Habari

BAKWATA yaionya serikali

Baraza Kuu la Waisilam Tanzania (BAKWATA), limeionya Serikali isiharakishe uundaji wa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki na badala yake ipokee na kuheshimu mapendekezo ya wananchi kabla ya kutoa maamuzi ya mwisho

Na Mwandishi Wa Nipashe

 
Baraza Kuu la Waisilam Tanzania (BAKWATA), limeionya Serikali isiharakishe uundaji wa Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki na badala yake ipokee na kuheshimu mapendekezo ya wananchi kabla ya kutoa maamuzi ya mwisho.

 

Naibu Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, alitoa onyo hilo jana mjini Morogoro, wakati akihutubia Baraza la Maulid lililofanyika kwenye ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu na kutangazwa moja kwa moja na Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD).

 

Maadhimisho ya Maulidi hufanywa kila mwaka na Waislamu wengi duniani kukumbuka kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W), aliyezaliwa Mecca, Saudi Arabia mwaka 571 baada ya Kristo.

 

�Serikali inalazimika kuwaeleza wananchi umuhimu wa shirikisho kabla ya kufanya maamuzi mazito kama haya� Na iheshimu mawazo ya raia, � alisema Sheikh Zubeir aliyekuwa anamwakilisha Mufti, Sheikh Issa Shaaban bin Simba.

 

Kadhalika alipongeza jitihada zinazoendelea za kukusanya maoni ya wananchi kutoka nchi wanachama wa shirikisho hilo za Kenya, Tanzania na Uganda.

 

Alisisitiza kuwa ili kufanikisha lengo hilo serikali ihakikishe wananchi wanafahamishwa na kuelimishwa juu ya masuala ya jamii, uchumi na siasa na umuhimu wake kwenye shirikisho.

 

�Tunakaribisha maoni na mapendekezo kutoka kwa Waislamu wote ili kuinua yaliyomo kwenye kutekelezaji wa uanzishwaji wa shirikisho, � alisema.

 

Kwa upande wa elimu, Naibu Mufti aliwataka Waislam kukitumia ipasavyo Chuo Kikuu cha Waislam cha mjini Morogoro na kukifanya kuwa kitovu cha kujiendeleza kitaaluma kwa waumini wake.

 

Alizungumzia suala la Homa ya Bonde la Ufa (RVF) na kuwataka waumini wake na Watanzania kwa ujumla, kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili kuudhibiti ugonjwa huu kwa nyakati hizo na kuuepuka siku zijazo.

 

Wageni wengine wa heshima katika Baraza la jana walikuwa ni Waziri Mkuu wa Kwanza Mstaafu Bw. Rashid Kawawa, ambaye alizungumzia umuhimu wa kujenga misingi ya amani, umoja na utulivu nchini.

 

�Ninafurahi kwamba nchi yetu ina utulivu, amani na usalama. Vitu hivi vinatupa fursa ya kuabudu Mwenyezi Mungu kikamilifu,� alisema Mzee Kawawa, maarufu kama Simba wa Vita.

 

Aliwaeleza waumini wa Kiislamu umuhimu wa kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali kupitia vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) ili kupigana na umaskini na kuboresha maisha yao.

 

�Tusikilize maagizo yanayotolewa na viongozi wetu tukitoa kipaumbele kwa suala la elimu kwenye kupambana na umaskini katika jamii zetu, � aliongeza Mzee Kawawa.

 

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa BAKWATA, anayeshughulikia Utawala, Sheikh Ramadhan Sawaka, alitangaza mpango wa chombo hicho wa kujenga msikiti mkuu utakaotumika kama kitovu cha shughuli zote za Kiisslam nchini.

 

Sheikh Sawaka kwa upande mwingine alipendekeza kujengwa kwa msikiti mkuu kwenye kiwanja cha Chang�ombe Dar es Salaam, ambao utakidhi mahitaji na huduma zote kama ukumbi wa sala, kituo cha afya, maktaba mahitaji mengine ya kijamii na kiuchumi.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents