Habari

`Baba ananitaka kimapenzi, ndo kisa nikampiga`

Msichana Elizabeth Dominic (26), anayekabiliwa na shtaka la kumshambulia baba yake mzazi, Daniel Zacharia, amedai kuwa baba yake amekuwa akimtaka kimapenzi kwa siku nyingi na alifikia hadi kuahidi kumpa shilingi milioni nne kama atakubali ombi lake.

Na Adam Fungamwango



Msichana Elizabeth Dominic (26), anayekabiliwa na shtaka la kumshambulia baba yake mzazi, Daniel Zacharia, amedai kuwa baba yake amekuwa akimtaka kimapenzi kwa siku nyingi na alifikia hadi kuahidi kumpa shilingi milioni nne kama atakubali ombi lake.


Kesi hiyo ipo mbele ya Hakimu Omari Mohamed wa Mahakama ya Mwanzo Magomeni, jijini Dar es Salaam, ambako Zacharia amemshitaki binti yake huyo akidai kwamba alimshambulia kwa ngumi, mateke na vibao.


Katika maelezo yake, Elizabeth alidai kuwa baba yake mzazi kwa muda mrefu amekuwa akimtaka kimapenzi na amewahi kumuonyesha shilingi milioni nne mikononi na kumwambia iwapo atakubali kufanya naye mapenzi atamkabidhi fedha hizo.


`Alikuwa na kiasi hicho na nilimuona nazo, nikazihesabu. Siyo utani� Akaniambia nilale naye, nikakataa. Hapo ndipo uhasama na baba yangu ulipoanza hadi leo hii,` alidai binti huyo, aliyeonekana kuudhika.


Msichana huyo aliendelea kudai kuwa baba yake pia amekuwa na wivu na wanaume wanaojitokeza kutaka kumuoa na amesababisha akataliwe na wachumba wawili.


`Nilikuwa naishi na mchumba wangu, alikuwa anataka kunioa. Siku moja baba akaja nyumbani, akamwambia aachane na mimi kwa sababu hata yeye anaweza kuishi nami na anachonifanyia hata yeye anakiweza na kwamba pia ubavu wa kunioa. Maneno hayo yalimkasirisha mchumba wangu.


`Alikereka na akawa kila siku ananituhumu kuwa nimewahi kulala na baba yangu na baadaye uhusiano wetu ukavunjika,` aliiambia mahakama Eliza, hali iliyosababisha jamaa zake wengi waliokuwa wamekuja kusikiliza shauri hilo kuanza kuondoka kwa aibu.


Binti huyo aliendelea kudai kuwa baada ya hapo alipata mwanaume mwingine.


Akawa anaishi naye kwa makubaliano kwamba wataoana, lakini baba yake akawa anamwandama kwa kumpeleka polisi mara kwa mara kwa kesi za kubambikiza hadi mwanaume huyo akaachana naye.


Mshtakiwa huyo alibainisha kuwa baba yake haoni aibu ya kumtamkia maneno hayo na kumpa ahadi za kumpangia chumba na kumnunulia vyombo vya ndani na kwamba watakuwa wakiishi kama mume na mke.


Aliongeza kuwa baba yake huyo aliachana na mama yake bado akiwa mdogo na akalelewa upande wa mama na ndiyo maana hata jina la ubini anatumia la upande wa mama yake kwa sababu hata baba yake amekuja kumjulia ukubwani kwa kuambiwa na mama yake.


Akijitetea juu ya kumshambulia baba yake, msichana huyo alisema alimpiga kibao kwa hasira, baada ya kumfuatafuata na maneno yasiyofaa lakini hakumpiga ngumi wala mateke kama inavyodaiwa kwenye hati ya mashitaka.


`Wala hakukuwa na ugomvi wa kufikia hatua hii,` alidai binti huyo.


Kwa upande wake, mlalamikaji Zacharia alidai kuwa maneno anayoyasema binti yake ni ya uzushi mtupu.


Akadai kwamba anampenda kama mtoto wake na si kama mpenzi na alikuwa anataka kumnunulia gari, lakini hatalinunua kwa sababu Elizabeth alimkodishia majambazi kumuua.


`Kwanza anasema mimi si baba yake. Alifikia hatua ya kunikodishia majambazi kuniua na kuchukua mali zangu,` alilalamika.


Hati ya mashtaka ya kesi hiyo inasemekana kwamba Julai 21 mwaka huu huko Magomeni Makuti, binti huyo alimshambulia baba yake mzazi kwa kumpiga ngumi na vibao.


Mshtakiwa amekana shtaka hilo na amedhaminiwa na mjomba wake hadi Agosti 15 kesi itakapoendelea tena.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents