolikuwa amepanga kulifanya December 16.

Akiongoa na kipindi cha Tagz Weekly cha DTV, rafiki yake wa karibu na Sajuki ambaye pia ni muigizaji, Dinno anasema wiki iliyopita alikuwa safarini kuelekea Arusha akiwa na Sajuki na Wastara ndipo alipopigiwa simu na msanii wa Bongo Movie ambaye hakumtaja jina, aliyempa taarifa kuwa wao pia walikuwa na tamasha lao jingine siku ya Jumamosi na hivyo kumtaka Sajuki aahirishe la kwake.

“Baada ya muda walimpigia Sajuki,” alisema Dinno. “Sajuki kwakweli tulikuwa naye kwenye safari wao hawakujua kuwa niko na Sajuki. Ile taarifa Sajuki kidogo aliipokea tofauti akawaambia basi niacheni tutazungumza baadaye.”

Aliendelea, “nikawa nimepokea simu ya muigizaji mwingine nguli tu kama mimi akawa ananiambia, ‘Dinno mi nashangaa mnang’ang’ania Arusha wakati sisi tumewaambia mbadilishe tamasha mlipeleke Moshi tuje tuwasupport Moshi sisi tunafanya tarehe 15’ Mi nikamwambia nashangaa wewe kusema hivyo wakati unajua tamasha hili limeandaliwa na mtu mwenyewe hali yake unaielewa sio nzuri. Mtu ametoa fedha zake mfukoni kutaka kutafuta nyingine ya kumjazia aende India kwa matibabu wewe unasema alibadilishe tamasha wakati mwenzako kashatumia pesa, hizo pesa anarudishiwa na nani?”

Dinno alisema alishangazwa na kauli hiyo kutoka kwa msanii mwenzie ambaye hakuonesha huruma kwa Sajuki ambaye ameingia gharama ya matangazo ya tamasha lake pamoja na mafuta zaidi ya laki tano kwa safari yao ya Arusha.

“Kwakweli kitu kama hicho kilituumiza sana, kilimuumiza sana Sajuki. Kiukweli baada ya hapo hali ya Sajuki ikabadilika. Siku ya kwanza tulilala vizuri. Siku ya pili tu ndio likaanza balaa. Kiukweli mimi nilikuwa nimelala kama saa kumi usiku ama saa tisa Wastara namkuta mlangoni analia ananiambia Sajuki kazidiwa sana. Kwenda kweli namkuta Sajuki yupo kwenye hali nyingine tofauti, anahemea juu, mapigo ya moyo ya juu, anapiga kelele. Sijawahi kumuona Sajuki akilia. Sajuki alikuwa analia ananiambia, ‘Dinno naumia sana, mimi nahisi nakufa sasa hivi’. Akaomba simu aongee na mama yake. Kwakweli maneno aliyokuwa akisema Sajuki ni maneno ambayo yaani mtu yeyote aliyekuwa anasikia angesema kweli yupo kwenye hali tofauti. Kweli Sajuki aliumwa siku hiyo, sikulala akawa ananiambia ‘mgongo unauma Dinno ni kama unawaka moto yaani kifua kinauma, sielewe ni nini.”

Dinno alisema bahati nzuri asubuhi ilipofika walimpeleka hospitali ambako alichomwa sindano na hali yake kurejea kawaida kiasi.

Hata hivyo aliongeza kuwa katika siku tatu zote walizokuwa Arusha, Sajuki hakuweza kulala na muda mwingi alikuwa akilia na kusikitika na wakataka kuahirisha tamasha hilo japo mioyo yao ilikuwa migumu.

Alisema aliamua kulibadilisha tamasha hilo kutoka kwenye kucheza mpira na kuwa tamasha la muziki ambapo wasanii wa Arusha walijitolea kutumbuiza bure na tamasha hilo kufana.

Kabla ya Arusha, Sajuki alikuwa na show nyingine mkoani Iringa ambayo ilifanikiwa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents