Habari

Bei ya petroli yatisha

MAKALI ya bajeti yameanza kudhihirika wazi baada ya mafuta kupanda bei kwa kiasi kikubwa huku mamlaka za zenye jukumu la kusimamia suala hilo zikiwa kimya.

Shadrack Sagati


MAKALI ya bajeti yameanza kudhihirika wazi baada ya mafuta kupanda bei kwa kiasi kikubwa huku mamlaka za zenye jukumu la kusimamia suala hilo zikiwa kimya. Mamlaka hizo zinaonekana kushindwa kudhibiti hali hiyo licha ya matamshi ya serikali kuwa hakutakuwa na ongezeko kubwa katika bidhaa za petroli.


‘Kupaa’ huko kwa bei ya petroli kunakuja siku chache baada ya Waziri wa Fedha, Zakia Meghji kutangaza ongezeko la ushuru kwenye mafuta alilosema litafanya ongezeko la bei ya rejareja ya mafuta lisilozidi Sh 100. Lakini sasa hali ni tofauti.


Kuanzia Julai Mosi baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta nchini wamepandisha bei hata kufikia Sh 1,700 kwa lita katika baadhi ya maeneo. Pengine katika hali inayoonyesha ni ulanguzi mkubwa, baadhi ya vituo Dar es Salaam vimepandisha (kwa jana) bei ya petroli hadi kufikia Sh 1,550 kutoka Sh 1,280 kwa lita, bei ambayo ilikuwapo wakati bajeti ilipokuwa ikiwasilishwa bungeni Juni 14, mwaka huu.


Kutokana na hali hiyo, wananchi wameanza kuonja machungu ya ugumu wa maisha kwa nauli za usafiri kupanda kuanzia za daladala hadi mabasi ya mikoani. Kutoka Mbeya Merali Chawe anaripoti kuwa baadhi ya abiria waliokuwa wanasafiri kati ya Uyole na Soko-Matola katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya, jana waligoma kulipa nauli mpya iliyoanza kutozwa na makondakta wa daladala.


Mgogoro huo ulizuka baada ya kondakta wa gari namba za T 809 AHU aina ya Toyota Hiace, ambaye jina lake halikufahamika mara moja, kutangaza kuwa waliopanda kutoka Uyole nje kidogo ya Jiji walipe Sh 550 badala ya Sh 300 na wengine wa vituo vya njiani walipe Sh 300 badala ya Sh 200.


Kondakta huyo alisema kuwa wamepandisha nauli hiyo kutokana na ongezeko la bei ya mafuta, kauli ambayo ilipingwa na abiria katika gari hilo ambao walisema kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra)haijatangaza bei mpya.


Kupanda kwa nauli za mabasi ya abiria kumekwenda sanjari na kupanda kwa bei ya mafuta. Katika baadhi ya vituo vya kuuzia mafuta, petroli imekuwa ikiuzwa kati ya Sh 1,500 hadi Sh 1,700 kwa lita, wakati awali ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh 1,320 hadi Sh 1,350 kwa lita.


Dizeli katika baadhi ya vituo imekuwa ikiuzwa kati ya Sh 1,400 na Sh 1,550 wakati awali ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh 1,270 na Sh 1,300 kwa lita, huku baadhi ya vituo vikiwa vimefuta matangazo yanayoonyesha bei za mafuta.


Naye Frank Leonard anaripoti kutoka Iringa kuwa bei ya mafuta katika vituo mbalimbali mjini hapa imepanda kwa kati ya Sh 200 na Sh 300 kwa lita kabla na baada ya bajeti ya mwaka huu wa fedha kusomwa bungeni.


Utafiti uliofanywa na HabariLeo umebaini kwamba kabla ya bajeti hiyo kusomwa dizeli ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh 1,250 na Sh 1,280 kwa lita na mpaka jana ilikuwa imepanda hadi kufikia kati ya Sh 1,480 na Sh 1,500 kwa lita. Kwa petroli iliyokuwa ikiuzwa kati ya Sh 1,300 na Sh 1,350 kabla ya bajeti, imepanda hadi kufikia Sh 1,600 huku mafuta ya taa yaliyokuwa yakiuzwa kati ya Sh 800 na Sh 900 sasa yanauzwa Sh 1,000 kwa lita.


Naye Nashon Kennedy kutoka Mwanza anaripoti kuwa baadhi ya wananchi hapa wameendelea kuilalamikia bajeti ya serikali ya mwaka huu kutokana na kile walichokieleza kuwa ni kupandishwa kwa kodi ya mafuta na hivyo kusababisha bei ya mafuta kupanda, jambo ambalo wamesema wanashindwa kupata huduma muhimu za kila siku.


Wakizungumza na HabariLeo kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema Serikali ifikirie uwezekano wa kuzungumza na wafanyabiashara wa mafuta kuona uwezekano wa kupunguza bei za mafuta ambazo kwa sasa zimepanda kutoka Sh 1,300 hadi Sh 1,500 kwa lita moja ya dizeli na Sh 1,370 na Sh 1,550 hadi Sh 1,590 kwa lita moja ya petroli.


Pamoja na kupanda huko ambako kunaweza kutafsiriwa ni kwa ulanguzi katika maeneo yote (mafuta na nauli za magari) Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) pamoja na Wizara ya Fedha zimekuwa ‘bubu’. Jana, Ewura walipoombwa kuzungumzia hali hiyo, baadhi ya maofisa ambao walizungumza na gazeti hili Dar es Salaam hawakuwa tayari kulizungumzia kwa kina.


Baadaye ofisa mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Kashaza alisema mamlaka hiyo imekwisha kuanza kuchukua hatua na hivi karibuni itatoa taarifa. “Hilo suala linaweza kuzungumzwa vizuri na Kaimu Mkurugenzi (Kisyeri Machage), lakini hata hivyo ninavyofahamu kuna taarifa inaandaliwa na vyombo vya habari mtapewa hivi karibuni,” alisema Kashaza.


Baadaye Kisyeri alipatikana kupitia simu yake ya mkononi na akathibitisha kuwa imeandaliwa taarifa ambayo imetumwa kwa mkurugenzi mkuu aweze kuipitia. Alisema taarifa hiyo inaeleza wajibu wa Ewura katika kupanda kwa bei za mafuta. “Mkurugenzi akiipitisha tu tutaitoa wakati wowote kuanzia kesho,” alisema Kisyeri.


Waziri Meghji wakati anafunga mjadala wa bajeti bungeni alisisitiza umuhimu wa mamlaka zinazohusika kama Ewura pamoja na Sumatra kusimamia kwa karibu kuhakikisha wafanyabiashara hawajipandishii ovyo bei na nauli.


Sumatra nayo haijasema lolote wakati mabasi yanayokwenda mikoani yamekwisha kupandisha nauli bila hata kushauriana na mamlaka hiyo kama sheria na taratibu zinavyoagiza. Juzi Sumatra ilieleza kuwa ingetoa taarifa juu ya kupanda kwa nauli jana, lakini kwa mara nyingine jana ilisema itatoa taarifa kwa kuzungumza na vyombo vya habari vyote bila kutaja siku kamili.


Waziri Meghji jana hakupatikana kuzungumzia suala hilo na habari zilisema yuko nje ya nchi kikazi. Hata hivyo, mmoja wa manaibu wake, Mustapha Mkullo alikataa kulizungumzia suala hilo na badala yake akamwelekeza mwandishi aonane na Naibu Katibu Mkuu. “Naomba ukamwone Kijjah yeye yuko kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia suala hilo,” alisema Mkullo.


Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu huyo alipotafutwa kwa simu za ofisini kwake zilikuwa zinaita bila kuwa na majibu. Naye Katibu wa Baraza la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na Ewura, Michael Msigwa alisema wenye vituo wamepandisha bei zaidi ya kiwango ambacho Serikali ilikadiria.


Msigwa alisema mafuta yalitakiwa kupanda kwa Sh 120 kwa lita, lakini ongezeko la sasa hivi ni Sh 180 kwa lita. Alisema kwa sasa wakaguzi wa baraza hilo wanaendelea kufanya ukaguzi sehemu mbalimbali na baadaye watapeleka takwimu hizo kwa Ewura. “Unajua Ewura ndiyo wenye meno sisi ni washauri tu,” alisema Msigwa.


Mwenyekiti wa Baraza hilo, Profesa Jamiddu Katima alisema amekwisha kuandika barua kwa mkurugenzi wa Ewura kupata ufafanuzi juu ya kupanda kwa gharama hizo. Alisema baraza lake linachofanya ni kushauri tu, lakini mamlaka yenyewe ndio yenye kazi ya kudhibiti. “Tumesoma magazeti na kuona malalamiko ya wananchi, tayari nimewaandikia na tunasubiri majibu,” alisema.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents