Bongo5 Makala

Barua ya wazi ya shabiki kwa Crazy GK: Tunamtaka yule wa enzi za ‘Sista Sista’ na ‘Hii Leo’

Mambo vipi Gwamaka? Nahisi bado sijasahau jina lako la mwanzo. Sijasahau kwasababu mimi ni shabiki wako mkubwa tangu unaanza muziki. Yeah nakukumbuka bado Miiko 10 ya rap uliyoitoa enzi zile, ilinisaidia kuwa rapper mzuri pia, yeah mimi pia ni rapper kama ulikuwa huna taarifa.

BSwb0VgIMAEKJp_

Rapper niliyekuwa kuwa inspired na wachanaji wengi wa Tanzania ukiwemo wewe. Naikumbuka albam yako, Nitakupa Nini. Ni miongoni mwa albam kali kabisa za hip hop kuwahi kutokea Tanzania. Ni wazi kuwa mimi na mashabiki wako wengi tulikuwa tumekumiss sana.

Jana uliachia single yako mpya, Baraka au Laana baada ya kukaa kimya kwa kipindi kirefu. Muda uliokuwa kimya, nafahamu ulienda chuo kuitafuta elimu na hatimaye hivi karibuni ulifanikiwa kutunikiwa shahada yako ya kwanza. Hongera sana bro kwakuwa sasa hivi hata kama muziki ukizingua, unayo taaluma yako tayari.

Nilifurahi sana jana pale washkaji zako wa siku nyingi wa East Coast Team walipoamua kukusindikiza kwenye siku muhimu ya jana. AY, Mwana FA, Snare, Buff G na Pauline Zongo, wote walikusindikiza hadi kwenye studio za Clouds FM kutambulisha wimbo huo kwenye kipindi cha XXL, ilikuwa mzuka sana bro. Nilibahatika kuona picha ukiwa na akina Fetty, B12, Mchomvu, Dj Zero na wengine mkipop champagne, dah! natamani name ningekuwepo pia.

bd199e3e0fdf11e39ad222000a1f97a2_7

Ilikuwa ni shangwe tu kwenye kipindi hicho hasa kwakuwa ulihit sana na nyimbo kama Sister Sister, Hii Leo, Tutakumbuka, Nitakufaje na zingine kibao, hivyo ulikuwa ukisubiriwa kwa hamu na mashabiki wako.

Wimbo wako mpya una mahadhi ya Kwaito. Nimekusikia ukiimba kuhusiana na matatizo yanayolikumba bara la Afrika yakiwemo magonjwa huku ukiuliza kama ni baraka ama laana kuzaliwa Afrika? Ungependa kupata jibu langu sasa hivi? Well, mimi sidhani kama ni laana kuzaliwa Afrika. Naona ni baraka tu kuzaliwa huku, hizo shida zilizopo zinavumilika na pia hata mabara mengine nayo yana shida zao na wanaitamani sana Afrika. Nitakuandikia barua nyingine kukueleza zaidi kuhusiana na mada hiyo.

Baraka au Laana, ni wimbo wa tofauti na Yuzo ameongeza utamu kwa sauti nzuri ya kuimba na kusindikizwa na gitaa lilichorazwa vizuri na Kameta, na kutengeneza kionjo chenye ladha ya nyimbo mfano wa zile za bondeni.

Wanasema ukweli unauma lakini ukiambiwa, utakufanya uwe huru na hivyo ningependa kukuambia ukweli kuwa mimi kama mmoja wa mashabiki wako wakubwa, sijapata kile nilichokuwa nakitarajia. Si kwasababu wimbo ni mbaya, lahasha, ni kwasababu sijakuzoea hivyo na sipendi sikio langu likuzoee hivyo.

Ningependa nikukumbushe kuwa miaka michache kabla hujawa kimya, ulikuwa umeshaanza kubadilisha mwelekeo na kufanya nyimbo tofauti na ulivyozoeleka. Nina uhakika kuwa ulianza kibadilika baada ya kuona kuwa enzi hizo muziki wa hip hop Tanzania ulikuwa haulipi, ama haukuwa wa kibiashara. Hivyo uliamua kufanya muziki wenye mrengo wa kuimba zaidi ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kuuzika, lakini sikumbuki kama ilikusaidia sana.

Naomba nikutoe wasiwasi kuwa katika kipindi ambacho umekuwa kimya, mambo yamebadilika sana. Woga wa wako kwamba hip hop hailipi unaanza kupitwa na wakati. Mfano mzuri ni mwana ECT mwenzako, Mwana FA. Ni lini umemsikia ametoa wimbo akiimba? FA ameendelea na style yake (hip hop) tangu atoe Ingekuwa Vipi hadi Kama Zamani.

FA ni mtu wa michano mpaka kesho lakini mbona mwaka jana alikuwa msanii wa tatu katika wasanii 10 walioingiza fedha nyingi kwenye mauzo ya miito ya simu? Mbona FA mwaka huu alifanya show ya hip hop tupu na watu na heshima zao wakanunua tiketi kwa shilingi 50,000 kwenda kumwangalia? Mbona FA ameendelea kupiga show kibao na umaarufu wake bado unaendelea kuongezeka? Hip Hop bado ni muziki wake na alishasema hata kwenye beat ya kapuka atachana tu hip hop, si umesikia alivyochana kwenye Bila Kukunja Goti? Michano ile ile!!

Hofu yako brother GK kufanya hip hop haina tena nguvu sasa hivi. Mashabiki tunakutaka GK wa enzi za Sister Sister ama Nitakufaje.

Yule GK anayerap kwa kigugumizi kwenye Hii Leo ‘Nikisema one na nyie machizi semeni two, nikisema three na nyie machizi semeni ohh, Ni King Crazy nasema wao wapo kivyao na sisi kwetu kivyetu’. Huyu ndiye GK tunayemtaka, hardcore rapper mwenye style yake mwenyewe, kwa style yako hakuna kama wewe bro. Ni rapper wangapi wenye style zao peke yao? Wa kuhesabu sana.

Huyu GK anayetuletea Kwaito anatuangusha mashabiki wake wa damu. Unatuangusha big time yaani!!!

Bro GK unahitaji kupata mdundo mkali kutoka ama kwa producer wako wa siku nyingi, John Mahundi ama kupata midundo mingine kutoka kwa maproducer wapya wakali wa beats hizo mathalan, Nah Reel. Nakumbuka niliongea na Mahundi mwaka huu na akanieleza kuwa ana kama nyimbo 3 mpya alizokufanyia. Sijui zikoje, lakini naamini John hawezi kukuangusha.

Napenda kusisitiza kuwa tunamtaka GK wa zamani, na kama ukiendelea kutuzingua na Kwaito zako, basi amini usiamini mimi na mashabiki wengine tutaandamana mji mzima, lol!! Sitanii lakini.

Pamoja sana Bro GK, nisikuchoshe na maneno mengi.

Ni mimi shabiki wako wa siku nyingi, Sky.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents