Habari

Babu Seya awatisha wazazi

WAZAZI wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kyela, ambao watoto wao wamekiri kuwa walikuwa wakilawitiwa na watu wazima, akiwamo mfanyabiashara mmoja, sasa wameamua kuwahamisha watoto hao.

na Christopher Nyenyembe, Kyela

 

WAZAZI wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kyela, ambao watoto wao wamekiri kuwa walikuwa wakilawitiwa na watu wazima, akiwamo mfanyabiashara mmoja, sasa wameamua kuwahamisha watoto hao.

 
Wazazi hao wameamua pia kuwahamisha watoto yatima wawili ambao nao walikuwa wakifanyiwa vitendo hivyo. Watoto hao wote watapelekwa kwenye shule za pembezoni mwa mji wa Kyela.

 
Mmoja wa wazazi hao, Robert Mwaseba, alithibitisha hatua hiyo na kusema ameamua kumhamisha mtoto wake mwenye umri wa miaka 13, anayesoma darasa la nne.

 
Alisema kuwa kitendo hicho kimeifedhehesha familia yake na anajua kuwa mtoto huyo hawezi kujisikia vizuri kuendelea kusoma akiwa kwenye mazingira hayo.

 
Mzazi mwingine, George Kyamba, alisema tayari amekwishapeleka picha kwa ajili ya kuandaa uhamisho wa mtoto wake anayesoma darasa la sita katika shule hiyo.

 
“Kitendo hicho kimetutia uchungu mkubwa sisi wazazi, tayari nimekwisha peleka picha ili mwanangu ahamishwe kwani akibaki hapa hawezi kusoma… inatuuma sana,” alisema mzazi huo.

 
Kyamba alisema ameamua kujifungia chumbani na mtoto wake ambako atafanya naye maombi ya siku saba ili kumuomba Mungu amrudishie mwanawe mawazo mapya na hatamwadhibu mtoto wake kwa kuwa Mungu ndiye anayejua maovu ya wanadamu.

 
Alisema kuwa anajua kuwa mwanawe amekwisha kuathirika kisaikolojia na njia pekee iliyobaki ni kuketi naye na kumuomba Mungu kwa nia, aamini kuwa baada ya maombi hayo kijana huyo mwenye umri wa miaka 14, ataendelea vizuri na masomo.

 
Alipohojiwa, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Lothi Kilanga, alikiri kuwapo hatua za wazazi hao kuwahamisha watoto wao ambao watapelekwa kwenye Shule ya Msingi Mbugani na Mbogela, huku mwingine akihamishiwa mkoani Singida.

 
Alisema uamuzi huo umefikiwa na uongozi wa shule hiyo na wazazi ili kuwawezesha watoto hao kuendelea na masomo bila hofu katika mazingira mapya.

 
Kutokea kwa tukio hilo kumezusha hofu kubwa kwa wazazi wengine waliozungumza na Tanzania Daima kwa madai kuwa hivi sasa watakuwa wakizifuatilia kwa karibu nyendo za watoto wao kwa kuogopa kufanyiwa vitendo hivyo vichafu na watu wazima wenye matamanio ya aibu.

 
Kuwapo kwa tukio hilo kuliibuliwa na wazazi wa watoto wanaosoma katika shule hiyo baada ya kubaini kuwapo kwa vitendo vya ulawiti vinavyofanywa na watu wazima ambao wamekuwa wakiwadanganya wanafunzi hao kwa kuwapatia fedha.

 
Mbali ya tuhuma hizo kujitokeza, Jeshi la Polisi wilayani humo limejikuta katika lawama nzito baada ya wazazi hao kubaini kuwa njama kubwa zimefanyika ili kumficha mtuhumiwa mkuu anayedaiwa kuhusika, na hivyo kuwaondolea imani wazazi wa watoto hao.

 
Akizungumza kwa njia ya simu, Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, amekilaani kitendo hicho na akataka sheria ichukue mkondo wake.

 
Dk. Mwakyembe, ambaye alisema yupo safarini kuja jimboni humu, alitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wote waliojihusisha na vitendo hivyo.

 
Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents