Tia Kitu. Pata Vituuz!

Balozi wa UN nchini Somalia, Nicholas Haysom atimuliwa kutokana na tuhuma hiziSerikali ya Somalia imemwamuru balozi wa Umoja wa Mataifa nchini humo Nicholas Haysom kuondoka baada ya kumtuhumu kuwa ameingilia masuala ya ndani ya taifa hilo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje wa nchi hiyo imesema Bw Haysom, ”hakaribishwi tena Somalia na hawezi kuendelea kuendesha shughuli zake nchini.”

Hatua hiyo imetokea baada ya mjumbe huyo kuandika barua akiuliza maswali mengi kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali wakati wa makabiliano yaliyotokea Baidoa katika jimbo la Kusini Magharibi wakati wa kumakatwa kwa naibu kiongozi wa zamani wa al-Shabab Sheikh Mukhtar Robow Abu Mansur mwezi uliopita.

Bw Haysom alikosoa kukamatwa na kuuawa kwa waandamanaji waliokuwa wakilalamikia kukamatwa kwa Bw Roobow mjini Baidoa kati ya 13 na 15 Desemba..

Kwa mujibu wa BBC, Haysom alimwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani wa Somalia Mohamed Abukar Islow na kuzungumzia uzito wa taarifa ambazo zilikuwa zimewahusisha wanajeshi wanaoungwa mkono na UN na kukamatwa kwa kiongozi huyo.Watu 15 waliuawa wakati wa mtafaruku uliotokea wakati huo.

Barua ya Bw Haysom pia ilizungumzia kukamatwa kwa watu 300 wanaodaiwa kushiriki maandamano kupinga kukamatwa kwa Robow.

Baadhi ya waandamanaji walizuiliwa kwa zaidi ya saa 48 na kisha kuachiliwa baadaye kati ya 18 na 22 Desemba.

Mjumbe huyo wa UN amesema kwamba usaidizi wa UN hutolewa kwa misingi ya kulinda haki za kibinadamu.

Hayo yakijiri, Umoja wa Ulaya umesitisha misaada kwa polisi wa serikali ya jimbo la Kusini Magharibi la Somalia kutokana na mzozo unaohusiana na kukamatwa kwa Bw Robow.

Kando na EU, mataifa ya Ujerumani na Uingereza pia yamesitisha msaada wao kwa polisi wa jimbo hilo la Kusini Magharibi.

Serikali ya Somalia ilikuwa imezuia Bw Robow kuwania kwenye uchaguzi wa urais wa jimbo hilo tarehe 19 Desemba ikisema bado anakabiliwa na vikwazo vya kimataifa.

Serikali hiyo ilimuunga mkono waziri wa zamani wa kawi Abdiasis Laftagaren ambaye alishinda.

Mzozo wa sasa unaendelea wakati ambapo kambi kuu ya Umoja wa Mataifa iliyo na usalama wa hali ya juu mjini Mogadishu ilishambuliwa kwa makombora.

Watu watatu walijeruhiwa baada ya wanamgambo kurusha makombora ambayo yalitua ndani ya kambi hiyo.Umoja wa Mataifa umetoa taarifa na kushutumu vikali shambulio hilo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, makombora saba yalianguka ndani ya kambi hiyo ya Umoja wa Mataifa na kujeruhi wafanyakazi wawili wa UN na mkandarasi mmoja.

“Hakuna aliyepata majeraha mabaya,” umoja huo umesema.

Kundi la wanamgambo wa Kiislamu la al-Shabaab limedai kuhusika.

Nicholas Haysom alishutumu shambulio hilo.

“Shambulio la leo la makombora katika kambi ya UN mjini Mogadishu huenda likawa ni ukiukaji wa sheria za kimataifa za kibinadamu, na nalaani vikali kitendo hiki kisichokuwa na sababu yoyote dhidi ya wafanyakazi wetu,” amesema Bw Haysom kupitia taarifa.

“Hakuna ajenda yoyote ya kisiasa inaweza kufanikishwa kupitia mashambulio ambayo moja kwa moja yanalenga mashirika ya kimataifa ambayo yanasaidia mchakato wa amani na kutia nguvu asasi za serikali nchini Somalia,” Nicholas Haysom ambaye ni mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia.

Watu walioshuhudia wanasema milipuko mikubwa ilisikika angani na moshi ukatanda angani kutoka kwenye baadhi ya majengo kwenye kambi hiyo.

Wanamgambo hao walio washirika wa mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda wamekuwa wakipigana kuiondoa madarakani serikali inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa.

Mashambulio yamekuwa yakitekelezwa mara kwa mara lakini huwa ni nadra kwa Umoja wa Mataifa kushambuliwa.

Ingawa al-Shabaab waliyakimbia maeneo ya mji mkuu waliyokuwa wanayadhibiti mwaka 2011 lakini bado wanadhiti maeneo mengine nje ya mji huo mkuu.

Eneo lililoshambuliwa hufahamika kama Halane Centre, na eneo hilo kunapatikana kambi kubwa zaidi ya kijeshi iliyo na wanajeshi wa nchi mbalimbali.

Kadhalika, kunapatikana mabalozi ya mataifa mengi ya Magharibi na makao makuu ya majeshi ya Umoja wa Afrika (Amisom) yanayopigana na al-Shabaab na kusaidia serikali ya nchi hiyo, pamoja na makao ya jeshi la Marekani.

By Ally Juma.Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW