Habari

Asilimia 54 ya wanaume hupigwa na wake zao – Utafiti

Wanaume wengi wanaopigwa na wake zao hawajitokezi kupata msaada wa kisheria kutokana na kuona aibu kuwa kufanya hivyo ni kujidhalilisha.

Na Joseph Mwendapole



Wanaume wengi wanaopigwa na wake zao hawajitokezi kupata msaada wa kisheria kutokana na kuona aibu kuwa kufanya hivyo ni kujidhalilisha.


Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Kituo cha Elimu na Mahusiano ya Kifamilia (FERC), Bi. Mwadawa Lugongo, wakati akizungumza na Nipashe kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu familia.


Alisema utafiti uliofanywa unaonyesha kuwa asilimia 54 ya wanaume wanapigwa na wake zao lakini hawatoi taarifa sehemu zinazohusika ili wapate msaada wa kisheria.


Kutokana na hali hiyo, alisema wanaume hao huamua kukaa kimya kwa muda mrefu hali inayowasababishia msongo wa mawazo.


Aidha, alisema wanaume wa aina hiyo wamegawanyika katika kada tofauti tofauti wakiwemo wa hali ya chini, wenye uwezo kimapato, wasio na uwezo, waliosoma na wasiosoma.


Alisema kiini halisi cha wanawake hao kuwapiga waume zao hakijulikani lakini wengi wa wanawake hulazimika kuwapiga waume zao kutokana na kuchoshwa na kukandamizwa kwa muda mrefu.


`Mwanamke anakandamizwa kwa muda mrefu anavumilia lakini hatimaye anachoka na akiamua kumpiga mwanaume anampiga kwelikweli mpaka mwenyewe anashangaa,` alisema.


Alisema kutokana na mateso wanayopata wanawake hupata msongo wa mawazo na hatimaye hufanya mambo yasiyo ya kawaida.


`Msongo wa mawazo ni ugonjwa mbaya sana na ni kama mtu amerukwa na akili, sasa anapoamua kumpiga mtu anakuwa na nguvu ambazo si zake,` alisema.


Alisema wakati hayo yakitokea, wanaume huwa hawarudishi vipigo kwa wake zao kwa kuwa kwa wakati huo wanakuwa wameshikwa na butwaa na kutoamini kinachotokea.


Bi. Lugongo alisema kutokuwepo kwa sera ya kitaifa inayoeleza majukumu ya kila mwanafamilia kumeathiri kwa kiasi kikubwa haki na mipaka ya utendaji katika ngazi hiyo muhimu.


Alisema, jamii imekuwa ikilichukulia utendaji na uwajibikaji katika ngazi ya familia kama jambo rahisi na kwamba hali hiyo imeongeza migogoro na maovu katika jamii.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents