Aliyemtoa Arsene Wenger nchini Japan na kumpa mkataba wa kuinoa Arsenal afariki dunia
Aliyekuwa mwenyekiti wa klabu ya Arsenal kwazaidi ya miaka 30, Peter Hill-Wood amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 82.
Hill-Wood aliingia kwenye bodi ya Arsenal mwaka 1962 na kupata nafasi ya mwenyekiti mwaka 1982 nafasi aliyoitumikia mpaka 2013 na kuachana nayo kufuatia kuanza kusumbuliwa ugonjwa wa shinikizo la moyo.
Maamuzi yake ya kwanza baada ya kupata nafasi ya mwenyekiti alimuajiri Arsene Wenger kuwa meneja wa timu hiyo mwaka 1996 akimchukua kutoka Japan, chaguo ambalo lilipingwa na watu wengi kwa wakati huo kabla ya Mfaransa huyo kuwaonyesha uwezo wake na kupata mafanikio makubwa.
Wakitoa taarifa ya kifo chake klabu hiyo imesema ‘’ Kwa majonzi makubwa wanatoa taarifa ya kifo cha aliyekuwa mwenyekiti wa timu hii Peter Hill-Wood,’’ imesema Arsenal.
Taarifa hiyo imeendelea ‘’Tukiwa tunasherehekea miaka 100 ya mafanikio msimu huu, familia ya Hill-Wood inapenda kuelezea tulipotoka, umoja na mabadiliko ya sasa kwenye soka la Uingereza,’’
Mbali ya kumleta George Graham kama kocha ndani ya Arsenal lakini pia Hill-Wood aliiongoza klabu hiyo kwa mafanikio makubwa ambapo wakati wake aliweza kutwaa makombe mawili ya ligi, FA Cup, League Cup na European Cup lakini pia mabadiliko ya kuachana na matumizi ya uwanja wa Highbury hadi kuamia Emirates mwaka 2006.
Wenger aliiyongoza Arsenal kuchukua mataji matatu ya Premier League, manne FA na huku ukiwemo msimu wake wa mafanikio mwaka 2003/04 ambapo aliweza kumaliza ligi hiyo bila kufungwa.