Habari

Ajali ya basi yaua 15

Pichani ni Gari dogo la abiria maarufu kama kipanya ambalo limepata ajali na kuuwa watu 15 mjini Mbeya baada ya kugongwa na lori la mizigo aina ya Scania 113 kwa nyuma.WATU 15 wamekufa na wengine zaidi ya wanane kujeruhiwa baada ya gari aina ya Toyota Hiace (kipanya), waliyokuwa wanasafiria kutoka Tunduma wilayani Mbozi kwenda Mbeya mjini kugongwa kwa nyuma na lori lililokuwa limekatika breki.

Pichani ni Gari dogo la abiria maarufu kama kipanya ambalo limepata ajali na kuuwa watu 15 mjini Mbeya baada ya kugongwa na lori la mizigo aina ya Scania 113 kwa nyuma.


Merali Chawe, Mbeya


WATU 15 wamekufa na wengine zaidi ya wanane kujeruhiwa baada ya gari aina ya Toyota Hiace (kipanya), waliyokuwa wanasafiria kutoka Tunduma wilayani Mbozi kwenda Mbeya mjini kugongwa kwa nyuma na lori lililokuwa limekatika breki.


Ajali hiyo ilitokea saa 12 jioni juzi katika eneo la Nanyala wilayani Mbozi baada ya lori namba T 947 AGT na tela lake namba T 900 AFZ ambalo lilikuwa kwenye mwendo wa kasi, kuligonga gari dogo aina ya Toyota Hiace namba T 283 AFJ.


Waliokufa katika ajali hiyo ni Atupakisye Sege, Friday Siwakwe, Salum Ramadhani, Frank Mwaigisy, Hussein Aman, Elizabeth Mwakalukwa, Andrew Mwalukama, John Poles na Askofu wa Kanisa la Sabato Nyanda za Juu Kusini, William Mtani na Katibu wake, Mchungaji Godlen Mwangilima.


Maiti za watu wengine wanne hazijatambulika wakiwamo wanawake wawili na wanaume wawili katika ajali hiyo ambayo watu saba walikufa papo hapo. Wanne walifariki dunia wakati wakikimbizwa hospitali na wengine watatu walikufa wakati wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.


Waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni dereva wa lori Elipamphrey Samky aliyelazwa Hospitali ya Rufaa, dereva wa Hiace Remijo John ambaye amelazwa katika Hospitali ya Ifisi Mbalizi, Aman Mwasanga, Hezron Mapunda na Amani Salehe.


Hata hivyo, wakati leseni ya biashara ya gari hilo aina ya Toyota Hiace mali ya Godfrey Mwacha ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam, inaonyesha gari hilo lina uwezo wa kubeba abiria 15, gari hilo wakati linapata ajali lilikuwa na zaidi ya abiria 22.


Majeruhi wengine ni Veronica George, Lucy Ndenga na Upendo Isaya. Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, aliyefahamika kwa jina moja la Zambi alisema kuwa hali za majeruhi hao zinaendelea vizuri ingawa hawawezi kuruhusiwa kutoka leo au kesho.


Mmoja wa watu walioshuhudia ajali hiyo, Julius Namwema (38) mkazi wa Nanyala wilayani Mbozi, alisema kuwa lori lililosababisha ajali na Hiace yalikuwa yakitokea wilayani Mbozi kwenda Mbeya, huku upande wa kulia wa barabara lilikuwapo gari kubwa jingine likitokea Mbeya kwenda wilayani Mbozi.


Alisema lori hilo lilikuwa katika mwendo wa kasi na dereva alishindwa kuipita Hiace hiyo na kuigonga kwa nyuma, kuiburuza umbali wa mita 50 kabla ya kuirusha nje ya barabara umbali wa mita 20. Alisema lori hilo lililokuwa limebeba matofali, nalo lilitoka nje ya barabara na kugonga nguzo ya umeme na kusababisha mlipuko mkubwa wa moto.


Dereva wa lori hilo, Samky alisema mipira ya upepo katika gari yake ilikuwa na hitilafu na kusababisha breki zisifanye kazi na hivyo gari kwenda kwa mwendo wa kasi.


Alisema alipofika katika eneo la Nanyala, aliiona Hiace ikiingia barabarani na alipiga honi za tahadhari, lakini dereva wa Hiace hakupisha njia na ndipo alipomgonga kwa nyuma na kuiburuza na lori lake pia likaanguka.


Dereva wa Hiace, Remijo John alisema alisikia kishindo ghafla na gari yake ikanasa mbele ya lori hilo na kuburuzwa umbali mrefu na kusababisha vifo vya watu kadhaa katika gari hilo.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Suleiman Kova alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa lori hilo lililokuwa limebeba matofali, baada ya kuigonga Hiace hiyo lilikwenda umbali wa mita 350 na kuanguka.


Alisema Polisi inaendelea na uchunguzi kuhusiana na ajali hiyo na dereva atakayebainika kuwa alisababisha ajali hiyo kwa uzembe atachukuliwa hatua za kisheria.


Kutokea kwa ajali hiyo kumefanya watu 17 kufa, baada ya ajali iliyotokea mwishoni mwa mwezi uliopita katika eneo la Nzovwe jijini, ambako lori liligonga maduka ya biashara na kusababisha vifo vya watu watatu akiwamo dereva.


Baadhi ya wakazi wa jijini hapa wamesema kuwa kukosekana kwa umakini wa madereva na magari kubeba abiria wengi kupita kiasi imekuwa ni moja ya sababu zinazochangia vifo vya watu wengi.


Pia waliwalaumu askari wa usalama barabarani kwa kutokuwachukulia hatua madereva na abiria wanaozidi katika magari.


Wakitoa mfano, walisema gari hilo aina ya Toyota Hiace lina uwezo wa kubeba abiria 15 lakini lilikuwa limebeba abiria zaidi ya 22, hali ambayo ni hatari kwa maisha ya abiria hao.


Katika tukio jingine lori lenye namba T 188 AFH, mali ya Kampuni ya Kanji Lalji, limeharibika sehemu ya mbele baada ya kugonga treni katika eneo la Iyunga jijini hapa saa saba usiku wa kuamkia jana.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents