Baba adaiwa kuua mwanawe kwa 500/-

MKULIMA wa Kijiji cha Wendete wilayani Kahama mkoani Shinyanga
Philipo Maziku (48) amekamatwa na kufikishwa mahakamani akishitakiwa
kwa kosa la kumuua mwanae mwenye umri wa miaka 18 aliyemtuhumu kuiba
sh. 500

Na Suleiman Abeid, Shinyanga

MKULIMA wa Kijiji cha Wendete wilayani Kahama mkoani Shinyanga
Philipo Maziku (48) amekamatwa na kufikishwa mahakamani akishitakiwa
kwa kosa la kumuua mwanae mwenye umri wa miaka 18 aliyemtuhumu kuiba
sh. 500.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Shaibu Ibrahimu
alimtaja mtoto aliyeuawa kuwa ni Mariamu Philipo aliyekuwa akisoma
kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Ngogwa wilayani Kahama.

Alisema Maziku anatuhumiwa kumshambulia kwa kipigo mwanawe huyo kwa
kumpiga fimbo kichwani na miguuni ambapo alimjeruhi vibaya mnamo Juni
25, mwaka huu saa 6.15 usiku akimtuhumu kwa wizi wa sh. 500 zilizodaiwa
kuwa za mdogo wake aliyetajwa kwa jina la Stephano Philipo (14).

Hata hivyo baada ya kubaini kuwa mtoto huyo amejeruhiwa vibaya
hakuweza kumpeleka hospitali kupatiwa matibabu na badala yake alianza
kumtibu yeye mwenyewe nyumbani kwa kumpa dawa za kienyeji na kumchoma
sindano ya dawa aina ya PPF.

Hali ya mtoto huyo iliendelea kuwa mbaya na alifariki dunia mnamo
Julai 5, mwaka huu na kuzikwa siku hiyo hiyo hali ambayo wanakijiji
waliitilia shaka na kutoa taarifa polisi, ambapo mwili wake ulilazimika
kufukuliwa na kufanyiwa uchunguzi ili kubaini sababu ya kifo chake.

Katika tukio lingine askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ)
aliyetambuliwa kwa jina la Mohamed Chambia (50) mkazi wa kata ya
Kitangili Manispaa ya Shinyanga amekufa papo hapo baada ya kugongwa na
gari wakati akiendesha baiskeli.

Kamanda Ibrahimu alisema ajali hiyo ilitokea Julai 24, mwaka huu
saa 3.30 usiku katika barabara ya Shinyanga – Tinde ambapo hata hivyo
gari lililomgonga mwanajeshi huyo halikuweza kutambulika mara moja
kutokana na dereva wake kutoroka mara baada ya ajali hiyo.

 

Source: Majira 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents