Habari

ATC yafufuka rasmi

SHIRIKA la Ndege la Tanzania (ATC) limerudi katika huduma baada ya kuwa na ushirikiano na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) kwa muda mrefu na litaanza na ndege za kukodi.

Na Pendo Mtibuche, Dodoma


SHIRIKA la Ndege la Tanzania (ATC) limerudi katika huduma baada ya kuwa na ushirikiano na Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) kwa muda mrefu na litaanza na ndege za kukodi.


Akizungumza katika uzinduzi wa tiketi za ATC ambazo zilizinduliwa jana mjini hapa, Mwenyekiti wa Bodi ya ATC Balozi Mustapha Nyang’anyi, alisema ATC inaangalia njia za kupata ndege zitakazoanza kutoa huduma kwa njia ya kukodi.


Alisema wanahitaji ndege mpya na imara ambazo zitakuwa hazina umri mkubwa na zenye uwezo wa kubeba idadi kubwa ya watu bila kutumia kiasi kikubwa cha mafuta.


Alisema baadaye watanunua ndege zao mpya, ili kuendelea na huduma ambapo hivi sasa hata kama wangekuwa na fedha za kutosha kununua ndege, wasingepata mpaka 2012 hadi 2014 zitakapoanza kutengenezwa.


Balozi Nyang’anyi aliishukuru Serikali kwa kuwa pamoja nao na kuwajengea mazingira ya kukopesheka ambapo wakiwezeshwa kukopa wataboresha zaidi huduma za usafiri.


Alibainisha kuwa watarejesha nembo ya twiga kama alama ya Taifa katika ndege hizo na ambapo wameanza kutoa huduma katika mikoa waliyokuwa wakienda awali na safari za nje ya nchi na kwa sasa wanatafuta njia mpya.


Naye Mkurugenzi wa ATC, Bw. David Mataka, alisema baada ya kuingia ubia na SAA, tiketi za Tanzania ziliacha kutumika.


Alisema kabla ya ubia walikuwa wakitumia tiketi za Tanzania hali iliyosababisha wateja kutambua kuwa wanapata huduma kutoka katika shirika la ndege la Tanzania na kuitangaza nchi.


Alisema katika kipindi hicho, mapato yaliyotokana na usafirishaji yalikuwa yakienda moja kwa moja ATC, kupitia wakala wake, ambapo walikuwa na uwezo mkubwa wa kudhibiti mapato hayo yaliyokuwa yakiwafikia baada ya muda mfupi.


Alisema baada ya kuingia ubia na SAA kwa mujibu wa mikataba, waliacha kutumia tiketi zao na badala yake kutumia za SAA ambapo wateja walikuwa wakihudumiwa na SAA na ATC kutumika kama chombo cha kutolea huduma.


Alibainisha kuwa taarifa za mapato kutoka SAA zilikuwa zikicheleweshwa na kuwafikia baada ya miezi mwili au zaidi, ambapo pia hawakuwa na njia rahisi ya kuhakiki mapato hayo ambayo waliamini kuwa huenda yakawa sahihi.


Alisema kwa kuona kuwa huenda mapato ya ATCL yanapotea, waliamua kuingia katika mchakato wa kurudisha tiketi za ATC ambapo tiketi za SAA ziliacha kutumika ilipofikia Juni 30 mwaka huu.


Aliongeza kwamba wanaamini kwa kuachana na SAA watasimamia mapato yao kikamilifu na wataanza rasmi kufanya mahesabu yao ifikapo Agosti mwaka huu.


Alisema wataendesha utaratibu huo wa kusimamia mapato kwa kupitia wataalamu wa Merkator walioko Dubai kwa teknolojia ambayo itawaunganisha moja kwa moja na hivyo kuwapa uwezo wa kujua mtiririko wa mapato yao siku hadi siku.


Katika hafla hiyo ya uzinduzi wa tiketi, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, Bw. Mohamed Missanga na Mbunge wa Same, Bibi Anne Kilango-Malecela, walikabidhiwa tiketi za bure za ATC za kwenda Johanesburg na kurudi.


Akikabidhi tiketi hizo, Waziri wa Miundombinu, Bw. Andrew Chenge, aliitaka ATC kuwajali wateja na kuongeza ufanisi kwa watendaji wake kwa kuwaboreshea mazingira ya kazi.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents