Michezo

Azam FC kuifuata Mwadui mkoani Shinyanga

Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuondoka alfajiri ya kesho siku ya Jumanee Jijini Dar es Salaam kuelekea mkoani Shinyanga tayari kabisa kuikabili Mwadui katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) inayotarajia kufanyika Oktoba 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.

Azam FC inauchukulia uzito mchezo huo na katika mikakati ya kuhakikisha inafanya vizuri, kikosi hicho kimepanga kuondoka na wachezaji wote iliowasajili msimu huu ambao wako fiti.

Baada ya kikosi hicho kucheza na Mwadui, kinatarajia kusalia Kanda ya Ziwa ili kufanya maandalizi ya mchezo mwingine wa ugenini dhidi ya Mbao, unaotarajia kufanyika mkoani Mwanza Oktoba 21 mwaka huu, ambao utahitimisha siku 12 za Azam FC katika mikoa hiyo miwili ya kanda hiyo.

Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii na Kombe la Mapinduzi msimu uliopita wanaodhaminiwa na maji safi ya Uhai Drinking Water, Benki bora nchini ya NMB na Tradegents, wanaelekea kucheza mechi hizo wakiwa na rekodi bora kabisa ndani ya ligi hiyo ikiwa ni miongoni mwa timu tatu za juu kileleni.

Timu hiyo ipo juu baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 11 sawa na Simba na Mtibwa Sugar zilizo juu yake kwa tofauti ya mabao ya kufunga, lakini Azam FC inabakia kuwa ndio timu pekee iliyofungwa bao moja pekee katika mechi tano za ligi zilizochezwa mpaka sasa.

 

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents