Siasa

AU yaagiza jeshi lake likang’oe waasi Comoro

UMOJA wa Afrika (AU) umeamuru kwenda kuung’oa uongozi uliojitangazia uhuru katika mojawapo ya visiwa vya Comoro, Anjouan, muda wowote kuanzia sasa.

Mgaya Kingoba aliyekuwa Addis Ababa, Ethiopia

 

UMOJA wa Afrika (AU) umeamuru kwenda kuung’oa uongozi uliojitangazia uhuru katika mojawapo ya visiwa vya Comoro, Anjouan, muda wowote kuanzia sasa.

 

“Tumekubaliana kuiondoa hii Serikali ya Kanali Mohammed Bakari, tumeamua ikaondolewe. Kazi hiyo imeachiwa Baraza la Amani na Usalama la Umoja,” Mwenyekiti wa AU, Rais Jakaya Kikwete aliwaambia waandishi wa habari wa Tanzania katika mkutano maalumu nao, baada ya kufunga mkutano huo mjini Addis Ababa juzi jioni.

 

Alisema uamuzi huo umefikiwa na wakuu wa nchi na viongozi wa serikali wa Umoja wa Afrika mwishoni mwa mkutano wao wa 10 uliofanyika mjini Addis Ababa na kufikia kilele chake juzi jioni. Sanjari na hilo, Umoja huo umesema kwamba hautaitambua serikali yoyote itakayoingia madarakani nchini Chad kinyume cha utaratibu wa kidemokrasia.

 

Mwenyekiti huyo mpya wa AU alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kiongozi huyo kujichukulia madaraka kinyume cha taratibu na kukataa kuondoka madarakani kwa hiari, licha ya kupewa muda mrefu wa kufanya hivyo na umoja huo. “Imebidi tuchukue uamuzi huo kwa sababu hii story imekuwa ya muda mrefu, kila siku habari ni ile ile. “Wallahi, haki ya Mungu nitaondoka tu,” alisema Rais Kikwete akimkariri Kanali Bakari.

 

Kisiwa cha Anjouan ambacho ni moja ya visiwa vinavyounda Comoro, kimejitangazia madaraka kwa muda sasa kutoka katika muungano huo wa visiwa vya Comoro, na hatua hiyo imekuwa ikileta hali ya wasiwasi kwa wakuu wa Comoro chini ya uongozi wa Rais Ahmed Abdallah Sambi.

 

Hivi sasa Comoro kuna jeshi la amani la Umoja wa Afrika (AU), ambalo miongoni mwa wanajeshi wake ni kutoka Tanzania. Inatarajiwa kuwa kiongozi huyo wa Anjouan ataondolewa muda si mrefu, katika uamuzi ambao utakuwa wa aina yake kufanywa na Umoja wa Afrika. Akizungumzia suala la Chad, Rais Kikwete alisema ni moja ya mambo yaliyozungumzwa kwa kina katika mkutano huo na imekubaliwa kuwa AU haitaitambua serikali itakayoingia nchini humo kinyume cha utaratibu, baada ya waasi kuripotiwa kutaka kumpindua Rais Idris Derby.

 

Alisema AU imewateua Rais wa Jamhuri ya Congo, Dennis Sassou-Nguesso na kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, kuongoza juhudi za kutatua mgogoro huo mpya katika Afrika. Rais Kikwete pia alisema AU imeamua kuwa mawaziri wa viwanda wa nchi hizo watakutana kujadili namna ya kuifanya Afrika ipige hatua katika masuala ya viwanda, hasa baada ya mjadala uliofanyika kutokana na kaulimbinu ya mkutano huo ya “Maendeleo ya Viwanda katika Afrika.”

 

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete ataongoza kamati ya marais 12 kushughulikia suala la mchakato wa uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Afrika na baadaye Muungano wa Afrika, baada ya kupokea ripoti maalumu ya wataalamu walioangalia namna ya muundo, mfumo na taasisi za AU, zitakavyofanya kazi.

 

Awali tume hiyo ilikuwa inaundwa na mawaziri 10, lakini sasa itakuwa na marais hao 12 ambao ni kutoka Ghana iliyokuwa Mwenyekiti wa AU kwa mwaka mmoja uliopita; Botswana, Cameroon, Gabon, Misri, Ethiopia, Libya, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini na Uganda.

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents