Siasa

Askofu ashitaki Ikulu

ULE mgogoro wa ushoga uliokuwa ukifukuta ndani ya Kanisa la Anglikana, sasa umetua kwa Rais Jakaya Kikwete. Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa Askofu Msaidizi wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dodoma, Ainea Kusenha, amemwandika barua Rais Jakaya Kikwete

na Fatma Gaffus, Dodoma

 

ULE mgogoro wa ushoga uliokuwa ukifukuta ndani ya Kanisa la Anglikana, sasa umetua kwa Rais Jakaya Kikwete. Habari zilizopatikana zinaeleza kuwa Askofu Msaidizi wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dodoma, Ainea Kusenha, amemwandika barua Rais Jakaya Kikwete, akimtaka awahimize viongozi wenzake ndani ya kanisa hilo, kumaliza haraka mgogoro huo.

 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, askofu huyo alisema amefikia uamuzi huo kwa kuwa ameona suala hilo linatishia amani katika jamii na nchi kwa ujumla.

 

Alisema athari za mgogoro huo ni kubwa kwa wote, kwani unahatarisha kuitumbukiza jamii katika janga lisilofaa, kwani ni kinyume cha maadili ya dini.

 

Kusenha alisema hayo yametokana na msimamo wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dodoma, Godfrey Mdimi Mhogolo, kutetea watu wanaojihusisha na ushoga, ambapo kumeleta mpasuko miongoni mwa waumini wa kanisa hilo mkoani humu na nchini.

 

Alisema yameibuka makundi ndani ya kanisa hilo kutokana na msimamo wa askofu huyo, kwani wapo watu wanaomuunga mkono wakati wengine wanapinga.

 

Lakini inaelekea askofu huyo alikuwa anatafuta namna ya kuufikisha mgogoro baina yake na askofu mwenzake huyo katika ngazi nyingine, kwani alilihusisha suala hilo na yeye kufukuzwa katika ofisi za dayosisi na kutakiwa kutoka katika nyumba ya dayosisi anayoishi.

 

Askofu huyo amefukuzwa katika ofisi na nyumba kutokana na madai ya ubadhirifu wa mali za kanisa, lakini mwenyewe ameapa kutoondoka katika nyumba anayoishi na hataacha kulitumikia kanisa mpaka sinodi itakapokaa na kuamua, kwa madai kuwa alichaguliwa na chombo hicho.

 

Akitetea uamuzi wake wa kumwandikia barua Rais Kikwete, alisema kuwa mgogoro huo hivi sasa si wa kanisa hilo pekee, bali ni mgogoro wa dunia.

 

Hata hivyo, Mwandishi Msaidizi wa Rais, Maura Mwingira, alipoulizwa hakuweza kuthibitisha kuwa barua hiyo imepokewa Ikulu, akisema kuwa yupo nje ya ofisi.

 

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Parishi za Kanisa la Anglikana unaopinga ushoga na usagaji, Mchungaji Christopher Milimo, alisema wao hawatalivumilia suala hilo la Askofu Mhogolo kuunga mkono masuala ya ushoga na kupokea misaada kutoka katika makanisa yanayounga mkono suala la ushoga, hasa ya Marekani.

 

Alisema kuanzia sasa wanajitenga na Askofu Mhogolo na kuwataka wanaounga mkono suala la ushoga na usagaji wamfuate askofu huyo na wale wasiounga mkono masuala hayo wamfuate Askofu Kusenha.

 

Alisema baadhi ya waumini ambao wamelivalia njuga suala hilo ni kutokana na umaskini, hivyo kuacha maagizo ya neno la Mungu na kufuata mambo yasiyofaa.

 

Mchungaji Milimo alisema wao hawatagawanyika kikanisa, bali wataendelea kutoa huduma ya neno la Mungu kwa wale watakaokuwa pamoja, ambao hawaungi mkono suala la ushoga.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents