Habari

ARUSHA: Mwimbaji wa nyimbo za Injili kortini kwa tuhuma za kumuua mke wake kwa kumkata na shoka kichwani

ARUSHA: Mwimbaji wa nyimbo za Injili kortini kwa tuhuma za kumuua mke wake kwa kumkata na shoka kichwani

Mwimbaji nyimbo za injili mkoani Arusha, Mosses Pallangyo (29), anayetuhumiwa kumuua mkewe kwa kumkata na shoka kichwani, amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za mauaji ya kukusudia.

Wakili wa Serikali, Ahmed Khatibu, akimsomea hati ya mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Nestory Baro, alidai mshtakiwa anatuhumiwa kwa kosa la mauaji kinyume na sheria ya kanuni ya adhabu namba 196 sura 16 kama kilichofanyiwa marejeo mwaka 2002.

Katika kesi hiyo ya mauaji namba moja ya mwaka 2020, Pallangyo ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kilinga wilayani Arumeru, anadaiwa Desemba 25 mwaka jana akiwa nyumbani kwake, alimuua mkewe Mary Mushi (24) kwa kumkata na shoka kichwani.

Hakimu Mkazi Baro alimtaka mshtakiwa huyo kutokujibu lolote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na mshtakiwa amepelekwa mahabusu ya Gereza Kuu la Kisongo hadi Januari 28 kesi hiyo itakapotajwa.

Pallangyo alikamatwa Desemba 28 mwaka jana katika Kijiji cha Ilkiushin, Tarafa ya Muklata akiwa njiani kuelekea mafichoni nchini Kenya.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shanna, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa walilazimika kufanya operesheni siku tatu mfulululizo wilayani humo kumsaka mtuhumiwa huyo wakitumia mbinu ya mbwa ambayo ilikuwa ya kunusa na kumkamata baada ya kuweka mtego.

Chanzo Mtanzania.

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents