Habari

Askari wa JWTZ adakwa akiuza risasi za Silaha nzito za kivita

ASKARI wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ametiwa mbaroni na Polisi eneo la Mlalakuwa Mwenge, Dar es Salaam, kwa kosa la kumuuzia risasi mkazi wa Kahama, mkoani Shinyanga.

Phillip Kabakama


ASKARI wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ametiwa mbaroni na Polisi eneo la Mlalakuwa Mwenge, Dar es Salaam, kwa kosa la kumuuzia risasi mkazi wa Kahama, mkoani Shinyanga.


Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kamanda Msaidizi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Liberatus Barlow alimtaja mwanajeshi huyo kuwa ni mwenye namba MT 80186 PT, Henry Mwisongo ambaye ni mkazi wa Keko Machungwa na askari wa JWTZ Kikosi cha 83 Kibaha.


Alikamatwa akimuuzia risasi Amosi Mwang’ombe (65), ambaye ni mkazi wa Kahama.


Barlow alisema Polisi walipata taarifa kutoka kwa mwananchi mwema na ndipo waliweka mtego na kuwanasa wahalifu hao wakiwa na risasi 2,593, na kati ya hizo, risasi 1,672 ni za bunduki aina ya G3 na 921 ni za SMG.


Alisema Polisi ilibidi wafanye ukaguzi nyumbani kwa Mwisongo, na kupata risasi nyingine nne, mbili za SMG na mbili za G3 pamoja na sare mbalimbali za JWTZ.


Wakati huo huo, Polisi wameyapata magari yaliyokuwa yameibwa kwa nyakati tofauti, ambako juzi Jumapili lilipatikana gari namba T 481 AAG Toyota Mark II iliyokutwa Kiluvya kwa Komba, mali ya Benedict Lukwembe (78) mstaafu wa JWTZ, mkazi wa Buza Kanisani lililoibwa Julai 15, mwaka huu, nyumbani kwake.


Katika tukio hilo, watu wawili walikamatwa ambao ni Daudi Lusingo (48) maarufu Tyson, ambaye gari hilo lilikutwa kwake na Elly Mnunga (22) mkazi wa Buza, ambaye alikiri kuiba gari hilo nyumbani kwa Benedict na lingeuzwa kwa Sh milioni mbili.


Kamishna Msaidizi Barlow alisema gari jingine lenye namba T 888 AKC aina ya Toyota Land Cruiser mali ya Checo Co-operation lililoibwa Sea Cliff, Julai 15, mwaka huu, lilipatikana maeneo ya Mbezi Beach nyumbani kwa Meja Ndosi likiwa limebandikwa namba T 257 AFL.
Alisema Polisi walifanya ukaguzi ndani ya nyumba hiyo na walikuta gari jingine dogo aina ya Toyota Sprinter lenye namba za usajili T 694 AFA, linaloshukiwa kuwa la wizi. Watuhumiwa katika tukio hilo ni Emmanuel Clement (33), Filbert Josef (20) na Kitoi Ndosi (23).


Alisema watuhumiwa walipohojiwa, walidai walitumwa kufanya kazi na mtu aitwaye Ernest Mushi, waliyemwacha kwenye baa ya Rainbow, Mbezi na askari walipomkamata, alidai gari hilo aliletewa na Alex Lyatuu (37). Lyatuu alikamatwa Kinondoni karibu na Vijana Hostel akiwa na gari lenye namba za usajili T 911 ADA Chaser, ambalo nalo linasadikiwa ni la wizi.


Alisema Alhamisi iliyopita saa 1:45 usiku, majambazi wapatao watano, wawili wakiwa na bastola na wengine mapanga, shoka na rungu waliwavamia walinzi Abasi Mustafa (59) na Abubakari Abdallah (32) wa nyumba ya kulala wageni ‘Aspec Resort’, iliyopo Sinza na kuwanyang’anya bunduki aina ya Shotgun ikiwa na risasi mbili.


Alisema kisha watu hao waliingia ndani ya nyumba hiyo na walimpora mhudumu Rosemary Josephat (23) shilingi 85,000 na simu mbili aina ya Nokia na walimkaba mteja aliyekuwa amepanga hapo, James Magwegwe na kumpora Sh 1,200,000 zilizokuwa kwenye bahasha na waliingia kwenye baa na kumpora Neema Magwegwe Sh 37,000.


Kwa mujibu wa Barlow, Polisi walifika na kukuta majambazi wamekwisha kutoweka na walimkamata mtuhumiwa Marystela Diomin (32) mkazi wa Lugalo Area E, baada ya kupata taarifa kutoka kwa James Magwegwe kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akiwasiliana kwa simu mara kwa mara na watu wasiofahamika akieleza kuwa yupo chumba namba 115.


Kamishna Msaidizi alisema watuhumiwa wa matukio yote hayo wanashikiliwa na polisi na watafikishwa mahakamani mara tu upelelezi utakapokamilika.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents