Michezo

Azam FC yarejea Dar baada ya ziara ya mikoani

Kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, tayari kimekaribia kuwasili jijini Dar es Salaam kikitokea mkoani Iringa.

Azam FC inatokea mkoani humo ilipocheza mchezo wa mwisho wa kirafiki katika mikoa ya nyanda za juu Kusini jana dhidi ya Lipuli na kuifunga mabao 4-0.

Awali Azam FC ikiwa kwenye kanda hiyo ilicheza mechi nyingine mbili, ilianza kwa kutoka suluhu dhidi ya Mbeya City mjini Mbeya kabla ya kupoteza kwa mabao 2-0 walipokipiga na Njombe Mji, mchezo uliofanyika mjini Makambako.

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz Meneja wa Azam FC, Phillip Alando, alisema mara baada ya kikosi hicho kurejea jijini Dar es Salaam leo, kitapumzika kwa siku mbili kabla ya kurejea tena mazoezini Julai 30 mwaka huu.

“Kikosi kitarejea mazoezini Julai 30, na wale wachezaji waliokuwa Taifa Stars, nao wataungana na wenzao, isipokuwa Mbaraka Yusuph na Shaaban Idd ambao bado wanaendelea na matibabu,” alisema.

Alando ameongeza kuwa “kikosi hicho kitafanya mazoezi ya pamoja kwa muda wa wiki moja ndani ya viunga vya Azam Complex kabla ya kutoka tena na kwenda kucheza mechi nne nyingine za kirafiki za maandalizi ya msimu ujao.

“Tunaendelea na taratibu, hatuwezi kusema tunakwenda wapi kwa sasa ila taarifa rasmi ni kuwa tutatoka tena na kwenda kucheza mechi nne za kirafiki baada ya kumaliza programu ya mazoezi kwa siku saba tukiwa Dar es Salaam ndani ya Azam Complex,” alisema.

Tayari ratiba ya msimu ujao ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) imeshatoka wiki chache zilizopita, ambapo Azam FC imepangwa kuanza na Ndanda katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara Agosti 26 mwaka huu.

By Hamza Fumo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents