Aisee DSTV!

BAJETI KUU 2019: Tozo 54 zafutwa, Nywele bandia kodi juu, Wafugaji na wakulima washushiwa neema

Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka mpya wa fedha 2019/20 jana imewasilishwa bungeni ambapo inakadiriwa kuwa ni Trilioni 33.1 ($14.3) na inalenga kuimarisha sekta ya uzalishaji na kilimo kwa lengo la kujenga uchumi wa viwanda.

Image result for bajeti 2019
Waziri Mpango

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma jana, amesema kipaumbele cha pili ni kulenga ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu.

Bajeti hiyo pia imefanya marekebisho mbalimbali ya tozo na kodi kwa lengo la kuondoa kero kwa wafanyabiashara na wazalishaji wa ndani.

Kwenye marekebisho hayo, Serikali imesamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), kwenye makasha yenye majokofu yanayotumika kwenye kilimo cha kisasa cha mboga mboga.

VILAINISHI VYA NDEGE

Dkt. Mpango alisema Serikali imetoa msamaha wa VAT kwa vilainishi vya ndege vinavyoingizwa nchini na waendeshaji wa ndani.

TAULO ZA KIKE 

Waziri Mpango amesema, Serikali imefuta msamaha wa VAT uliokuwa unatolewa kwenye taulo za kike kwa kuwa haujawezesha kupatikana kwa bidhaa hiyo muhimu kwa bei nafuu kwa walengwa na badala yake unawanufaisha wafanyabiashara.

Amesema Serikali imefanya marekebisho hayo kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332, ambapo imepunguza Kodi ya Mapato ya Makampuni kutoka asilimia 30 hadi 25 kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka 2019/20 hadi 2020/21 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya kuzalisha taulo za kike.

SAKATA LA UMEME ZANZIBAR

Dkt. Mpango amesema Serikali imepunguza VAT kutoka asilimia 18 hadi 0 kwenye huduma ya umeme unaouzwa kutoka Tanzania Bara kwenda visiwani Zanzibar.

KODI YA ZUIO 

Dkt. Mpango amesema Serikali imesamehe Kodi ya Zuio inayotozwa kwenye gharama zinazoambatana na mikopo kama ada za bima, gharama ya usimamizi na uandaaji wa mkopo.

NYWELE BANDIA 

Dkt. Mpango pia amesema Serikali itatoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye nywele bandia zinazotengenezwa ndani ya nchi na asilimia 25 zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.

MABOMBA, VIFAA VYA PLASTIKI

Serikali inapendekeza kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye bidhaa za mabomba na vifaa vya plastiki vinavyotumika kwenye ujenzi wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya maji kwa kuwa hivi sasa kuna viwanda vingi vyenye uwezo wa kuzalisha bidhaa hizo na kutosheleza mahitaji hapa nchini.

LESENI YA UDEREVA 

Serikali imependekeza kuongeza tozo ya leseni ya udereva kutoka Sh 40,000 hadi Sh 70,000 huku ikiongeza ada ya kadi ya usajili wa magari kutoka Sh 10,000 hadi Sh 50,000.

Kwa upande wa pikipiki za matairi matatu kutoka  Sh 10,000 hadi Sh 30,000 na pikipiki  kutoka Sh 10,000 hadi Sh 20,000.

USHURU WA FORODHA

Serikali imependekeza kupunguza ushuru wa forodha kutoka 10% hadi 0% kwenye malighafi ya kutengeneza taulo za watoto zinazotengenezwa hapa nchini kwa mwaka mmoja.

Kupunguza ushuru wa forodha kutoka kiwango cha asilimia 25 hadi asilimia 0 kwa mwaka mmoja kwenye vifaa vinavyotumika katika kukata, kung’arisha na kuongeza thamani ya madini ya vito.

Kwa upande mwingine, Waziri Mpango, amesema Serikali imefuta tozo 54 zinazotozwa na wizara, idara na taasisi zinazojitegemea ili kuondoa kero na urasimu kwa wafanyabiashara.

Dkt. Mpango amesema katika Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), anapendekeza kufuta tozo za kushikilia usajili wa dawa za chanjo inayotozwa kwa Dola za Marekani 150 (Sh 350,000)  dawa za mitishamba Dola 100 (Sh 230,000) , vitendanishi Dola 250 ( Sh 580,000) chakula Dola 100(230,000), vipukusi Sh. 100,000 na tozo za bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.

Amesema anapendeza kufuta tozo za kudurufu cheti cha usajili wa vitendanishi inayotozwa kwa kiasi cha Dola 100, tozo ya ukaguzi wa maduka mapya ya kuuzia vyakula Sh. 50,000, tozo ya usajili wa maduka ya rejereja ya dawa za mifugo ambayo ni kati ya Sh. 50,000 na 100,000.

Katika mamlaka hiyo, Dk, Mpango pia alisema anapendekeza kufuta tozo ya ukaguzi wa viwanda vya samaki iliyokuwa inatozwa kati ya Sh. 200,000 na 250,000, tozo ya ukaguzi wa maduka mapya ya samaki Sh. 50,000 na tozo ya leseni ya mwaka ya biashara kati ya Sh. 50,000 hadi Sh. 300,000.

Alisema hatua hiyo iliyolenga kuweka mazingira rafiki ya kibiashara na uwekezaji, inatarajiwa kupunguza mapato ya serikali kwa Sh. bilioni 2.5.

Kuhusu tozo za Shirika la Viwango (TBS), Dk. Mpango alisema anapendekeza kufuta tozo ya Sh. 50,000 ya maombi ya alama ya ubora, tozo ya nembo ya ubora ambayo ni asilimia 10 na 15 ya tozo ya gharama za mwanzo za ukaguzi wa ubora, tozo ya dhamana ya cheti cha kutumia nembo ya ubora na tozo ya asilimia 50 ya ununuzi wa fomu ya maombi ya bidhaa zinazotoka nje kwa bidhaa zote.

Tozo zingine zinazopendekezwa kufutwa katika shirika hilo ni za gharama za ugenzi ambazo hutozwa kulingana na umbali wa sehemu (mfano Dar es Salaam umbali wa Km tano ni Sh. 10,000) na tozo ya asilimia 0.2 ya gharama za mzigo na usafirishaji ya udhibiti wa vipodozi, vifaa tiba ikiwa ni pamoja na kondomu, mabomba ya sindano, glavu, pamba na bandeji.

Alisema hatua hiyo inayolenga kupunguza mzigo kwa wafanyabiashara, inatarajiwa kupunguza mapato ya serikali kwa Sh. bilioni 2.687.

Akizungumzia tozo za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk. Mpango alisema anapendekeza kufuta tozo ya huduma za kusitisha kutoa kibali cha awali na kutoa kibali kipya inayotozwa kwa kiwango cha Dola 50 na tozo ya huduma ya kubadilisha taarifa za kibali inayotozwa kwa kiwango cha Dola 50.

Pia, anapendekeza kufuta tozo ya Dola 500 kwa ajili ya usajili wa kampuni ya Wakala wa Forodha kipindi cha usajili na kufuta ada ya kulinda cheti cha usajili kwa wasambazaji wakubwa Dola 1,000 na wasambazaji wa kati Dola 500 kwa mwaka.

Aidha, Serikali imependekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Majumbani na Viwandani Sura 182 ambapo marekebisho yake yatahusisha  kutoza tozo ya Sh. 40,000 ya usajili wa kemikali kwa kila kemikali kwa kipindi cha usajili badala ya dola 20.

Pia kutoza kodi ya Sh. 200,000 kwa wafanyabiashara wakubwa na Sh. 50.000 kwa wajasiliamali wadogo kwa kila cheti cha usajili.

Zaidi amependekeza tozo ya Sh. 200,000 badala ya dola 100 kwa wafanyabiashara wakubwa na Sh. 50,000 kwa wafanyabiashara wadogo kwa usajili wa eneo la kuhifadhia kemikali.

Dk. Mpango alibainisha pendekezo la kutoza kodi ya Sh. 300,000 kwa siku kwa kila mtu ya kuchambua kemikali chakavu badala ya dola 300 (Sh 690,000).

“Kutoza tozo ya Sh. 200,000 ya kuanisha na kuidhinisha njia ya kuteketeza kemikali badala ya dola 500,” alieleza.

Kadhalika, serikali imependekeza kutoza tozo ya Sh. 300,000 kwa kila siku kwa mtu ya kusimamia kupakia, kusafirisha, kushusha na kuteketeza kemikali chakavu badala ya dola 300.

Aidha, kutoza tozo ya Sh. 300,000 ya ukaguzi wa maghala na sehemu za kuhifadhia kemikali badala ya dola 200.

Pia kutoza tozo ya Sh. 150,000 kwa kila siku kwa kila mtu kwa tathimini ya njia za usafirishaji na ukaguzi wa dharura badala ya dola 100.

Alisema kwenye mabadiliko hayo ya sheria, serikali imependekeza kutoza tozo ya Sh. 150,000 kwa siku kwa kila mtu kwa kusindika kemikali hatarishi badala ya dola 100.

Alisema ili kutimiza matakwa ya sheria ya kutumia fedha za Kitanzania, tozo zote zilizokuwa zinatozwa kwa dola, hivyo zitatozwa kwa fedha za Kitanzania isipokuwa shehena za kemikali zinazosafirishwa nje ya nchi.

Dk. Mpango alisema hatua hiyo inatarajiwa kupunguza mapato ya serikali kwa Tsh. milioni 450.

TOZO 16 MIFUGO ZAFUTWA

Waziri Mpango amesema, Serikali imependekeza kufuta tozo mbalimbali kwenye sekta ya mifugo ikiwamo tozo ya Tsh. 5000 ya vibali vya vyombo vya kusafirisha maziwa chini ya lita 51.

Pia kufuta tozo ya Tsh. 50,000 ya usajili wa vituo vya kukusanyia maziwa lita 201 kwa siku, tozo ya Sh. 5000 ya usajili wa wazalishaji wa maziwa chini ya lita 51 kwa siku na kufuta tozo ya Sh. 500,000 ya usajili wa wasambazaji wa pembejeo za maziwa.

Tozo nyingine iliyofutwa ni ya Tsh. 15,000 ya usajili wafugaji wadogo wa mifugo ya nyama na kufuta tozo ya Tsh. 50,000 ya usajili wa wafugaji wadogo wa mifugo ya nyama.

Pia kufuta tozo ya Tsh. 50,000 ya usajili wa wafugaji wa kati wa mifugo ya nyama, kufuta tozo ya Tsh. 75,000 ya usajili wafugaji wakubwa wa mifugo ya nyama na kufuta tozo ya Sh. 20,000 ya usajili wasimamiziwa minada ya awali.

Mpango amesema Serikali imependekeza kufuta tozo ya Sh. 30,000 ya usajili wasimamizi wa minada ya upili na mipakani pamoja na kufuta tozo ya Sh. 50,000 ya usajili wa minada ya upili na mpakani.

Kwa upande mwingine, tozo ya Tsh. 30,000 ya usajili wafanyabiashara wa minada ya awali na kufuta tozo ya Sh. 60,000 ya usajili wafanyabiashara wa minada ya upili na mipakani.

Mpango pia amependekeza kufuta tozo ya Tsh. 200 ya kibali cha kusafirisha kuku mkubwa nchini, hatua ambayo inatarajiwa kupunguza mapato ya serikali kwa Tsh. bilioni 16.6.

Related Articles

Back to top button
Bongo5

FREE
VIEW