Habari

Askofu Mokiwa: Siondoki Dayosisi ya Dar

Hali ya amani katika kanisa la Anglikana nchini, bado haiko vizuri baada ya Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa aliyevuliwa uaskofu kutoa msimamo wake na kudai kuwa yeye ni msafi, na ndio Askofu wa Dar es Salaam, huku akisema kuwa haondoki.

Askofu huyo aliyasema hayo Jumanne hii kwenye Kanisa la Anglikana Ilala alipozungumza na wanahabari. Alisema licha ya kusemwa mambo magumu, lakini yeye kama Askofu, kazi yake ni kuwaombea waliomkosea na hana matatizo nao, kwani amekwisha wasamehe.

“Siogopi kusema baba askofu kapotoka katika hili, ameshauriwa vibaya na washauri wake wa kisheria,”alisema Askofu Mokiwa huku akimtaja Profesa Palamagamba Kabudi kuwa mshauri wa kisheria wa askofu mkuu. Aidha Askofu Mokiwa aliugomea uamuzi huo, kwa maelezo kuwa mwajiri wake ni Sinodi ya Dar es Saalam, ambayo ndiyo yenye uamuzi wa kumfuta kazi na si askofu mkuu, au askofu mwingine yeyote wa kanisa hilo Tanzania.

Mokiwa alisema, “Alikuja na maaskari zaidi ya 12 ambao wamevaa sare, na wengine ambao hawakuvaa sare siwajui idadi yake, askofu mkuu alidai amekuja kuleta mrejesho wa halmashauri kuu, na matokeo yake akaishia kusema ameniondoa kwenye huduma ya uaskofu. Nimesema siondoki, na nimeona wanasema wataweka kila kitu hadharani, nawaambia hivi, mimi ni msafi na sina uchafu sehemu yoyote ile, wawe huru na amani kuanika madudu yangu kama yapo, waweke tu hadharani wala siogopi.”

Uamuzi wa kumvua uaskofu ulichukuliwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Askofu Mokiwa kugoma kujiuzulu, kama ilivyoshauriwa na Nyumba ya Maaskofu, ambayo ilimkuta na hatia ya kufuja mali za kanisa hilo na kukiuka maadili ya kichungaji, ambayo yalibainishwa kwenye ripoti ya uchunguzi iliyoundwa na kiongozi mkuu wa kanisa hilo nchini.

BY: Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents