Michezo

Azam FC yatumia saa 15 kuifuata Njombe Mji

Msafara wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, umewasili salama mkoani Njombe jana jioni, ukiwa tayari kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuvaana na Njombe Mji katika mchezo wa raundi ya 10 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Azam FC imetumia takribani saa 15 kuwasili mkoani humo, ambapo kilianza safari jijini Dar es Salaam saa 10 alfajiri.

Wakati kikosi hicho kikiwasili, taarifa kutoka Bodi ya Ligi hiyo, inaeleza kuwa mchezo kati ya wenyeji Njombe Mji na Azam FC, uliotarajiwa kufanyika Jumamosi hii umesogezwa mbele kwa siku moja hadi Jumapili.

Mchezo huo umesogezwa mbele ili kuwapa nafasi wadhamini wa matangazo ya televisheni, Kampuni ya Azam Media kupitia luninga yao ya Azam TV, kurusha mbashara mpambano huo.

Kikosi hicho kipo kwenye hali nzuri kabisa kuelekea mchezo huo unaotarajia kuwa mkali na wa aina yake, ambapo kitawakosa nyota wake watatu mabeki Daniel Amoah, Yakubu Mohammed na nahodha Himid Mao ‘Ninja’, ambao kila mmoja amekusanya kadi tatu za njano.

Wachezaji wa Azam FC waliowasili mkoani hapa ni makipa Razak Abalora, Mwadini Ally, Benedict Haule, mabeki ni Nahodha Msaidizi Agrey Moris, David Mwantika, Abdallah Kheri, Bruce Kangwa, Hamimu Karim, Swaleh Abdallah.

Viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Frank Domayo ‘Chumvi’, Salmin Hoza, Stephan Kingue, mawinga ni Enock Atta Agyei, Ramadhan Singano ‘Messi’, Joseph Mahundi, Idd Kipagwile, huku kwa upande wa washambuliaji wakiwa ni Mbaraka Yusuph, Wazir Junior, Yahya Zayd na Andrea Simchimba, aliyepandishwa wiki iliyopita akitokea timu ya vijana ya Azam FC (Azam U-20).

Azam FC hadi sasa imefanikiwa kucheza mechi tisa za ligi, ikishinda mechi tano na sare nne, ikiwa haijapoteza mchezo wowote huku ikiwa ndio timu pekee iliyoruhusu mabao machache baada ya kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili tu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents