Michezo

Azam FC yaipiga Tanzania bila huruma

Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, asubuhi ya leo imeichapa timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 23 mabao 2-0, katika mchezo wa kirafiki uliofanyika uwanja wa nyasi za kawaida kwenye viunga vya Azam Complex.

Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa kwa pande zote mbili, ulikuwa ni mahususi kwa ajili ya kikosi cha Azam FC kujiweka kwenye ushindani ikiwemo maandalizi kuelekea mtanange ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Njombe Mji utakaofanyika Novemba 18 mwaka huu.

Mabao ya Azam FC yalifungwa na nahodha msaidizi Agrey Moris, dakika ya 41 aliyeunganisha kwa kichwa mpira wa faulo uliopigwa na winga Enock Atta, faulo hiyo iliyotokana na Ramadhan Singano, kufanyiwa madhambi.

Winga Joseph Mahundi aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Agyei, aliipatia Azam FC bao la pili dakika ya 48 akimalizia kwa mguu wake krosi safi aliyopenyezewa na beki wa kushoto Bruce Kangwa.

Katika mchezo huo, Kocha Mkuu Aristica Cioaba, aliweza kuwatumia wachezaji wake wote kikosini waliokuwa fiti.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitapumzika kesho Jumapili kabla ya kurejea mazoezini keshokutwa Jumatatu, kuendelea na maandalizi ya kuivaa Njombe Mji, mchezo utakofanyika Uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents