Michezo

Bosi wa SportPesa afurahishwa na mahaba ya Watanzania kwenye soka

Kwa kipindi cha wiki kadhaa zilizopita, nchi yetu ilikuwa katika utayari wa hali ya juu kushuhudia ziara ya kihistoria ya kimichezo ambapo tulipata kutembelewa na klabu maarufu ya Everton kutoka nchini Uingereza.

Ujio wa mabingwa hao mara tisa wa Ligi Kuu nchini Uingereza ulitokana na matunda ya mkataba wa udhamini kati yake na kampuni ya SportPesa ikiwa ni katika harakati zetu za kuinua sekta ya michezo kitaifa na kimataifa.

Tuliona umuhimu wa kuileta Everton nchini ili kuweza kuhakikisha kuwa mkataba wetu na klabu hiyo unalinufaisha soka la Tanzania na ndipo hapo tulipoanza mazungumzo na wenzetu hao kuona uwezekano wa wao kuja na ikiwezekana waweze kucheza mechi hapa nyumbani kama sehemu ya maandalizi yao ya msimu mpya wa ligi.

Halikuwa jambo jepesi kutokana na Tanzania kutokuwa na historia ya kutembelewa na klabu za nchini Uingereza, lakini tunashukuru kuwa wenzetu walituamini na kukubaliana na ombi letu hali ambayo ilitufanya tuumize vichwa kuona ni jinsi gani tutaitumia vyema fursa hiyo adhimu.

Kwa kuanzia, tuliamua kubuni michuano ya SportPesa Super Cup ili kuhakikisha kuwa vilabu ambavyo tuna ushirika navyo katika ukanda huu wa Afrika Mashariki vinapata fursa ya kushiriki katika ziara hiyo kikamilifu ambapo mshindi miongoni mwao ataweza kucheza na Everton.

Tulikuwa na wiki nzima ya mshikemshike pale uwanja wa Uhuru katika kuhakikisha kuwa tunampata bingwa wa SportPesa Super Cup na nipende kuvishukuru vilabu vyote nane vilivyoshiriki kwa kutoa ushirikiano licha ya kuwa na muda mfupi wa maandalizi.

Mashindano yalifana na kila mtu aliifurahia burudani licha ya kuwa na mapungufu ya hapa na pale ambayo tuliahidi tutayafanyia kazi ili yasiweze kujirudia mwakani.

Licha ya timu za Tanzania kushindwa kufanya vizuri kwenye michuano hiyo ili kupata fursa ya kucheza na Everton lakini bado tuliweza kuumiza vichwa na kuona ni jinsi gani Tanzania itaweza kunufaika na ujio wa magwiji hao nchini.

Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini pamoja na wenzetu wa Everton, tuliweza kubuni shughuli mbalimbali zenye manufaa kwa taifa ambazo pindi Everton watakapokuja nchini waweze kuzifanya katika kuhakikisha kuwa ile dhana yetu ya kuboresha soka inafanywa kwa vitendo.

Sote tumekuwa mashahidi katika wiki hizi mbili zilizopita jinsi ambavyo si tu kwamba tuliwaona wachezaji wa Everton kama vile Wayne Rooney, lakini pia tuliweza kushuhudia jinsi ambavyo semina mbalimbali za kuwajengea uwezo viongozi wa vilabu nchini, makocha, waaandishi wa habari pamoja na wachezaji wachanga zikiendeshwa na wataalamu kutoka Everton.

Kwa niaba ya SportPesa, tutakuwa wachoyo wa fadhila kama tutashindwa kuwashukuru wadau wote ambao kwa namna moja au nyingine walituunga mkono katika kuhakikisha kuwa maandalizi ya ziara hii yanafanikiwa.

Nipende kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dk, John Pombe Magufuli kwa kutoa baraka zake, lakini pia nipende kumshukuru Makamu wa Rais Mh. Mama Samia Suluhu Hassan kwa moyo wake wa utayari wa kuwapokea wageni wetu.

Lakini pia shukrani za dhati zimuendee Mh. Dk Harrison Mwakyembe kwa niaba ya Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa kuwa nasi bega kwa bega, Mh. Mwiguli Nchemba kwa niaba ya Wizara ya Mambo ya Ndani bila kulisahau Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wizara ya Utalii, Bodi ya Utalii nchini (TTB), Uhamiaji, Vyombo vya Usalama na wadau wengine wote ambao sitaweza kuwataja mmoja mmoja kwa majina.

Hakika mchango wenu ulikuwa na tija kubwa katika kuhakikisha kuwa nchi yetu inanufaika na ujio wa Everton na hatimaye kuweza kujitangaza vyema kimataifa si tu katika soka, bali pia katika utalii, ulinzi na usalama.

Lakini pia shukrani za dhati ziwaendee wapenzi wa mpira wa miguu nchini ambao mliweza kuwa na sisi tangu kwenye michuano ya SportPesa Super Cup hadi kwenye mchezo wa Everton dhidi ya Gor Mahia Julai 13 uwanja wa Taifa.

Sisi kama kampuni inayojidhatiti kuendeleza michezo nchini, tumefarijika sana na muitikio wenu mkubwa hususani siku ya mechi ambapo hadi wageni wetu wameshangazwa na jinsi ambavyo watanzania wanapenda soka.

Hakika kwa pamoja tumeweza kutengeneza historia ambayo haitakuja kufutika vizazi hadi vizazi, na tunaomba muendelee kutuunga mkono kwani ndio kwanza tumeanza na bado tuna nia ya dhati ya kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika anga la michezo kwa kukuza na kuviendeleza vipaji vilivyotukuka.

SportPesa imekuja kuleta matumaini mapya katika sekta ya michezo, na ziara ya Everton ilikuwa ni moja ya mambo mengine mengi yanayokuja huko mbeleni. Mmetuonesha nia ya dhati ya kutuunga mkono nasi tunaahidi kuwa nanyi bega kwa bega.

Umoja ndio ngao kuu katika safari yetu hii tuliyoianza kwa pamoja. Asanteni Tanzania.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents