Habari

ATC yatapeliwa sakata la mahujaji

UTATA umegubika mchakato mzima wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC) wa kukodi ndege za Mahujaji kwenda Makka, Saudia kutokana na taarifa kuonyesha shirika hilo limeingizwa mkenge.

Imeandaliwa na Muhibu Said, Ramadhani Semtawa na Salim Said (MUM)


UTATA umegubika mchakato mzima wa Shirika la Ndege Tanzania (ATC) wa kukodi ndege za Mahujaji kwenda Makka, Saudia kutokana na taarifa kuonyesha shirika hilo limeingizwa mkenge.


Mkenge huo unathibitishwa na wakala Kampuni ya Al wasam ya Saud Arabia kushindwa kupata kibali cha kutua na kuegesha ndege hizo za mahujaji kutoka Tanzania nchini humo.


Taarifa kutoka ndani ya ATC, zinaeleza kwamba wakala huyo alipaswa kutuma ndege Boing 747 ya Shirika la Rak Leasing la Dubai tangu Novemba 30, lakini haikufanya hivyo kwa kisingizio kwamba ilikuwa mbovu.


Pia wakala huyo alishindwa kupata ndege nyingine baada ya Rak Leasing (Jumbo Jet) yenye uwezo wa kubeba abiria 500, kuharibika.


Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Ndege nchini (ATC), Balozi Mustafa Nyang�anyi, alisema katika kushugulikia tatizo hilo walihisi kuwapo kwa utapeli uliochangia safari ya mahujaji hao kukwama na kulazimika kuripoti serikalini kuomba msaada zaidi.


Alipoulizwa na mwandishi wa gazeti hili uwanjani hapo jana iwapo serikali ilifuatilia utapeli uliotajwa na Balozi Nyang�anyi na hatua gani ilizochukua kuukabili, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro alikataa kuuzungumzia na kusema kwamba kinachofanywa na serikali hivi sasa ni kushughulikia safari ya mahujaji na si kupeleleza.


Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge pia miongoni mwa watu wanaohoji na kuwa na mashaka na wakala huyo akisema kuna uwezekano ATC ilifanyakazi na kampuni ambayo haina uwezo mkubwa.


Hata hivyo, Chenge alisema lazima hadhi ya serikali na nchi vilindwe na kusisitiza kwamba taarifa zote muhimu zitapatikana.


“Tatizo bado hatujajua, lakini wakati mwingine haya mambo ya kushirikiana na watu ambao …., wasioeleweka ni tatizo,” alisema Chenge.


Chenge alisisitiza jana kwamba, mahujaji wote walitarajiwa kuendelea kusafirishwa kwenda Saudi Arabia na kusema kasoro iliyojitokeza katika ndege ilikuwa ikipatiwa ufumbuzi wa haraka.


“Msimamo wa serikali ni kuhakikisha mahujaji wote wanawahi kwenda kuhiji, huo ndiyo msimamo wetu na sasa ndilo jambo kubwa tunahangaika nalo ili kuutimiza,” alisisitiza.


Chenge alisema ndege hiyo imekodiwa na ATC baada ya serikali kuingilia kati na si wakala.


Mkurugenzi Mkuu wa ATC alipoulizwa kwamba haoni shirika limetapeliwa kutokana na mchakato ulivyokwenda, alisema: ” Jamani naomba sasa hivi mniache haya mambo yaishe kwanza”.


“Nafikiri taarifa zote muhimu zitatolewa, lakini sasa tusubirini hili suala limalizike kwanza,” alisema kwa kifupi Mataka alipouzungumza na gazeti hili makao makuu ya ATC jijini Dares Salaam jana.


Mataka akiahidi kuzungumzia suala hilo kwa undani baadaye na taarifa zaidi kutoka ndani ya shirika hilo zinaeleza kwamba shughuli zote ikiwemo ndege hiyo ya kukodi ambayo ni Kampuni ya Global Aviation ya Afrika Kusini, zinafanywa na serikali.


Chanzo hicho ndani ya ATC kinaeleza kwamba Al wasam ambayo iliikabidhiwa jukumu hilo na shirika hilo kutafuta kibali cha kutua na ndege kama sheria za kimataifa zinavyoeleza, haikuweza kutimiza chochote.


“Wameshindwa kufanya hata kitu kimoja kilichomo katika makubaliano, kibali kimetafutwa na serikali kupitia ubalozi wa Saudi Arabia na ndege imekodiwa kutoka Global Aviation ya Afrika Kusini,” kiliongeza chanzo hicho.


Huku hali hiyo ya kutapeliwa ikiendelea, jana asubuhi juhudi za serikali za kuwaokoa mahujaji 698 waliokwama kuondoka nchini kwenda Makka, kutekeleza ibada ya Hijja zilkwama baada ya ndege iliyotarajiwa kusafarisha kundi la pili la mahujaji hao kupata tatizo la kiufundi.


Hali hiyo ilidhihirika saa 12, baada ya ndege hiyo aina ya DC 10, inayomilikiwa na kampuni ya Global Aviation ya Afrika Kusini kusafirisha kundi la kwanza la mahujaji 379 kwenda Madina, Saudi Arabia juzi saa 12:45 jioni na kurejea nchini jana saa 1:05 asubuhi.


Ndege hiyo ya mahujaji iliondoka jana saa 12:30 jioni na kwamba mahujaji waliobaki walitarajiwa kuchukuliwa leo saa 12:00 asubuhi kwa ndege hiyo ya DC 10.


Wakati tatizo hilo likitokea, serikali ya Saudi Arabia, imeipiga imeitoza ATC kfaini ya dola za Marekani 5,000 kutokana na kuchelewa kufika nchini humo katika muda uliopangwa.


Awali, tatizo la ndege hiyo, lilitangazwa kupitia vipaza sauti vya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 3:13 asubuhi, wakati mahujaji hao wakiwa wamejipanga kwenye foleni ya kuingia ndani ya ndege hiyo tayari kwa safari hiyo.


Kutokana na hali hiyo, mahujaji hao waliondolewa kwenye foleni hiyo na kuelezwa kuwa muda wa safari yao umeahirishwa hadi saa 2:00 usiku badala ya saa 3:00 asubuhi kama ilivyokuwa imepangwa. Hata hivyo, iliondoka kabla ya muda huo wa usiku.


Akizungumzia tatizo la ndege hiyo, Kandoro aliwaambia waandishi wa habari uwanjani hapo jana kuwa tatizo hilo liligundulika wakati wakijaza mafuta kwa ajili ya kuanza safari hiyo ambapo moja ya pampu zake zilizoko kwenye mfumo wa mafuta ilianza kuvuja maji ambayo yaliingia kwenye vyombo vya umeme.


�Mafundi walitoa kile chombo ili kujaribu kukausha maji lakini ikaonekana kuwa hakiwezi kurudishwa kwenye ndege, hivyo ikaamuliwa kiagizwe chombo kingine kipya kutoka makao makuu ya kampuni ya ndege hiyo iliyoko Afrika Kusini,� alisema Kandoro.


Hata hivyo, alisema chombo hicho kingeweza kuchelewa kufika nchini kutokana na ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini (South Africa Airways) hadi kufikia jana saa 5:00 asubuhi, ilikuwa imeshaondoka nchini humo kuja nchini.


Kutokana hali hiyo, Kandoro alisema chombo hicho kilitarajiwa kuwasili nchini jana saa 8:30 mchana na ndege ya ATC.


Alisema jana mchana, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Chenge, Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Dk Enos Bukuku na Mataka, walikutana kwa ajili ya kushughulikia utaratibu wa kupata ndege nyingine kwa ajili ya kuwasafirisha mahujaji hao.


Kandoro alisema mahujaji walioondoka nchini juzi kwenda Saudia, walifika salama na walipokelewa vizuri.


Katika hatua nyingine, Balozi Nyang�anyi alisema wamelipa faini ya dola za Kimarekani 5,000 kwa serikali ya Saudi Arabia kutokana na ndege hiyo kuchelewa kufika nchini humo katika muda uliopangwa.


Ndege hiyo iliyoondoka nchini jana saa 12:45 jioni, ilitakiwa kuwasili nchini nchini humo saa 8 mchana.


Alisema pia wanatarajia kulipa faini nyingine kutokana na ndege ya pili iliyotarajiwa kusafirisha kundi la pili la mahujaji hao kuchelewa kuingia Saudia na kwamba watahakikisha kuwa ndege ya tatu inaingia nchini humo katika muda unaotakiwa ili kukwepa kulipa faini zaidi.


Mwenyekiti wa taasisi ya kuratibu safari ya mahujaji ya Zanzibar Istiqama Hajj Trust, tawi la Dar es Salaam, Abdallah Mohamed alisema pamoja na matatizo ya ndege yaliyojitokeza, bado wana matumaini makubwa ya kwenda Makka kutekeleza ibada ya Hijja.


�Kama mahujaji wengine wameondoka basi na sisi tutaondoka,� alisema Mohamed.


Mmoja wa mahujaji ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alionyesha masikitiko yake kutokana na tatizo la ndege lililojitokeza na kusema kuwa:


�Kama mtu amepewa kibali cha kusafiria baada kukamilisha taratibu za safari na kupanga foleni ya kuingia kwenye ndege halafu unaombwa kurudi, baadaye kidogo mnaambiwa ndege ni mbovu, ni jambo linalotaka mazingatio na asitazamwe mtu tena, ila Mungu�.


Kiongozi wa Muda wa Mahujaji hao, Amiri Seifullah Rajabu alisema mahujaji wote walioondoka jana, wamefika salama na tayari wamepelekwa Makka kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hijja.


�Tutaendelea na utaratibu wetu mzuri tulioanza nao tangu juzi wa kuswali na kusubiri ili kumuomba Mwenyezi Mungu atusaidie,� alisema Amiri Seifullah.


Naye Saada Mfuruki, ambaye ni mmoja wa mahujaji hao, alisema hii ni mara yake ya kwanza kwenda kutekeleza ibada hiyo na mwaka huu ameambatana na mama yake aliyemleta kutoka Kenya.


�Nilijiandaa kwa muda mrefu kukamilisha gharama zote, lakini ratiba imevurugika. Tumekosa ibada zote za Madina na baadhi ya ibada za Makka,� alisema Saada.


Kutokana na hali hiyo aliiomba serikali na ATCL kufanya mipango itakayowezesha mahujaji kuondoka nchini, kwani ni aibu na udhalilishaji kwa Watanzania.


Katika hatua nyingine, mahujaji 22 kutoka nchi tano za Afrika, wamekwama uwanjani hapa kwa takriban siku sita zilizopita. Mahujaji hao waliowasili nchini wakitokea Nairobi, Kenya kwa ndege ya Shirika la Ndege la nchi hiyo (Kenya Airways) wiki iliyopita, wanatoka katika nchi za Mali, Guinea Bissau, Congo Brazzaville, Mauritius, Gambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).


Kiongozi wa Muda wa Mahujaji, Seifullah alithibitisha kukwama kwa mahujaji hao na kuwataja kuwa ni Diaby Mamadou, Konte M�pa, Samassa Aissata, Diawara Mody Camara Kadiata, Coulibaly Macire, Fofana Mamadou kutoka Mali.


Wengine, ni Conde Namory, Bah Thieno Soulemane, Diallo Mamadou, Cisse Baba na Barry Thierno Ibrahima (Guinea Bissau), Fofana Cheick, Nahamala, Souleyamane Diallo, Budiaka Djunga na Matondo Nsimba Fidele (Congo Brazzaville), Elhaiba Mohamed Lemine Sidi Ould Mohamed na Ould Ahmed Yahye (Mauritius) na Kebbeh Mohamed kutoka Gambia.


Kandoro na Balozi Nyang�anyi walikiri kukwama kwa mahujaji hao, lakini wakasema kuwa serikali na ATC, haziwezi kuwahudumia kwa kuwa hawakupitia katika mashirika yanayoratibu safari za mahujaji hapa nchini.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents