Habari

Amina aliza maelfu Dar

Mama Mzazi wa Amina Chifupa, Judy Mbanga akilia wakati akiwasili kutoka hospitali ya Lugalo kuuchukua mwili wa marehemu janaMSIBA wa Amina Chifupa Mpakanjia aliyefariki dunia juzi, umewaliza viongozi wakiwamo wabunge na maelfu ya watu waliohudhuria kuuaga mwili wake nyumbani kwao Mikocheni, Dar es Salaam.

Mama Mzazi wa Amina Chifupa, Judy Mbanga akilia wakati akiwasili kutoka hospitali ya Lugalo kuuchukua mwili wa marehemu jana


Waandishi Wa Habari Leo


MSIBA wa Amina Chifupa Mpakanjia aliyefariki dunia juzi, umewaliza viongozi wakiwamo wabunge na maelfu ya watu waliohudhuria kuuaga mwili wake nyumbani kwao Mikocheni, Dar es Salaam.


Katika msiba huo, gazeti hili lilimshuhudia Waziri Mkuu Mstaafu, Rashidi Kawawa akishindwa kuvumilia na kububujikwa machozi aliposhuhudia jeneza lililobeba mwili wa Amina likiwasili nyumbani kwa Mzee Hamisi Chifupa saa 7.47 jana mchana.


Simanzi kubwa ilizidi nyumbani hapo baada ya wabunge 30 wakiongozwa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta walipowasili, kwani karibu wote walikuwa wakilia hivyo kuibua huzuni, simanzi isiyo kifani kutoka kwa wafiwa, jamaa na marafiki waliokuwapo.


Kati ya wabunge hao waliowasili hapo saa 10.34 jioni, Sitta na Mbunge wa Mbinga Magharibi, John Komba walibubujikwa na machozi walipokuwa wakiwapa pole mumewe Amina, Mohammed Mpakanjia na baba mzazi, Luteni mstaafu Hamisi Chifupa.


“Amina vijana wanakutegemea, jamani tulikuwa hatuamini kama kweli umekufa, hivi ni kweli Amina,” ni baadhi ya maneno yaliyosikika kutoka kwa Mbunge Janeth Masaburi baada ya kuwasili nyumbani hapo.


Naye Mbunge Komba alipokuwa akipita kumpa pole na kumkumbatia Mpakanjia, alianza kulia hali ambayo ilimfanya Mpakanjia naye alie na kuongeza simanzi zaidi eneo hilo.


Wabunge wengine ambao waliangua kilio kwa uchungu baada ya kuwasili nyumbani kwa baba mzazi wa marehemu ni Anne Kilango Malecela, wabunge wa Viti Maalumu Chadema, Halima Mdee na Grace Kihwelu.


Wengine ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mwantumu Mahiza, Naibu Waziri wa Miundombinu, Dk. Maua Daftari, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Aisha Kigoda na Mwenyekiti wa Vijana CCM na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi.


Wengine ni Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ritha Mlaki, Lucy Mayenga (Vijana-CCM), Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu na Mbunge wa Viti Maalumu Singida, Martha Mlata.


Wabunge hao walionekana kutoamini kama kweli Amina hayuko tena duniani.


Katika hali iliyoonyesha kuwa watu wengi wameguswa na msiba huo, mamia walijitokeza kwa wingi nyumbani hapo kumuaga, hali iliyosababisha kuwekwa ulinzi wa kutosha wa Polisi walioongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow.


Hali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa wa watu ambao wengi ilibidi wabanane na wengine kukosa hata nafasi ya kusimama, hali iliyosababisha manung’uniko kwa baadhi yao wakidai eneo hilo halitoshi.


Pamoja na umati huo wa watu kuanzia asubuhi, baadhi ya viongozi walijitokeza kutoa pole pamoja na rambirambi zao kwa familia ya marehemu.


Baadhi ya viongozi hao ni Waziri Mkuu Mstaafu, Salim Ahmed Salim, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, Mufti Mkuu, Issa Shaaban bin Simba na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Muhammed Seif Khatib.


Wengine ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad, Waziri wa Usalama wa Raia, Bakari Mwapachu, Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Adam Kimbisa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Hemed Mkali.


Wakati huo huo, baba yake Amina, Hamisi Chifupa alisema haamini kama mwanawe ameuawa kwa sababu ya msimamo wake wa kupiga vita biashara ya dawa za kulevya.


Lakini alisema familia yake ilishangazwa na magonjwa ya ghafla yaliyosababisha kifo hicho.


Chifupa alisema jana kuwa yeye anaamini kuwa kifo cha mwanawe ni cha kawaida na hakukuwa na uzembe katika kumpatia tiba.


Kada huyo wa CCM alisema madaktari wa Hospitali wa Jeshi Lugalo walijitahidi kuokoa maisha ya Amina, lakini Mungu alimpenda zaidi akamchukua usiku wa Jumanne saa 2.45.


Aliyasema hayo nyumbani kwake Mikocheni Dar es Salaam saa kadhaa kabla mwili wa Amina haujafikishwa kwenye viwanja vya nyumba hiyo saa nane kamili mchana.


Kwa mujibu wa maelezo ya Chifupa, familia ilishangazwa na magonjwa ya ghafla yaliyoanza kumsumbua Amina, ukiwamo wa kisukari ikizingatiwa kuwa Amina hakuwahi kusema alikuwa akisumbuliwa na kisukari.


Alisema madaktari walikuwa hawalali katika juhudi za kuokoa maisha ya Amina, ikiwa ni pamoja na kujitahidi kushusha homa na kisukari, lakini haikuwezekana.


Chifupa alisema Amina alitoa kauli za kutabiri kifo chake, kwa kuwa alimwambia babu yake kuwa endapo angekufa, azikwe kijijini Lupembe wilayani Njombe, mkoani Iringa.


Aliwaambia waandishi wa habari kuwa watu wengi walipendekeza Amina azikwe Dar es Salaam, lakini familia imeamua kutekeleza matakwa ya marehemu hivyo atazikwa kama alivyoagiza kwenye makaburi ya Kiislamu.


Naye mume wa marehemu , Hemed Mpakanjia alisema haamini kama Amina amefariki dunia na pia haamini kama kuachana kwao kulisababisha kifo hicho.


“Kifo cha Amina ni pigo kubwa ambalo halijawahi kutokea katika maisha yangu, lakini inabidi nikubali kwa kuwa kazi ya Mungu haina makosa,” alisema.


Amina anatarajiwa kuzikwa kesho Lupembe, Njombe, Mkoa wa Iringa.


Souce: Habari Leo


Maelfu ya watu


Prayers


Mpakanjia akimwaga chozi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents