Burudani

BASATA yamfungia Nay wa Mitego kwa muda usiojulikana, akutwa na makosa matatu

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungia kwa kipindi kisichojulikana msanii wa muziki wa Hip Hop, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ hadi hapo litakapojiridhisha kwamba ametekeleza maagizo yote aliyopewa na baraza sambamba na yeye kubadilika katika kubuni kazi zenye maadili na zisizo dhalilisha watu wa kada mbalimbali.
Nay true boy

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa waandishi wa habari na Katibu Mkuu wa BASATA, Godfrey L. Mngereza, imemtaka rapper huyo kulipa faini ya shilingi milioni 1, na kufanya marekebisho ya mashairi ya wimbo wake wa ‘Pale Kati’, kufuata sheria, kanuni na taratibu za urasimishaji sekta ya Sanaa kwa maana ya kusajiliwa na BASATA na kuhakikisha wimbo wake umefuata taratibu zote.

Aidha, ameagizwa kuwaomba radhi watanzania kwa kutoa kazi ya muziki yenye kuvunja maadili na kudhalilisha watu wa kada mbalimbali hususani wanawake.

Maamuzi hayo yamefanyika kwa mujibu wa kifungu cha 4(2) cha sheria nambari 23 ya mwaka 1984, ikisomwa pamoja na kifungu cha 30(1)(2) na waraka wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo wa tarehe 16/7/2009 ambayo kwa sasa inafahamika kama Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Adhabu hizo zimetolewa baada ya BASATA kufanya kikao cha pamoja na msanii huyo siku ya jana.

Makosa aliyosomewa na yeye kuyakiri kwa maandishi ni pamoja na;

1. Kujihusisha na shughuli za Sanaa pasipo kusajiliwa na BASATA.

2. Kutoa wimbo wa “Pale Kati” na kuupakia katika mitandao ya kijamii bila kuuleta kufanyiwa uhakiki wa maudhui yake.

3. Maudhui ya wimbo wa ‘Pale Kati’ kwa sehemu kubwa hayafai kwa matumizi ya wazi na ni kinyume cha sheria za nchi na maadili ya mtanzania.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents