Habari

Asilimia 20 ya manunuzi serikalini ni hewa

Asilimia 20 ya fedha za serikali zinazotumika katika manunuzi ya vifaa mbalimbali zinapotea kwa njia ya rushwa. Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na…

Na Richard Makore



Asilimia 20 ya fedha za serikali zinazotumika katika manunuzi ya vifaa mbalimbali zinapotea kwa njia ya rushwa.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Mratibu wa mradi wa Millennum Challenge Threshold uliopo chini ya Shirika la Misaada la Marekani la USAID, Bw. Aaron Karnell.


Bw. Karnell alikuwa akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa kuwapatia mafunzo waandishi wa habari kuhusu sheria mpya ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.


Alisema kwa mujibu wa tafiti zinazofanywa na Mradi wa Millennum Challenge Threshold, asilimia hiyo inapotea kwa kuingia mifukoni mwa watu.


Alisema manunuzi mengi yanayofanywa kwenye vifaa vya serikali ni hewa na mengine huongezwa pesa na kuishia mikononi mwa wajanja na kwamba wenye kufanya hivyo ni wale waliopewa dhamana ya kununua vitu kwa ajili ya serikali.


Alisema wananchi wanatakiwa kubadili utamaduni katika kupambana na rushwa nchini ili kupunguza tatizo hilo.


Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi wa Shirika la Kitaifa la Msaada wa Sheria (Nola) Bw. James Kabakama alisema, mradi huo utagharimu zaidi ya Sh. 300 milioni.


Bw. Kabakama alisema, mafunzo hayo yataanza kutolewa kwa waandishi wa habari nchi nzima kuanzia mwezi huu na yatakuwa yanaendeshwa kwa kanda.


Alisema mradi huo umelenga kuwashirikisha wananchi kuhusiana na mabadiliko ya sheria hiyo iliyopitishwa na Bunge Aprili 16, 2007.


Aliongeza kuwa wananchi wanatakiwa kutoa taarifa kwa vyombo husika wanapoona mtu anapokea rushwa kwani wasipofanya hivyo na wao watahesabiwa kuwa wametenda kosa kisheria.


Aidha, alisema sheria hiyo mpya imeiongezea mamlaka Tume kuzuia na kupambana na rushwa nchini (TAKUKURU) ambapo kwa sasa ina uwezo wa kushughulikia makosa 24 yanayohusiana na rushwa badala ya manne iliyokuwa ikiyashughulikia hapo awali.


Alisema mafunzo hayo yatatolewa na watalaamu wao pamoja na maofisa kutoka TAKUKURU.


Sheria mpya ya kuzuia na kupambana na rushwa ilianza kutumika Julai Mosi mwaka huu.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents