Bongo Movie

Bodi ya Filamu yawaamsha waigazaji wa mikoani kurudisha heshima ya filamu Tanzania

WARSHA kubwa iliyoandaliwa na Bodi ya filamu na michezo ya kuigiza imefanikiwa kufanyika Babati Mkoani Manyara kwa kuwashirikisha wasanii ambao walipongeza uwepo mafunzo hayo ambayo yanafungua njia mpya katika ukuaji wa tasnia ya filamu Tanzania.

Bodi ya filamu kwa ushirikiano wa Multichoice Tanzania imelenga kuwajengea uwezo wasanii wan chi nzima ili kutengeneza ajira kwa zaidi ya vijana wa Tanzania kupitia tasnia ya filamu, Katibu wa Bodi ya Filamu Bi. Joyce Fissoo anasema kuwa kuna wakati hutumika wasanii wa nje kisa ikiwa ukosefu wa taaluma.

Kuelekea katika ushindani kimataifa Bodi ya Filamu na Michezo ya kuigiza imegundua kuwa moja ya changamoto kubwa katika tasnia ya filamu ni ukosefu wa Weledi katika Nyanja tofauti tofauti, kwa kuliona hilo inaandaa mafunzo kwa wasanii na wadau wa filamu.

Bodi ya Filamu kwa kuwatumia wasomi wa masuala ya Filamu kutoka Vyuo vikuu Chuo kikuu cha Dar es salaam, Udom na Chuo cha Sanaa Bagamoyo (Tasuba) Katibu wa Bodi ya Filamu na Michezo ya kuigiza Bi. Joyce Fissoo amesema kuwa ili kufanikisha ubora na ukuaji wa Filamu kuna maeneo yanahitaji uboreshaji.

Kutokana na utafiti ambao umefanywa na kuona baadhi ya mapungufu katika utengenezaji wa filamu na kuona umuhimu wa kuwajengea uwezo wadau na wasanii wa filamu, Bodi imefanya semina katika mikoa ya Mwanza, Mara,Morogoro na Mikoa mingine pamoja na Manyara.

“Wadau wetu wamekuwa wakifanya vizuri katika uigizaji lakini kuna baadhi ya maeneo kama suala la Mikataba, Ubora wa filamu Bodi kwa kushirikiana na Wadau kama Multichoice kusaidia kuwafikia Wadau,”alisema Bi. Fissoo.

Mafunzo haya yanaratibiwa na Wizara Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kupitia Bodi ya Filamu na Michezo ya kuigiza imeendesha mafunzo kwa wasanii wa filamu Babati Mkoani Manyara huku wasanii kutoka katika katika Wilaya za Mkoa wa Manyara kushiriki na kupata mafunzo ya utengenezaji wa filamu.

Akifungua mafunzo hayo Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison G. Mwakyembe alisema kuwa Tanzania ni moja ya nchi barani Afrika yenye vipaji vingi katika massuala ya uigizaji lakini kuna vitu vidogo vidogo vinaharibu sifa ya kazi zetu hasa katika tafsiri.

Dkt. Mwakyembe katika ufunguzi wa mafunzo ya ubora wa filamu aliongozana na Mbunge wa Babati mjini Mh. Paulina Gekulu ambaye alimpongeza waziri kwa kutoa fursa kwa Mkoa wake wa Manyara huku akiwaomba wasanii washirikiane na ofisi ya Mbunge ili wawezeshe katika kufanikisha miradi yao.

Waziri anasema kuwa kuna wakati alikuwa Afrika ya Kusini kwa rafiki yake ambaye anapenda sana filamu za kitanzania naye kuungana katika kuangalia lakini ilipofika wakati wa kuangalia tafsiri kwa Lugha ya Kiingereza hapo ndio ilikuwa tatizo kwani kiingereza kilikuwa si fasaha na hiyo ndio dosari katika baadhi filamu.

Pia ni kushindwa kuingia mikataba ya kimaslahi katika Runinga ambazo hutumia kazi za filamu sehemu ambayo anaamini kuwa ingekuwa nafasi ya kujitengenezea kipato kwani kuna tofauti kubwa sana kati ya Tanzania na Uganda au Kenya ambao wanauza filamu zao kwa Dola 5000 na kuendelea huku Tanzania wakiuza kwa bei ya chini.

Hivyo Waziri anasisitiza wasanii kujengewa uwezo kitaluma ili wasiendelee kupata hasara na kulalamika kuhusu kushindwa kuvuna kulingana na jasho lao, kwa hilo atakuwa mkali zaidi lakini pia inapotokea fursa kwa ajili ya kujiendeleza basi wadau wasiwe wazito kujitokeza kushiriki.

Wasanii washiriki

Wasanii kutoka mkoa wa Manyara wameimwagia sifa Bodi ya filamu kwa kuwawezesha kupata elimu ya utengenezaji wa filamu kwani wamekuwa wakitengeneza filamu kwa kubahatisha kwani hawakuwa na Weledi huo kwa kuletewa wanazuoni waliobobea katika Filamu kwao ni bahati.

“Wakenya wamekuwa wakija sana hapa kwetu kwa ajili ya utengenezaji wa Makala wakiwa na wazungu sisi hatupati kitu baada ya kuanza mkuwabana walituwekea semina lakini hakuna kitu,”alisema Said Seif msanii.

Mwalim Gabriel akiongea kwa niaba ya wasanii wa Mkoa wa Manyara alisema kuwa Mafunzo waliyoyapata ni ya kiwango cha juu sana na hawajawahi kuyapata, hivyo watapiga hatua kubwa katika utengenezaji wa filamu kitalamu zaidi, na kuhaidi kuleta ushindani na wasanii wa Dar es salaam.

Akiongea katibu mtendaji wa Bodi ya Filamu Bi. Joyce Fissoo alisema kuwa wameamua kuwafuata wadau wa filamu Mkoani Manyara kwa sababu ya kuwajengea uwezo na kutumia rasimali za mkoa huo ambao unatumiwa sana na wageni katika kutengeneza filamu za Kiasili lakini bila wasanii kufaidika na fursa hizo.

“Wasanii wa ndani hutumia asilimia 4% tu kutengeneza filamu za kiasili huku mataifa ya nje wakitumia karibu asilimia 56% kutengeneza makala za asili hiyo inatokana na ukosefu wa taaluma ya filamu,”alisema Bi. Fissoo.

Mafunzo hayo yaliwezeshwa na Mwl. Richard Ndunguru, Dr. Vicensia Shule kutoka Idara ya Creative Arts Dept. UDSM (Chuo Kikuu Dar es salaam), Hajat Shani Kitogo mtaalam wa Lugha, Dr. Herbeth Makoye na Christa Komba kutoka Tasuba, Johnson Mshana kutoka DSTV, wengine ni mjumbe kutoka TAKUKURU, COSOTA na TRA.

Wakufunzi hawa walilenga jinsi ya uandishi wa mswada, Upigaji wa picha bora, Kujitangaza na kujeanga alama (Film Branding), Umuhimu wa Mikataba bora, Uongozaji wa filamu kiweledi, kazi bora zenye sifa ya kuonyeshwa katika runinga kubwa, matumizi sahihi ya Lugha ya Kiswahili katika filamu.

Mafunzo hayo yalifanyika kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 12 Julai 2018 kwa kufungwa na katibu mkuu wa wizara ya habari Utamaduni, Sanaa na michezo Bi. Susan Mlawi kwa kuwapatia vyeti washiriki na kuwapongeza kushiriki pamoja na wawezeshaji kuwajengea uwezo wasanii wa Mkoa wa Manyara.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents