Siasa

Bosi mpya BoT acharuka

Profesa Benno Ndulu, ambaye ndiye Gavana mpya wa Benki Kuu ya Tanzania, BoT, aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo nyeti baada ya aliyekuwepo kuboronga na kulitia taifa hasara ya mabilioni ya pesa, ametoa msimamo wake.

Na Abdul Mitumba, Mbezi Beach

 
Profesa Benno Ndulu, ambaye ndiye Gavana mpya wa Benki Kuu ya Tanzania, BoT, aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo nyeti baada ya aliyekuwepo kuboronga na kulitia taifa hasara ya mabilioni ya pesa, ametoa msimamo wake.

 

Katika hali inayoonyesha kwamba profesa huyo hatakuwa tayari kuyumbishwa na kigogo yeyote ili atende sawasawa na matakwa yake, amesema msimamo wake ni kusimamia haki, usawa na uadilifu na si zaidi ya hapo.

 

Gavana huyo ambaye ameshika nafasi hiyo huku Benki Kuu ya Tanzania ikinuka kutokana na kufunikwa na kashifa chungu nzima, amewahakikishia Watanzania kuwa jukumu lake la kwanza litakuwa kuhakikisha anatenda haki kwa kila mwananchi anayestahili kupata huduma ya chombo hicho kikubwa cha fedha nchini bila kujali uwezo wa mtu kiuchumi, cheo chake wala hadhi yake.

 

Profesa Ndulu alisema hayo jana usiku wakati wa hafla ya kumpongeza na kumuaga iliyoandaliwa na majirani zake wa eneo la Mbezi Beach, Jijini.

 

“Natambua wazi kuwa uteuzi wangu umekuja wakati ambapo taifa lina mtazamo tofauti dhidi ya BoT, lakini pia nikiri kuwa uteuzi huu ni changamoto kwangu na taifa kwa ujumla,“ Profesa Ndulu akawaeleza wageni waliohudhuria kwenye hafla hiyo.

 

Amesema kibarua chake kingine ndani ya taasisi hiyo kitakuwa kuyapa nafasi mambo muhimu yatakayosaidia kuinua na kujenga uchumi wa nchi ili kutoa nafasi kwa sekta mbalimbali za fedha kusonga mbele kwa kasi mpya.

 

Ameahidi kuendesha chombo hicho kwa haki, uadilifu na uwazi ili kurejesha imani ya Watanzania.

 

Kabla ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kuwa gavana wa BoT, nafasi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Dk.Daud Balali, ambaye uteuzi wake ulitenguliwa hivi karibuni kufuatia chombo hicho kukumbwa na kashfa ya matumizi mabaya ya fedha zinazokaridiwa kuwa zaidi ya Sh. Bilioni 133 za Kitanzania.

 

Mapema akizungumza katika hafla hiyo, msemaji wa majirani wa Profesa Ndulu, Bw. Sigfied Ng`itu, pamoja na kumpongeza pia alimkumbusha umuhimu wa kujali shida za watu wa kawaida ambao ndiyo wengi hapa nchini.

 

Bw.Ng`itu, ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ruangwa mkoani Lindi, alisema licha ukweli kuwa nafasi aliyopewa ni kubwa na inahitaji utulivu zaidi kufikia malengo, ni vyema pia akafahamu kwa sasa taifa linazizima na upotevu wa fedha za walipa kodi.

 

Katika hafla hiyo, Profesa Ndilu alipata fursa ya kuburudishwa na ngoma aina ya sangula kutoka mkoa wa Morogoro ambako ndiko anakotoka.

 

Wakati bosi huyo mpya wa BoT akitoa msimamo huo, taarifa za ndani kutoka Benki Kuu zinadai hivi sasa ni msheke mshike tu na kwamba watumishi kadhaa wanahaha wakihofia kuhusishwa na kashfa ya ulaji wa mabilioni.

 

Taarifa hizo zinadai kuwa wengi wa wanaohangaika ni wale waliokuwa karibu na aliyekuwa gavana na wana wasiwasi wa kupoteza vibarua hasa baada ya kubaini Profesa Ndulu hataki dili za uwani.

 

Source: Alasiri

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents