Habari

Aliyeua watu 17 apandishwa kizimbani

Mtu mmoja amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara, kwa makosa ya mauaji ya watu 17, wote wa familia moja, wakazi wa eneo la Mugaranjabo wilayani humo, kwa kuwakata mapanga wakati wakiwa nyumbani kwao.

Tukio la mauaji ya watu hao 17, na wote wakiwa ni wanafamilia moja lilitokea mwaka 2010. Aliyefikishwa katika mahakama hiyo mbele ya hakimu Richard Maganga, ametambuliwa kwa majina ya Sura Bukaba Sura maarufu kwa majina ya Phinias Yona au Epoda (35), mkazi wa wilayani Butiama mkoani Mara.

Akisomewa mashitaka yake ya mauaji ya watu 17 hao, Mwendesha Mashitaka wa Polisi Jonas Kaijage, aliiambia mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa huyo akiwa na wenzake wapatao 15, ambao wote wakazi wa wilayani humo, walitenda makosa hayo Februari 16 mwaka 2010 majira ya usiku katika eneo la Mugaranjabo, nje kidogo ya mji wa Musoma.

Kaijage alisema mtuhumiwa huyo, alitenda kosa hilo akiwa na wenzake hao, ambao tayari walishakamatwa na kufikishwa mahakamani, ambapo kati yao wanane walikwishafariki dunia wakiwa mahabusu. Inadaiwa watu hao walimuua Kawawa Kinguye na wenzake wapatao 16, ambao wote ni wa familia moja kwa kuwakata mapanga wakati wakiwa nyumbani kwao.

Alifafanua kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Julai 18 mwaka huu, kwa kesi nyingine ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika eneo la Rwamulimi mjini Musoma.

Alisema katika tukio hilo la unyang’anyi wa kutumia silaha, mtuhumiwa huyo alivamia nyumbani kwa mwananchi mmoja na kuvunja nyumba kwa kutumia nondo na kufanikiwa kuiba Sh 500,000 taslimu. Alisema kuwa polisi walifanikiwa kumkamata na kumtambua kuwa alishiriki katika tukio la mauaji ya watu hao 17 lililotokea mwaka 2010.

Mtuhumiwa huyo baada ya kusomewa mashitaka yake, hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria kusilikiza kesi za mauaji. Hakimu Karimu Moshi aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 7 mwaka huu, itakapotajwa tena mahakamani hapo na kuunganishwa na washitakiwa wengine waliosalia.

Source: Habari Leo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents