Habari

Baada ya kumuua mumewe…Amzika kwenye ua na kuendelea na biashara

MWANAMKE wa tarafa ya Isimani, mkoani Iringa, Grace Lawa (35) anatuhumiwa kumuua mumewe Fedi Hongoli (40) na kumzika ndani ya ua wa nyumba yao.


NA PIUS KADINDE, IRINGA


MWANAMKE wa tarafa ya Isimani, mkoani Iringa, Grace Lawa (35) anatuhumiwa kumuua mumewe Fedi Hongoli (40) na kumzika ndani ya ua wa nyumba yao.
Pamoja na kumuua mumewe, Grace aliendelea kufanya biashara ya marehemu ya kuuza mifugo na aliwadanganya watu kwamba mumewe amesafiri.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Advocate Nyombi, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kudai mwanamke huyo ambaye amekamatwa, alimuua mumewe kwa kumpiga rungu kichwani.
Alisema tukio hilo lilitokea Machi 26, mwaka huu katika kijiji cha Ilambilole, Kata ya Nduli, Tarafa ya Isimani, Wilaya ya Iringa vijijini na kwamba tukio hilo liligundulika kutokana na harufu kali iliyokuwa ikitoka kwenye nyumba hiyo.
Kamanda Nyombi alisema wananchi wanaoishi jirani na eneo la tukio, walishitushwa na harufu hiyo ambayo ilitokana na kina cha ‘kaburi’ kuwa kifupi.
Alisema wananchi walitoa taarifa polisi ambao walifika eneo la tukio na kumkamata mwanamke huyo na baada ya kumbana alikiri kufanya mauaji hayo na kumzika mumewe huyo. Hata hivyo, hakueleza sababu za kutenda kitendo hicho.
Alisema polisi iliufukua mwili wa marehemu ambao ulikuwa umeanza kuoza ndani ya ua wa nyumba yao.
Kamanda Nyombi alisema mtuhumiwa Grace anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya mauaji.
Awali, wakiongea kwa nyakati tofauti wananchi wa kijiji cha Ilambilole walisema mwanaume huyo aliyeuawa alikuwa mfanyabiashara wa mifugo na kuwa walikuwa wanashangazwa kwa kutoonekana kwake kipindi kirefu.
Waliongeza kuwa, mifugo ambayo alikuwa anauza Hongoli alianza kuiuza mkewe na kuwa kitu ambacho hakikuwa cha kawaida na hivyo wananchi kwenda kumuulizia mumewe mara kwa mara.
Walisema kuwa Grace kila alipoulizwa, alikuwa akijibu kuwa mumewe amesafiri na ameachiwa mifugo hiyo aendelee kuiuza.
Waliendelea kuelezea kuwa kutokana na Grace kuchimba ‘kaburi’ kwenye ua wa nyumba yao likiwa na kina kifupi, harufu kali ilianza kutoka eneo la nyumba hiyo na ndipo watu wakataka kujua chanzo.


Source: Uhuru

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents