Michezo

Azam FC, Kagera zafikia muafaka 

Uongozi wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC na ule wa Kagera Sugar jana ulifikia muafaka kuhusu usajili wa mshambuliaji Mbaraka Yusuph.

Baada ya klabu hizo kukaa mezani, sasa Kagera Sugar imemruhusu rasmi mshambuliaji wake huyo wa zamani kukipiga kwa mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi na Ngao ya Jamii msimu uliopita.

Awali uongozi wa Kagera Sugar, ulimwekea pingamizi mshambuliaji huyo wakidai bado ana mkataba wa miaka mitatu ndani ya kikosi hicho, jambo ambalo zilizifanya pande zote mbili kukutana na kufikia muafaka.

Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa baada ya makubaliano hayo uongozi wa Kagera Sugar umeamua kwenda kuliondoa pingamizi waliloenda kumwekea Yusuph kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

“Baada ya mazungumzo ya muda mrefu kila kati ya Kagera na Azam lakini kila mmoja akivutia upande wake, hatimaye jana Kagera Sugar walikuja katika ofisi zetu za Azam na kuweza kufanya mazungumzo ya pamoja tunashukuru Mungu kwamba mazungumzo yamekwenda vizuri na utaratibu umekwenda vizuri.

“Kila siku Azam FC tunasema kwamba michezo ni udugu na vile vile ni familia, kwa hiyo katika mazungumzo kati ya Azam FC na Kagera Sugar ni kwamba Kagera Sugar imemruhusu rasmi mchezaji Mbaraka Yusuph Abeid kuweza kuichezea klabu ya Azam FC,” alisema.

Idd alisema kuwa mara baada ya klabu hiyo kuridhia, jana hiyo hiyo uongozi wa Kagera Sugar uliandika barua ya kumruhusu kuondoka (release letter), ambayo nakala moja imekwenda TFF, nyingine Azam FC na moja wamempa mchezaji huyo ikiwa ni kumruhusu na kwamba yuko huru kujiunga na mabingwa hao.

“Kinachoendelea ni kwamba Kagera Sugar wamekwenda kutoa pingamizi lao dhidi ya Azam FC juu ya mchezaji Mbaraka Yusuph baada ya mazungumzo ya jana kwenda vizuri, tunashukuru Mungu kuwa suala hili limekwenda vizuri, na tunawaambia masha biki wa Azam FC wasiwe na wasiwasi, Mbaraka Yusuph kwa sasa yupo Azam FC na amepata baraka zote za Kagera Sugar,” alisema.

B y Hamza Fumo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents