Ajinyonga kupinga ndoa ya bintiye

MZEE wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Ilboru, wilayani Arumeru, Exaud Solomon (58), amefariki dunia baada ya kujinyonga akipinga binti yake kuolewa na mwanamume ambaye hakumtaka

na Mustafa Leu, Arusha




MZEE wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Ilboru, wilayani Arumeru, Exaud Solomon (58), amefariki dunia baada ya kujinyonga akipinga binti yake kuolewa na mwanamume ambaye hakumtaka.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Matei Basilio, alisema kuwa majirani wa mzee huyo wa kanisa ndio walioukuta mwili wake ukining’inia kwenye mti shambani kwake.

Alisema kuwa mwili huo uligundulika asubuhi ya Mei 3 mwaka huu na taarifa kutolewa polisi na inaaminika kuwa alijinyonga usiku wa kuamkia siku hiyo.

Alisema kuwa licha ya kuwa mzee wa kanisa, marehemu alikuwa pia kiongozi wa kwaya wa kanisa hilo na binti yake, ambaye hakumtaja jina, alikuwa aolewe kesho yake.

Matei alisema marehemu alipopekuliwa mfukoni alikutwa na karatasi iliyokuwa na ujumbe uliosema: ‘Dunia tunapita, nimekuwa nikiishi kwenye mateso makubwa.’ Aidha, ujumbe huo ulibainisha kuwa mateso hayo yalikuwa yamesababishwa na ndugu zake wawili wa kiume ambao aliwataja majina yao.

Kamanda Matei alisema kuwa ndugu hao wamehojiwa polisi kuhusiana na tukio hilo.

Habari kutoka kwa majirani zimeeleza kuwa marehemu alikuwa hataki binti yake huyo kuolewa na kijana ambaye hakumtaka lakini ndugu hao wamekuwa wakishinikiza binti huyo kuolewa na kijana huyo.


 


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents