Habari

Balali ana kwa ana na Kamati ya Bunge

KAMATI ya Bunge ya Fedha na Uchumi, imeanza kumhoji Gavana wa Benki Kuu (BoT), Daudi Balali, kuhusu matumizi ya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2005/2006.

na Tamali Vullu, Dodoma


KAMATI ya Bunge ya Fedha na Uchumi, imeanza kumhoji Gavana wa Benki Kuu (BoT), Daudi Balali, kuhusu matumizi ya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2005/2006.


Kazi hiyo ya kumhoji Balali, ilianza jana na leo wajumbe wa kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Handeni, Dk. Abdallah Kigoda (CCM) wanatarajia kuanza kuichambua kwa kina Ripoti ya Matumizi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) inayohusu matumizi ya BoT kwa mwaka huo iliyowasilishwa jana hiyo hiyo.


Taarifa kutoka kwa maofisa serikalini zinaeleza kuwa, ingawa ripoti hiyo ya CAG imetoa hati safi kwa BoT, bado kuna mambo mengi yanayoweza kuibua mjadala mkali wakati wa kikao cha kamati hiyo leo.


Aidha, mbali ya kutoa hati safi, CAG katika ripoti yake hiyo amehoji mambo kadhaa yakiwamo mahesabu ya madai ya malimbikizo ya malipo ya nje, yanayofikia sh 131,725,294,000.


Mbali ya hilo, taarifa hiyo ya CAG inaonyesha pia kuwapo kwa watu waliofanya kazi na BoT (suppliers) ambao hawakutoa hati halisi za kuthibitisha madai yao, jambo ambalo tayari linaonekana kuibua maswali.


Jambo jingine linaloweza kuibua mjadala kutokana na ripoti hiyo ni kufanyika kwa malipo makubwa ya ada ya huduma iliyolipwa kwa kampuni moja maarufu ya uwakili ya jijini Dar es Salaam.


Ripoti hiyo ya CAG, inaonyesha kuwa kampuni hiyo ya uwakili ililipwa ada inayofikia sh 2,990,221,907 kwa kuendesha kesi moja, hatua ambayo imeibua maswali mengi.


Katika ripoti yake hiyo, CAG alitaka suala hilo lichunguzwe na kueleza kuwa malipo kwa kampuni hiyo ya uwakili ni asilimia 13.5 ya fedha ambazo serikali inadaiwa ambazo ni sh bilioni 60.


CAG katika ripoti yake hiyo amependekeza utaratibu wa sasa wa kumfanya Gavana wa BoT kuwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi (audit committees) kubatilishwa.


Tukio la sasa la Balali kuwasilisha maelezo mbele ya kamati hiyo ya Bunge, limekuja wakati taasisi hiyo anayoiongoza na yeye mwenyewe wakikabiliwa na lundo la tuhuma zinazohusisha matumizi yenye kuleta shaka, ya mabilioni ya fedha.


Hata hivyo, pamoja na miito mbalimbali ya kumtaka ajiuzulu ili kupisha uchunguzi huru na wa haki, Balali ameshasema hatojiuzulu wadhifa wake, kwani madai ya ubadhirifu yanayotolewa dhidi yake ni uzushi na uongo mtupu.


Akizungumza na waandishi wa habari Julai 12 mwaka huu, Balali alisema: “Niko comfortable (muruwa), moyo wangu mweupe, ari yangu ya kazi iko juu, kwani tuhuma hizo ni uongo na uzushi mtupu na siwezi kujiuzulu kwa tuhuma zisizo na ushahidi.”


Ingawa hakutaja majina ya anaowatuhumu alipokutana na wandishi, Balali alisema tuhuma hizo zilizosambazwa kwenye mtandao wa intaneti, zimetokana na watu wenye ugomvi wa kibiashara na kusisitiza kuwa ni uzushi usio na chembe ya ushahidi.


“Tuhuma zote dhidi yangu ni za uongo mtupu. Kwanza sijui zimetoka wapi, nani mtunzi na kwanini amefanya hivyo, hilo tunawaachia wanaofanya uchunguzi na naamini siku moja atajulikana na ukweli utajulikana, lakini mimi siwezi kujiuzulu kwa mambo ya uzushi,” alisisitiza.


Aliwahusisha wafanyabiashara wakubwa na tuhuma hizo dhidi yake na kusema kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa na mikakati yao ya kibiashara kama walivyozoea zamani licha ya serikali kufanya mageuzi makubwa kiuchumi.


Alisema hivi sasa BoT imekuwa makini kuwabana wafanyabiashara wanaokopa kwenye mabenki makubwa ili walipe madeni yao, jambo ambalo zamani halikufanyika, kwani walikopa bila kurejesha mikopo, lakini sasa BoT imeamua kuwabana, jambo ambalo limewafanya wajenge chuki kati yao na BoT.


Balali alisema hata madai kuhusu kupandishwa kwa gharama za ujenzi wa minara pacha (Twin Tower), iliyojengwa kwa gharama kubwa, BoT bado inaendelea na mchakato wa kubaini gharama halisi ya majengo hayo na kuahidi kulitolea taarifa suala hilo baada ya kazi hiyo kukamilika.


Alisema kashfa ya upanuzi wa majengo ya BoT imekuwa ikiwakumba hata magavana waliopita, na hata kashfa ya ujenzi wa majengo hayo chini yake si jambo geni.


Hata hivyo, alikataa kutoa ufafanuzi kuhusu tuhuma za ubadhirifu kupitia akaunti ya madeni ya nje kwa maelezo kuwa jambo hilo lilishafafanuliwa na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji na hata Waziri Mkuu, Edward Lowassa.


Kutokana na tuhuma hizo, Waziri Meghji wakati akifanya majumuisho ya hoja yake, alisema serikali imeagiza kuanza kufanyika kwa uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa fedha katika akaunti ya madeni ya biashara ya nje zinazoikabili BoT.


Alikiri serikali kupata taarifa za kuwapo kwa vitendo vya rushwa na nyingine za matumizi mabaya ya fedha katika Benki Kuu.


Waziri Meghji alisema, tayari alikuwa ameshamwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali, kuanza uchunguzi kuhusu tuhuma hizo.


Meghji alisema, serikali ilikuwa ikitarajia kukamilisha kazi hiyo na taarifa kamili ya uchunguzi huo kutangazwa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.


Mbali ya BoT kutuhumiwa kutumia fedha nyingi kuliko inavyostahili katika ujenzi wa majengo yake mapya ya ‘minara miwili pacha’ (Twin Towers), kiasi cha dola za Marekani milioni 30.8 sawa na sh bilioni 40 kinatuhumiwa kufujwa katika akaunti ya madeni ya biashara ya nje.


Taarifa zinaonyesha kuwa, wakopeshaji wa kimataifa kutoka nchi 12 waliingia mkataba wa kusimamia akaunti hiyo na kampuni ya Kitanzania ijulikanayo kwa jina la Kagoda Agriculture Ltd kati ya Septemba na Novemba mwaka jana.


Uchunguzi wa awali wa wakaguzi wa nje wa mahesabu ya akaunti hiyo, unaonyesha kuwapo kwa mazingira yenye utata mkubwa unaozingira makubaliano kati ya wakopeshaji na kampuni hiyo iliyolipwa dola milioni 30.8.


Taarifa za awali za uchunguzi huo zinaonyesha kuwa, BoT ilifikia hatua ya kuipa kampuni hiyo fedha zote hizo ikidai kuingia mkataba na wakopeshaji hao katika mazingira ambayo nyaraka zilizopatikana zinaonyesha kuwa na hitilafu nyingi.


Miongoni mwa hitilafu zilizobainishwa katika uchunguzi wa awali ni, kukosekana kwa karatasi rasmi zenye majina ya kampuni hizo za kimataifa.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents