Habari

Barabara nne kujengwa kuukabili msongamano

Halmashauri ya Manispaa ya Arusha ina mpango wa kujenga barabara nne mpya ili kuondoa msongamano wa magari katika maandalizi ya mkutano wa Lion Sullivan.

Na Catherine Meing`arana wa PST
Halmashauri ya Manispaa ya Arusha ina mpango wa kujenga barabara nne mpya ili kuondoa msongamano wa magari katika maandalizi ya mkutano wa Lion Sullivan.

 

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika mkoani hapa Juni, mwaka huu. Ujenzi huo ambao unatarajiwa kuanza katikati ya mwezi huu, utagharimu jumla ya Sh. milioni 803.

 

Hayo yalisemwa na Mbunge wa jimbo la Arusha mjini (CCM) Bw. Felix Mrema alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mkutano huo.

 

Aliongeza kuwa, lengo la ujenzi wa barabara hizo ni kuondoa tatizo la msongamano wa magari katikati ya Jiji.

 

Alizitaja barabara hizo kuwa ni NMC mpaka PPF (Njiro) inayokadiriwa kuwa na urefu wa kilometa mbili, ya pili ni kutoka Ngarenaro (Kwa father Babu) mpaka barabara kuu ya Arusha-Nairobi inayokadiriwa kuwa na urefu wa kilometa moja.

 

Hata hivyo, Bw. Mrema aliongeza kuwa, kutakuwa na barabara nyingine kutoka Maboksini mpaka Tanzania Little yenye urefu wa kilomita 1.4.

 

Katika hatua nyingine wananchi waliokuwa wakiishi katika eneo la Maboksini walihamishwa na serikali na kupelekwa Makuyuni wilayani Monduli ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo.

 

“Nashukuru wale wananchi waliokuwa katika eneo hilo kwa kukubali wenyewe kuachia eneo hilo, ambapo tumewatafutia eneo jingine Makuyuni na kwa hiari yao wamekubali kuhama,“ alisema Mrema.

 

Hata hivyo wakazi hao waliokuwa katika eneo hilo waliiambia PST kuwa, hawakukubali kuhama na kwamba serikali haikuwatendea haki kuwahamisha bila kuwalipa fidia yao.

 

Bw. Mrema alisema serikali imeandaa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya maboksini kwa kiwango cha lami na kwamba iwapo itakamilika itapunguza msongamano kwa kiwango kikubwa.

 

Barabara nyingine ni ya kutoka Njiro mpaka Mbauda inayotarajiwa kuwa na urefu wa kilometa 6.5 ambayo serikali imeiombea fedha kwa ajili ya kuwalipa fidia watakaoathiriwa na kwamba barabara hiyo itakamilishwa ujenzi wake kwa kiwango cha changarawe.

 

Alisema mpango huo ni wa muda mfupi, hasa kwa ajili ya ugeni huo wa Sullivan lakini pia alisema ina mpango wa kujenga barabara zenye urefu wa kilometa 140 kwa kiwango cha lami ndani ya manispaa.

 

Aidha, Bw. Mrema alitoa malori 80 ya moramu kama mchango wake katika ujenzi wa barabara hizo.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents