Habari

Alichokizungumza Waziri Kigwangalla kuhusu sekta ya utalii nchini

Tanzania imefanikiwa kuongeza idadi ya watalii kutoka 1,284,279 mwaka 2016 hadi kufikia 1,327,143 mwaka 2017 hali iliyopelekea kuongezeka kwa mapato ya Serikali.

Akizungumza wakati wa Kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mali Asili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala amesema Wizara hiyo itaendelea kuvutia watalii zaidi ili kukuza utalii na kuongeza pato la Taifa.

“Mapato yanayotokana na utalii yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani Bilioni 2.1 mwaka 2016 hadi Dola za Kimarekani Bilioni 2.2 mwaka 2017” Alisisitiza Kigwangala.

Akifafanua Dkt. Kigwangala amesema lengo la Serikali ni kuona mafanikio haya yanazidi kuimarika, hivyo kila mtumishi katika Wizara hiyo lazima atimize wajibu wake ipasavyo.

Aliongeza kuwa ili kufanikisha majukumu ya Wizara hiyo ipasavyo ni muhimu kuwa na bajeti ambayo itawezesha kushughulikia changamoto za migogoro ya mipaka katika maeneo ya hifadhi, kufanya mapitio ya Sera, Sheria na Kanuni mbalimbali, upungufu wa watumishi, uhaba wa vitendea kazi, kutoa elimu ya maadili na kusimamia watumishi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Meja Jenerali Gaudensi Milanzi amesema kuwa Wizara hiyo itazingatia ushauri unaotolewa na watumishi wake ili kuongeza tija katika kutatua changamoto zinazojitokeza.

“Wizara itaendelea kupambana dhidi ya ujangili, biashara haramu ya nyara na magogo na kuwachukulia hatua kali watumishi wote watakaogundulika kukiuka maadili ya utumishi wa umma kwa kushiriki katika vitendo hivyo, “ Alisisitiza Meja Jenerali Milanzi.

Wizara kwa mwaka wa fedha 2017/2018 iliendelea na utaratibu wa kuendeleza watumishi katika mafunzo ya aina mbalimbali kama ifuatavyo:Jumla ya watumishi wanne (4) wanahudhuria mafunzo ya muda mrefu nje na ndani. Aidha, mtumishi mmoja(1) yupo nje ya nchi.

Watumishi wengine kumi na moja (11) walihudhuria mafunzo ya muda mfupi. Mafunzo haya yalihusu watumishi wa kada mbalimbali.

Jumla ya watumishi saba (7) wamehudhuria mafunzo ya ujasiliamali unaohusiana na maandalizi ya kustaafu. Aidha, Wizara bado inaendelea na utaratibu wa kuwaandaa watumishi wote wanaokaribia kustaafu kuhakikisha wanapata mafunzo hayo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents