Habari

Asilimia 90 ya wenye presha ya macho hawajijui

Serikali imesema ugonjwa wa shinikizo la macho ‘Glaucoma’, huathiri zaidi watu wenye umri wa miaka 40 na zaidi, na Tanzania inakadiriwa kuwa na asilimia 4.2 ya watu wenye umri zaidi ya miaka 40 wakiwa na ugonjwa huo ikiwa ni sawa na watu 440,000.

Aidha imesema kwa bahati mbaya asilimia 70 hadi 90 ya watu wenye ugonjwa huo, hawajijui. Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Faustine Ndugulile alisema hayo Dar es Salaam wakati akizungumzia wiki ya maadhimisho ya utoaji wa elimu kuhusu ugonjwa huo. Maadhimisho hayo yalianza Machi 11 na yataendelea hadi Machi 17, mwaka huu.

Glaucoma ndio chanzo kinachoongozakwa idadi ya watu wasioona. Alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na watu milioni 1.7 wenye matatizo ya kutokuona vizuri, kunakosababishwa na matatizo mbalimbali ikiwemo kuwa na mtoto wa jicho, upeo mdogo wa macho kuona na shinikizo la macho linalojulikana kitaalamu kama ‘Glaucoma’. Alisema katika mwaka 2017, ni watu 13,240 tu waliohudhuria kwenye vituo vya tiba wakiwa na tatizo la shinikizo la macho, idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na watu walio katika hatari ya kuwa na ugonjwa huo ambao wapo katika jamii na hawajagunduliwa.

“Ugonja huu wa shinikizo la macho ni moja kati ya kundi la magonjwa ya macho yanayoshambulia mshipa wa fahamu unaopeleka mawasiliano ya uoni kwenye ubongo yaani neva optiki ili kuweza kutafsiri kile kinachoonekana,” alisema Ndugulile.

Aliongeza kuwa ugonjwa huo, husababisha upofu kwa taratibu sana kwa siku hadi siku bila dalili yoyote katika hatua ya awali, na ili kuweza kugundua iwapo mtu ana ugonjwa huo, upo umuhimu wa kupima macho angalao mara moja kila mwaka, hasa kwa makundi yaliyo hatarini hata kama mtu haoni tatizo lolote kwenye macho.

“Ugonjwa huu hauna dalili zozote wakati wa hatua za awali na ndiyo maana wakati mwingine huitwa mwizi wa kimyakimya wa uwezo wa macho kuona, kwa kuwa ugonjwa huleta ulemavu wa kutokuona katika umri mdogo na taifa kupoteza nguvu kazi,” alisema. Kuhusu maadhimisho alisema kutakuwepo na shughuli za elimu ya afya ya macho pamoja na upimaji wa afya ya macho kwenye hospitali mbalimbali nchini na katika kliniki zote za macho na elimu pia itatolewa kuhusu ugonjwa huo.

Chanzo; Habarileo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents