Habari

Askofu afungwa miaka 7

Askofu Peter Mutafungwa wa kanisa la Blessing Afrika la Marekani amehukumiwa kwenda jela miaka saba baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia Dola 1,454.38 za Marekani kupitia Mfuko wa Mwalimu Nyerere kwa njia ya udanganyifu.

Na Hellen Mwango


Askofu Peter Mutafungwa wa kanisa la Blessing Afrika la Marekani amehukumiwa kwenda jela miaka saba baada ya kupatikana na hatia ya kujipatia Dola 1,454.38 za Marekani kupitia Mfuko wa Mwalimu Nyerere kwa njia ya udanganyifu.


Sambamba na hukumu hiyo Askofu huyo pia ametakiwa kulipa fedha hizo wakati akitumikia kifungo.


Hukumu hiyo ilisomwa jana na Hakimu Mkazi Adolf Mahay wa mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa niaba ya Hakimu Mkazi, Neema Chusi, aliyesikiliza shauri hilo ambaye yupo masomoni.


Akitoa hukumu hiyo Hakimu Mahay alisema kuwa mshtakiwa alikuwa akikabiliwa na mashtaka 30, ambapo 15 kati ya hayo ni makosa ya kughushi na 14 ya kutoa hati zisizo halali.


Pia alisema kuwa mshtakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na shtaka la kujipatia huduma kwa njia ya udanganyifu.


Hata hivyo, alisema kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha mashtaka yote 29 kwa kushindwa kuonyesha jinsi mshtakiwa huyo alivyoghushi.


Aliongeza kuwa hata hivyo kwenye shtaka la kujipatia huduma kwa njia ya udanganyifu mahakama imemuona kuwa ana hatia.


Alisema kuwa hakuna ubishi kuwa mshtakiwa alijipatia tiketi ya kutoka Atlanta Marekani kuja nchini yenye namba 074220805013 ya Dola za Kimarekani 1,454.38 kutokana na michango ya Mfuko wa Mwalimu Nyerere ya watoto yatima na wajane kwa makubaliano kuwa angerudisha lakini hakufanya hivyo.


Baada ya mshtakiwa kutiwa hatiani, upande wa mashtaka uliomba mahakama iangalie nafasi ya mshtakiwa ambaye ni Askofu na hivyo alistahili kuonyesha wema kwa jamii lakini hakuwatendea haki watoto yatima na wajane na hivyo kusababisha wapoteza fedha.


Katika hukumu yake Hakimu Mahay alisema kuwa pamoja na ombi la upande wa mashtaka, lakini mahakama inazingatia suala lenyewe kwani mshtakiwa ni Askofu na alistahili kuonyesha mfano mzuri kama mapadre wa makanisa ya Katoliki ambao wanachukua misaada kwa ajili ya kusaidia jamii lakini yeye ameonyesha mfano mbaya wa kula fedha za watoto yatima.


Katika kesi ya msingi ilidaiwa kuwa Septemba 28, 2005 alijipatia tiketi ya dola za Kimarekani 1,454.38 kwa njia ya udanganyifu baada ya kuwadanganya kuwa angezilipa.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents