Habari

Alichokisema Makamu wa Rais baada ya kupokea vifaa vya upasuaji kutoka Ubalozi wa KUWAIT

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema uboreshaji wa huduma katika hospitali zetu za kibingwa kama MOI, zitaipunguzia Serikali mzigo wa kupeleka wagonjwa nje ya nchi na hivyo kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa kupokea vifaa vya Chumba Cha Upasuaji wa Watoto vilivyotolewa na Ubalozi wa Kuwait kwa Taasisi ya Mifupa (MOI) leo Mei 15, 2018.

“Aidha kwa namna ya kipekee nakushukuru Mheshimiwa Balozi wewe binafsi na Serikali ya Kuwait kwa ushirikiano ambao mnaendelea kuipatia Serikali yetu ya awamu ya Tano katika Sekta mbalimbali za maendeleo lakini hasa hasa katika sekta ya afya” alishukuru Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais amesema kuwa Balozi wa Kuwait Mhe. Jasem Al Najem amekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza sekta ya Afya hapa nchini ambapo leo wamesaidia vifaa vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 258 ambavyo vitaiwezesha Taasisi kuimarisha utoaji wa huduma ya upasuaji hasa kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.

Makamu wa Rais amesema msaada huo utaiwezesha Taasisi kuwa na chumba cha upasuaji ambacho kitakuwa maalum kwa watoto tu, hivyo idadi ya wagonjwa watakaopata huduma ya upasuaji itaongezeka kutoka 500-700 kwa mwezi, kufikia zaidi ya wagonjwa 1000 kwa mwezi na watahudumiwa kwa haraka zaidi.

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndugulile amesema Tanzania iatendelea kuimarisha uhusiano na nchi ya Kuwait kwani wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa msaada haswa msaada inayohusu sekta ya afya.

Balozi wa Kuwait hapa nchini Mhe. Jasem Al Najem amesema kuwa Wananchi wa Kuwait wana mapenzi makubwa na Watanzania na kuahidi wataendelea kutoa msaada.

Tazama picha zaidi;

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents