Promotion

Airtel na One8 kusaidia shule 50

Airtel na One8 kusaidia shule 50

Shule 50 za msingi hapa nchini zinatarajiwa kunufaika kutokana na mafanikio ya kundi la kwanza la muziki kutoka Afrika, ‘Airtel ONE8’, kwa kupata asilimia ya mapato kutoka wimbo wa kundi hilo unaokwenda kwa jina la Hands across the world.

 

Akizungumza katika hafla ya kutambulisha kazi hiyo iliyofanywa na Ali Kiba na wenzake, Mkurugenzi wa Masoko na Bidhaa wa Airtel, Kelvin Twissa alisema Airtel ilidhamini mradi huo wa One8 kwa lengo la kusaidia masikini duniani kote na hasa Afrika ambako fedha zitakazopatikana kwenye mradi huo zitakwenda kusaidia jamii hiyo na kuendeleza.

“Tumedhamini mradi huu wa One8 pamoja na wimbo wa Hands Across the World ambao sasa utapatikana kwenye simu kama ‘mlio maalum’ pamoja na picha za wasanii hao wakirekodi studio kwa watumiaji wa mtandao wetu Afrika nzima na fedha zitakazokusanywa zitakwenda kusaidia ujenzi ama ukarabati mkubwa wa shule mbalimbali za msingi hapa nchini,” alisema Twissa.

Airtel na One8 kusaidia shule 50

Wanawamuziki ambao waliimba na R Kelly wimbo wa ‘Hands across the world’ mbali na Ali Kiba ni 2Face (Nigeria), Fally Pupa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Amani (Kenya), 4×4 (Ghana), Navio (Uganda), JK (Zambia) na Movaizhalene (Gabon).

Kwa mujibu wa Twissa, Airtel itatumia mradi huo wa One8 kusaidia shule za Afrika nzima kupitia asilimia za mauzo yatakayotokana na rekodi za kundi la One8 na maonesho yake pamoja na kusaidia kuendeleza elimu kwa masikini sehemu za vijijini kwa kujenga, kuweka vifaa na kuajiri watu katika shule hizo na kuwapa watoto waliosahaulika nafasi nzuri ya kufikia malengo yao.

Kwa kuanzia, Twissa alisema mradi huo umeanza kufanya kazi katika shule ya msingi Kiromo iliyopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani ambapo madarasa ya shule hiyo yatajengwa upya, pamoja na kujengwa maktaba, na shule itapewa madawati, pamoja na wanafunzi kupewa sare za shule, viatu pamoja na chakula cha mchana kwa muda wote.

Kwa mujibu wa Airtel ujenzi huo wa shule hiyo ambao umekwishaanza hivi sasa unatarajiwa kukamilika Machi mwakani ambapo mradi huo ambao ni endelevu utahamia katika shule nyingine.

Kundi la One8 lipo chini ya kampuni ya Rockstar 4000 huko mwanadada Christine ‘Seven’ Mosha akiwa mratibu wake kwa nchi za Afrika Mashariki. Wasanii wengine wa Tanzania ambao wapo chini ya Rockstar 4000 ni Ambwene Yesaya ‘AY’, Hamisi Mwinyijuma ‘Mwana FA’ na Marlaw.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents