Habari

Askari 99 wa Somalia wanaswa mkoani Mbeya

Askari 99 wa Jeshi la Somalia wamekamatwa mkoani Mbeya wakiwa katika harakati za kutaka kuvuka mpaka kuingia nchini Malawi.

Na Thobias Mwanakatwe, PST Mbeya



Askari 99 wa Jeshi la Somalia wamekamatwa mkoani Mbeya wakiwa katika harakati za kutaka kuvuka mpaka kuingia nchini Malawi.


Askari hao walikutwa wamejichimbia porini kando kando ya Mto Songwe ndani ya lori huku wakiwa wamefunikwa turubai mithili ya magunia yenye bidhaa.


Hata hivyo, mbinu hiyo ilibainika kufuatia baadhi ya watu waliosikia sauti za minong`ono zikitoka ndani ya `magunia` hayo yenye bidhaa na kutoa taarifa polisi.


Baada ya kukamatwa kwa askari hao na kuhojiwa, walidai kwamba wameingia nchini kutokana na kukimbia mapigano nchini kwao Somalia.


Wanajeshi hao walikamatwa juzi saa 1:00 jioni kando kando ya mto huo wakipanga mikakati ya namna ya kuvuka mpaka wa Tanzania kuingia nchini Malawi.


Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Bw. Suleiman Kova alisema jana kwamba, askari hao wa Kisomali, walikamatwa wakiwa ndani ya lori aina ya Scania lenye namba za usajili T286 ANM, mali ya Bw. Benson Nyemba, mkazi wa Njombe mkoani Iringa.


Alisema dereva wa lori hilo, Yassin Kansamba (33), anashikiliwa na polisi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa makosa ya kujihusisha na biashara ya kusafirisha binadamu.


Kamanda Kova alifafanua kuwa, kukamatwa kwa wanajeshi hao, kunafuatia taarifa za wananchi waliolishuku lori hilo lililoegeshwa porini huku ndani yake kukiwa na watu `kibao`.


Alisema wakati wananchi hao wakitaka kufahamu kulikoni, walisikia sauti za watu zikinong�ona kutoka ndani ya lori hilo wakiwa wamefunikwa turubai lililofungwa kamba mithili ya mizigo.


Alisema ndipo wananchi hao walipoliarifu Jeshi la Polisi ambapo polisi walikwenda katika eneo la tukio mara moja na kuwakamata watuhumiwa hao.


Kamanda Kova alisema kutokana na kukaa kwa muda mrefu bila kula, wanajeshi tisa waliishiwa nguvu na kupoteza fahamu na kupelekwa katika hospitali ya rufaa ya Mbeya kwa matibabu.


Alisema katika mahojiano na dereva wa lori hilo, ilibainika kuwa, wanajeshi hao kwa kushirikiana na watu wengine ambao ni raia wa hapa nchini, walikodi lori hilo kwa Sh. 500,000 ili liwafikishe mpakani waweze kuvuka na kuingia nchi jirani ya Malawi.


Dereva huyo alidai kuwa, aliwakuta askari hao wakiwa wamesimama kando kando ya barabara mjini Makambako mkoani Iringa na ndipo alipowachukua na kuwapeleka Vwawa Mbozi mkoani Mbeya ambako walitiwa mbaroni.


Dereva huyo alisema alikuwa anaongozwa na watu waliokuwa ndani ya gari dogo kwa njia ya simu kuhusu mahali alikotakiwa kuwapeleka askari hao.


Kamanda Kova alisema wanajeshi hao wanadai kwamba, walikuwa wanakimbia mapigano yanayoendelea katika eneo la Kusini mwa Somalia na kwamba waliamua kukimbia nchi ili kwenda kutafuta maisha huko Ulaya kupitia nchini Malawi.


Hata hivyo, alisema watu hao walipopekuliwa hawakukutwa na kitu chochote isipokuwa nguo walizokuwa wamevaa.


Lakini alisema Jeshi la Polisi linaendelea kuwasaka watu waliokuwa ndani ya gari dogo ambao wanadaiwa kuwaongoza askari hao mahali kwa kwenda.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu sakata hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Bw. John Mwakipesile, alisema kuna wimbi kubwa la wahamiaji haramu kutoka Ethiopia na Somalia wanaoingia mkoani Mbeya kinyume cha sheria.


Hata hivyo, alisema wimbi la wakimbizi kutoka nchini Ethiopia wanaoingia nchini, hasa mkoani Mbeya limepungua na kwamba tatizo kubwa sasa linaloukabili mkoa, ni uingiaji wa raia wa Somalia.


Alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na serikali, hasa polisi kutoa taarifa za watu wanaowashuku kuwa ni wageni haramu.


Wasomali hao 99 wakiwemo wale walilazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya, walitarajiwa kufikishwa mahakamani jana baada ya kukabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji mkoani hapa ili kujibu mashtaka ya kuingia nchini kinyume cha sheria.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents