Habari

Benki ya NMB yakabidhi mabati ya Mil. 17- kwa shule Kisarawe

Benki ya NMB imekabidhi msaada wa mabati 565 yenye thamani ya Shilingo. Milioni 17 kwa shule tatu za msingi Wilayani Kisarawe mkoani Pwani, uliopokelewa na Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo, aliyeukabidhi kwa Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo, Jokate Mwegelo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo (kushoto) wakipiga makofi baada ya kupokea mabati 565 yaliyotolewa na Benki ya NMB kwa ajili ya kuezekea vyumba vya madarasa vya shule za Kurui Chole, Msegamo na Kidugalo. Kulia ni Meneja wa NMB Kanda ya Mashariki, Dismas Prosper na Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Benedicto Baragomwa

Hafla ya kukabidhi msaaada huo ilifanyika leo, katika Shule ya Msingi Chanzige, mjini Kisarawe, huku shule zilizonufaika na msaada huo zikiwa ni Shule ya Msingi Kurui Chole (mabati 200), Msegamo (mabati 165) na Kidugalo (mabati 200) zilizoko Maneromango wilayani humo yote yakiwa na tahamani ya Sh. Milioni 17, ambazo ni sehemu ya asilimia moja ya faida yao kwa mwaka.

Akizungumza wakati akipokea mabati hayo, Waziri Jafo aliipongeza Benki ya NMB kwa namna inavyoacha alama kwa jamii, kutokana na misaada inayotoa katika vijiji, Kata, Tarafa, Wilaya na Mikoa mbalimbali hapa nchini kupitia Programu ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Aliitaka NMB kuendelea kusapoti maendeleo ya wilaya ya Kisarawe kama ilivyofanya kwa kutoa elimu na mikopo ya fedha kwa vikundi mbalimbali, pamoja na Tamasha la Mama Lishe Festival 2020, lililofanyika hapo mapema mwaka huu.

Naye Kaimu Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Benedict Baragomwa, aliishukuru Serikali ya Wilaya ya Kisarawe kwa kuitazama Benki yake kama mdau muhimu wa Elimu na Afya, na kwamba wamejitoa kila wapatapo maombi, ili kuunga mkono juhudi za Serikali.

‘‘Msaada huu ni sehemu ya utaratibu wetu wa kurejesha kwa jamii asilimia moja ya faida yetu kwa mwaka,ambapo mwaka huu tuilitenga Sh. Bilioni 1, ambayo inaendelea kutatua changamoto katika Sekta za Elimu, Afya na Majanga,’’ Baragomwa alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate, alimpongeza Waziri Jafo, ambaye ni Mbunge wa Kisarawe aliyemaliza muda wake na sasa akiwania tena, kwa namna anavyojitoa katika kuleta maendeleo wilayani mwake, na kwamba wananchi wanapaswa kujivunia uwepo wake.

‘‘Maboresho na mafanikio mbalimbali iliyonayo Kisarawe sasa, siri yake ni uongozi imara wa watu kama Waziri Jafo, ambaye ameipa mvuto kwa wadau kiasi cha kuzishawishi taasisi kama Benki ya NMB kujitoa kusaidia masuala mbalimbali ya kijamii hapa Kisarawe,’’ alisema Jokate.

Viongozi wengine waliohudhuria ni Katibu Tawala Kisarawe, Mwanana Msumi, Ofisa Elimu ya Msingi, Shomari Bane, huku NMB ikiwakilishwa na Meneja wa Kanda ya Mashariki, Dismas Prosper, na Meneja wa Tawi la Kisarawe, Justina Kikuli.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents