Habari

EWURA yatangaza kushuka kwa bei ya mafuta

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetoa bei kikomo ya bidhaa za mafuta aina ya petroli kwa mwezi Agosti, ambazo zimeendelea kushuka kwa miezi minne mfululizo kuanzia Aprili.

Tokeo la picha la mafuta sheli

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godwin Samwel, bei zinazoanza kutumika leo zimeshukwa kwa Sh36 na Sh44 kwa lita ya petrol na dizeli.

Taarifa hiyo inasema kwamba tofauti ni katika mafuta ya taa ambapo bei yake imeongezeka kwa Sh24 kwa lita, hali iliyosababishwa na kuongezeka kwa gharama ya usafirishaji wa bidhaa katika mfumo wa Uagizwaji wa Mafuta kwa Pamoja (BPS).

Wastani wa matumizi ya mafuta kwa siku ni lita milioni tano kwa mafuta ya dizeli, Lita milioni tatu kwa mafuta ya Petrol na Lita 100,000 kwa mafuta ya taa.

Kutokana na bei hizo mpya, kuanzia leo lita moja ya petrol katika jiji la Dar es Salaam itauzwa kwa Sh1,978 kutoka ilivyokua mwezi uliopita ya Sh2,014, wakati lita ya dizeli sasa itauzwa Sh1,830 kutoka Sh1,874 na mafuta ya taa yatapanda mpaka Sh1,830 kutoka Sh1,806 kwa lita kwa mwezi uliopita.

Mhandisi Samweli amesema kwa Mkoa wa Tanga, hakutakuwa na mabadiliko kwa petroli na dizeli kwa sababu hakuna mzigo uliopokelewa kupitia bandari ya Tanga kwa mwezi wa saba 2017. Hii itafanya bei za bidhaa hizo kwa mkoa huo kubaki kama zilivyokua kwa mwezi wa saba 2017.

“Pia, kwa kuwa hakuna bidhaa mpya ya mafuta ya taa iliyoingizwa kupitia bandari ya Tanga, wafanyabiashara wanashauriwa kuchukua bidhaa hiyo kutoka mkoa wa Dar es Salaam na pia, bei ya mafuta ya taa kwa mkoa wa Tanga zitategemea na gharama za mafuta ya taa yaliyopokelewa kupitia bandari ya Dar es Salaam na gharama za usafirishaji kutoka Dar es Salaam hadi Tanga”, amesema Mhandisi Samwel mbele ya waandishi wa habari jana.

Kwa upande wa waendesha magari ambao wangependa kupata bei za mafuta, wanaweza kupata bei kikomo kwa kutumia simu ya mkononi kwa kupiga *152*00# na kisha kufuata maelekezo.

Taarifa ya Ewura inasema pia Kampuni za kuuza mafuta ziko huru kuuza bidhaa zao katika bei ya ushindani yenye faida, isipokuwa wazingatie kuwa bei hizo hazizidi bei elekezi.

By Godfrey Mgallah

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents